Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

MABASI SITA YA KATARAMA YAREJESHEWA HUDUMA
Imewekwa: 20 Sep, 2024
MABASI SITA YA KATARAMA YAREJESHEWA HUDUMA

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) imerejesha leseni ya utoaji huduma kwa mabasi sita ya Katarama Luxury kati ya mabasi 10 yaliyositishiwa leseni ya kutoa huduma ya usafirishaji abiria kwa kosa la kubadili sehemu ya Kifaa cha Kufuatilia Mwenendo wa Magari (VTD) na kuweka kifaa kingine kilichosababisha utumaji wa taarifa potofu kwenye Mfumo wa Kufuatilia Mwenendo wa Magari (VTS) mnamo Septemba 13, 2024.

Hayo yamebainishwa na Bw. Salum Pazzy, Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano LATRA kwenye mkutano na waandishi wa habari uliofanyika Septemba 20, 2024 ofisi za LATRA Mkoa wa Dar es Salaam.

Bw. Pazzy amesema kuwa Mamlaka imefikia uamuzi huo baada ya kufanya uchunguzi wa awali na kubaini kuwa kati ya mabasi 10 mabasi manne ndio yaliyoharibu mfumo huo.

“Katika uchunguzi wa awali kosa lilibainika kwenye mbasi mawili namba T420EDR na T836EDR mara baada ya kusitisha huduma Mamlaka ilifanya uchunguzi kwenye mabasi yote 10 na kubaini mabasi mengine mawili namba T835EDR na T435DXE kuwa yamefanya aina hiyohiyo ya kuingilia mfumo wa VTS, na mabasi hayo yanaendelea kufanyiwa uchunguzi na Jeshi la Polisi” amesema Bw. Pazzy.

Vilevile Bw. Pazzy amebainisha mabasi sita yaliyorejeshewa leseni ya utoaji huduma ambayo yanafanya safari kutoka Dar es Salaam kuelekea Mikoa ya Bukoba na Mwanza kuwa ni, T212ECR, T587EHC, T314 EHW, na T315EHW yanayofanya safari za Mwanza T446EH na T431EHW yanayofanya safari za Bukoba.

Aidha Mamlaka inawakumbusha wasafirishaji wote kuendelea kutii Sheria kanuni na Taratibu zilizopo na Mamlaka inaendelea kufuatilia kwa ukaribu magari yote yaliyopatiwa leseni ya utoaji huduma ya usafirishaji.

“Tunawakumbusha wasafirishaji wote kuwa Mamlaka inaendelea kufuatilia kwa ukaribu magari yote yaliyopewa leseni kwa mujibu wa Sheria na endapo tukabaini uvunjifu wowote wa Sheria, Taratibu na Kanuni au hila zozote ambazo zina haribu utaratibu wowote uliowekwa na kusababisha hasara ambazo hazikuhitajika, Mamlaka haitosita kuchukua hatua kwa msafirishaji yeyote anaevunja taratibu hizo” amesema Bw. Pazzy.

Kwa upande wake Bw. Laurian Katarama, Mmiliki wa Kampuni ya Katarama Luxury, amesema kuwa, watafuata Taratibu na Sheria za Barabarani na kuwaomba radhi abiria kwa usumbufu uliojitokeza baada ya kusitishiwa huduma.

Naye Bw. Elimboto Njoka, Meneja Oparesheni wa kampuni ya Katarama, amesema, Kampuni imepitia kipindi kigumu cha kusitishiwa huduma lakini wameishukuru LATRA kwa kuwapa nafasi nyingine ya kuzungumza na kuweza kupewa maelekezo.

“Tumepitia kipindi kigumu na tunaahidi kuzingatia yale ambayo ni mapungufu katika masharti ya leseni ya usafirishaji na tutaenda kuyafanyia kazi na tunaamni tutakuwa watu bora katika utoaji huduma ya usafirishaji” amesema Njoka.

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo