Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) imetolea ufafanuzi tuhuma za rushwa zilizosambaa katika mitandao ya kijamii Julai 17, 2024 zikihusisha utoaji leseni za LATRA kwa pikipiki za magurudumu mawili na matatu (Bodaboda na Bajaji) mkoa wa Morogoro ambapo wamiliki wamelalamika kutishwa na kuombwa rushwa ili kupatiwa leseni za LATRA.
Bw. Salum Pazzy, Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano LATRA amefafanua tuhuma hizo kuwa, “LATRA imeona taarifa hiyo iliyosambaa kupitia mitandao ya kijamii ikimuainisha Afisa anayejulikana kwa jina la Fadhili anawalazimisha Madereva wampe fedha awalipie Faini na Stika za LATRA kwa madai mfumo unasumbua, Mamlaka imechukua hatua stahiki kwa haraka ili kupata ufumbuzi wa taarifa hiyo” amesema Bw. Pazzy
Aidha Bw. Pazzy ameeleza kuwa Mamlaka imewasiliana na Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro na kupata ufafanuzi zaidi juu ya tuhuma hizo ambapo Ofisi hiyo imeeleza kuwa imepokea tuhuma hizo na kuchukua hatua za uchunguzi juu mtuhumiwa.
“Afisa anayetuhumiwa ni Bw. Fadhili Elieza, Mwajiriwa wa muda mfupi (temporary staff) katika Halmashauri yetu idara ya ukusanyaji mapato na tumemsimamisha kazi mtuhumiwa huyo kupisha uchunguzi ufanyike hadi pale tutakapo jiridhisha ukweli juu ya tuhuma hizo na hatua stahiki zitachukuliwa endapo ukweli utabainika” imeeleza ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Morogoro.
Kwa upande wake Bw. Omary Mpulila, Katibu wa Umoja wa Wamiliki wa Bajaji Mkoa wa Morogoro ameieleza LATRA kuwa Umoja huo haujawahi kupokea malalamiko hayo kutoka kwa wanachama wake.
“Umoja wetu haujawahi kupokea malalamiko ya wanachama wake kutishwa au kuombwa rushwa wanapohitaji leseni za LATRA, nashauri taarifa hizo zinapaswa kuchunguzwa kwa umakini zisiichafue LATRA inavyoboresha huduma zake kwa wateja kwa uwazi na bila vishawishi vya rushwa” ameeleza Bw. Mpulila.
LATRA ina Hati ya Maelewano (MoU) inayoiwezesha Halmashauri Kutoa Leseni za LATRA kwa Pikipiki za Magurudumu Mawili na Matatu (Bodaboda na Bajaji), Mamlaka inakemea vikali vitendo vyote vya rushwa katika utoaji wa huduma zake, na inatoa wito kwa wadau wake na wananchi wote kutoa taarifa za vitendo vya rushwa kupitia namba 0800110019/20 bila malipo, zinazofanya kazi siku zote saa 24.