Watumishi wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) wamepatiwa mafunzo ya Maadili katika Utumishi wa Umma ili kuchochea utendaji kazi unaozingatia Sheria, Kanuni na Taratibu zilizowekwa kwa kuongeza uwazi, usawa, uwajibikaji na uweledi wa kuwahudumia wateja.
Mafunzo hayo yamefanyika Aprili 25 na 26, 2026 na kufunguliwa na Mha. Eliud Kataraihya, Kaimu Mkurugenzi Mkuu LATRA na kuhusisha watumishi wa LATRA Dodoma, Dar es Salaam, Kilimanjaro na ofisi zote za LATRA Tanzania bara.
Mha. Kataraihya amesema kuwa, elimu ya maadili ni muhimu kwa kila mtumishi wa LATRA kuyapata kwa lengo la kuwawezesha watumishi kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu na uweledi wakati wote.
“Eliimu mnayopatiwa leo ni muhimu kwa kila mtumishi, kwa sababu maarifa mnayoyapata leo yatawakumbusha kuhusu umuhimu wa kuzingatia maadili mnapotekeleza majukumu yenu, hivyo kila mtumishi anapaswa kuwa makini kusikiliza mafunzo haya na kutekeleza yale yanayotakiwa kwa kuzingatia Sheria na Kanuni za utumishi wa umma” amesema Mha. Kataraihya.
Bi. Dorice Mwakibete, Kaimu Meneja Rasilimaliwatu na Utawala LATRA amesema, Maadili ni msingi muhimu wa kuhakikisha taasisi inajenga imani kwa wananchi pamoja na wadau wa sekta ya usafiri ardhini na kila mtumishi anapaswa kuwa mfano wa kuigwa kwa kuzingatia uwazi, uadilifu na uwajibikaji katika nafasi yake.
Naye Bi. Mariam Kuhenga, Mhadhiri wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC), ameipongeza Menejimenti ya LATRA kwa kuandaa na kuwapatia watumishi wake mafunzo ya maadili kwa kuwa ni muhimu kwa kila mtumishi wa umma kufahamu misingi ya kiutumishi inayowaongoza katika kazi zao za kila siku.
“Watumishi wa umma wanatakiwa kupata mafunzo ya maadili kila mwaka kwa lengo la kuwawezesha kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu kwasababu maadili ni suala la kisheria na kila mtumishi anapaswa kuwa muadilifu kwa kutii Kanuni na Sheria za utumishi wa umma,” amesema Bi. Kuhenga.
Kwa upande wao watumishi wa LATRA walioshiriki mafunzo hayo wameeleza kuwa, mafunzo hayo yamekuwa na manufaa makubwa kwao, hususan katika kuboresha utendaji kazi na elimu waliyoipata itaenda kuwawezesha kutekeleza majukumu yao kwa uweledi zaidi na kuongeza ufanisi wanapohudumia wananchi.
LATRA inaendelea kuweka mkazo katika kujenga utamaduni wa uwajibikaji na maadili bora miongoni mwa watumishi wake, ikiwa ni sehemu ya dhamira ya Serikali ya kuboresha huduma za usafiri ardhini nchini.

