Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

LATRA Logo

LATRA YAENDELEA KUSHUGHULIKIA CHANGAMOTO ZA TEKSI MTANDAO
Imewekwa: 12 Sep, 2022
LATRA YAENDELEA KUSHUGHULIKIA CHANGAMOTO ZA  TEKSI MTANDAO

Na. Mambwana Jumbe

Mkurugenzi Mkuu LATRA CPA Habibu Suluo amesema kuwa Mamlaka inaendelea kushughulikia changamoto za huduma za teksi mtandao, ikiwa ni pamoja na kufanya mazungumzo na madereva na kampuni za teksi mtandao nchini.

CPA Suluo amesema hayo  Septemba 12, 2022 jijini Arusha alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu Mkutano wa Wadau wa Reli, Tiketi Mtandao na Mazungumzo kuhusu Tiketi Mtandao.

Aidha ameeleza kuwa, kati ya tarehe 5 na 8 Septemba, 2022, Mamlaka ilifanya vikao na Chama cha Madereva wa Teksi Mtandao Tanzania (TODA), kampuni za Bolt na Uber ili kubadilishana taarifa na hoja za kibiashara na kiuchumi ili kusaidia kampuni za mifumo ya teksi mtandao, madereva na abiria kupata huduma bora, endelevu na kwa thamani halisi ya pesa.

CPA Suluo ameongeza kuwa, "kufuatia vikao hivyo, Mamlaka imeona itoe taarifa kwa umma kwamba vikao vyetu na mazungumzo yetu na TODA, Bolt na Uber yalikwenda vizuri. Kuna taarifa ya maandishi tunasubiri tupate leo na si zaidi ya kesho toka kwa Bolt na Uber ili na sisi tukamilishe taratibu zetu za ndani kabla hatujatangaza rasmi maamuzi ya Mamlaka."

"Niwashukuru kipekee Uongozi wa TODA na watoa huduma wa teksi mtandao walioendelea kutoa huduma ikiwa ni pamoja na Paisha, Ping, Indrive na Little Ride," amesema CPA Suluo.

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA), kwa mujibu wa Sheria Na. 3 ya mwaka 2019 ilitangaza viwango vya nauli za teksi mtandao kupitia Gazeti la Serikali Na. 1369 la tarehe 8 Aprili, 2022 na vyombo vingine vya habari. Kampuni za mifumo ya teksi mtandao za Bolt na Ubber zilisitisha baadhi ya huduma za usafiri wa teksi mtandao kufuatia kutoridhika na kiwango cha ukomo cha kamisheni cha asilimia 15 wanayopaswa kuwatoza madereva husika.

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo