Watumishi wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) wamejengewa uwezo wa kukabiliana na majanga mbalimbali ikiwemo ya moto pamoja na masuala ya kiusalama mahala pa kazi ili kuhakikisha mazingira salama ya utendaji kazi.
Mafunzo hayo yamefanyika Aprili 25 na 26, 2026 ofisi za LATRA Tanzania bara na kuhusisha wafanyakazi wote wa Mamlaka waliojifunza umuhimu wa kuzingatia usalama na kuwa na mazingira salama ya kazi kwa kuwa ni chachu ya kuongeza ufanisi na tija katika utoaji huduma kwa wadau wa sekta ya usafiri ardhini nchini.
Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Bw. David Elisha, Afisa Mkaguzi kutoka Wakala wa Usalama na Afya Mahala pa kazi (OSHA) na mwezeshaji wa mafunzo amesema kuwa watumishi wa LATRA, wamewaongezewa uelewa wa masuala yanayohusu vihatarishi vya kiusalama na athari zake zinavyoweza kujitokeza pindi wanapotekeleza majukumu yao pamoja na namna ya kukabiliana nazo.
“Watumishi hawa wameelezwa namna ya kujilinda na majanga pamoja na matumizi sahihi ya vifaa vya kukabiliana na majanga ikiwemo vifaa vya kuzimia moto kam vile matumizi ya mtungi wa gesi wa kuzima moto (fire extinguisher),” amesema Bw. Elisha.
Naye Mohamed Selungwi, Mkaguzi msaidizi wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Wilaya ya Ilala, Dar es Salaam amesema, wananchi wanatakiwa kuchukua tahadhari ya kujikinga pindi inapotokea majanga ya moto na wanashauriwa kutoa taarifa haraka kupitia namba za dharura ambazo ni 114 wakati wowote watakapohitaji msaada wa uokozi.
Kwa upande wake Bw. Athumani Kwikima, Mkurugenzi wa Huduma za Mamlaka LATRA amewasihi watumishi wa LATRA kuzingatia mafunzo waliyopatiwa na kuchukua tahadhari ya kulinda usalama wao na wale wanaowahudumia pindi wanapotekeleza majukumu ya Mamlaka.
“Niwaombe tuzingatie na tuyaishi yote tuliyofundishwa, naamini kupitia mafunzo haya sisi sote tumepata kufahamu mambo mengi na tukayafanyie kazi hasa pale tunapopata majanga yenye kuhatarisha usalama wetu,” amesema Bw. Kwikima.
Kwa upande wao watumishi walioshiriki mafunzo hayo wameeleza namna mafunzo hayo yamekuwa yenye manufaa makubwa kwao, yakiongeza uelewa na kujiamini katika kukabiliana na majanga yanayoweza kutokea mahala pa kazi.
Bw. Patel Ngereza, Kaimu Meneja Leseni Usafiri wa Barabara LATRA ameishukuru Menejimenti ya LATRA kwa kuandaa mafunzo hayo na kuwawezesha watumishi wote kushiriki na kujengewa uwezo wa kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na kuzingatia usalama mahala pa kazi nje ya kazi.
Mafunzo haya yamewapatia watumishi uelewa mpana kuhusu mbinu za kujikinga na vihatarishi vinavyoweza kusababisha ajali kazini, ikiwa ni pamoja na matumizi sahihi ya vifaa vya kuzimia moto, utambuzi wa maeneo hatarishi na hatua za haraka za kuchukua pindi dharura inapojitokeza

