Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) imeendelea kuimarisha udhibiti wa huduma za usafiri wa mabasi ya mijini (daladala) kwa wanafunzi, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuhakikisha wanapata huduma salama, nafuu na ya uhakika wanapokwenda na kurudi kutoka shuleni.
Hayo yamebainishwa na Bw. Denis Daudi, Afisa Leseni na Usajili LATRA Machi 24, 2026 jijini Dar es Salaam na kueleza kuwa Mamlaka imechukua hatua mbalimbali ikiwemo kutoa elimu kwa wadau wa usafirishaji ili kuongeza uelewa kuhusu umuhimu wa kuwasafirisha wanafunzi kwa wakati na kwa kuzingatia Sheria Kanuni na Taratibu zilizowekwa na Mamlaka.
“Tumekuwa tukitoa elimu kwa wadau wa usafirishaji ambao wanatoa huduma hii ya usafirishaji ili wafahamu umuhimu wa kuwasafirisha wanafunzi kwa wakati kutoka katika vituo wanavyopandia hadi kufika shuleni na kuwataarifu majina ya kila kituo ili wale wasiofahamu wajue ni kituo gani wanapaswa kushuka,” amesema Bw. Daudi.
Vilevile amesema, LATRA imeimarisha ukaguzi wa mara kwa mara katika vituo vya daladala jijini Dar es salaam na mikoa mingine Tanzania Bara na kwenye magari yanayotoa huduma ya kubeba wanafunzi, ili kuhakikisha yanazingatia Sheria, Kanuni na Taratibu za leseni za usafirishaji.
Amefafanua kuwa, nauli elekezi kwa mwanafunzi ni shilingi 200, kiwango ambacho kimewekwa na Mamlaka ili kumuwezesha kila mzazi kumudu gharama za usafiri huo na endapo atabainika mtoa huduma yeyote anatoza zaidi ya kiwango kilichoidhinishwa, Mamlaka haitosita kuchukua hatua dhidi yake kwa mujibu wa taratibu zilizopo.
Naye Bw. Joshua Changa, dereva wa daladala, amesema kuwa wanaendelea kuzingatia nauli elekezi ya shilingi 200 kama ilivyoelekezwa na LATRA, licha ya changamoto za uendeshaji wa huduma hiyo, na amewasihi makondakta wa daladala kutowakataa wanafunzi kwa kuwa ni sehemu ya abiria wanaopaswa kuhudumiwa kikamilifu na kuwapa kipaumbele wanapofika vituoni ili waweze kuwahi vipindi vyao shuleni.
Kwa upande wake Bw. Jackson Chavala kondakta wa daladala, amesema kuwa wanaendelea kujitahidi kutekeleza maelekezo na taratibu zilizowekwa na kutoa huduma bora kwa wanafunzi bila kikwazo na katika nyakati za asubuhi wanafunzi wasiopungua tano hadi kumi wamekuwa wakipakiwa katika kila daladala ili kuwawezesha kufika shuleni kwa wakati.
Bw. Joseph Kabogo ni mzazi wa mwanafunzi anayetumia huduma ya usafiri wa daladala amewashauri wazazi kuwapeleka watoto wao katika shule zilizo karibu na makazi yao ili kupunguza changamoto za kuchelewa kufika shuleni kutokana na changamoto za usafiri.
Juhudi za LATRA zinaendelea kulenga kuhakikisha huduma ya usafiri wa wanafunzi katika jiji la Dar es Salaam na mikoa mingine inaboreshwa na kuendana na viwango vinavyotakiwa, ili kuwezesha wanafunzi kufika shuleni kwa wakati na kwa usalama.

