Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) imesitisha leseni ya usafirishaji kwa mabasi ya kampuni ya Katarama Luxury yanayotoa huduma ya usafiri kwa umma katika mikoa mbalimbali nchini kutokana na kukiuka Kanuni, Sheria na Taratibu za usafirishaji licha ya kuonywa mara nyingi.
Makosa ambayo yamebainika kufanywa ni pamoja na kuondoa kifaa kilichofungwa kwenye mabasi hayo na kufanya ujanja wa kufunga kifaa chao kingine cha kutuma taarifa zisizo sahihi kwenye mfumo wa Kufuatilia Mwenendo wa Magari (VTS).
Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mkuu LATRA CPA Habibu Suluo alipozungumza na waandishi wa habari Septemba 12, 2024 katika ofisi za LATRA Mkoa wa Dar es Salaam.
CPA Suluo amesema uamuzi wa kusitisha leseni ya usafirishaji kwa mabasi hayo, umefanyika kwa mujibu wa Kifungu cha 5(1)(b) ya Sheria ya Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini, Sura ya 413 na Kanuni ya 27(1)(c) na (d) ya Kanuni za Leseni za Usafirishaji (Magari ya Abiria) za Mwaka 2020.
“Mtakumbuka kwamba mwaka jana tulimsimamisha kwa kosa la kufanya ushindani usio na tija na kampuni ya Ally’s Star, na mwaka huu tulimsimamisha tena kwa kufanya vurugu barabarani na kwa sasa amepiga hatua zaidi kwa kung’oa sehemu ya kifaa kilichothibitishwa na Mamlaka ya Viwango Tanzania (TBS) na kubandika kifaa ambacho kinabadilisha taarifa ya mwenendo wa mabasi na amebadilisha kifaa cha antena, kwa hiyo inakuwa haitupi ile taarifa tunayoitegemea, huyu mtu hatuwezi kumvumilia, tumeamua kusitisha leseni ya usafirishaji kwenye mabasi yake yote kuanzia sasa mpaka tumfanyie uchunguzi, na kazi hii itafanywa kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi” amesema CPA Suluo.
Pia, CPA Suluo ameeleza kuwa, Mamlaka kwa kushirikiana na Jeshi la polisi Kikosi cha Usalama Barabarani wanaendelea kufanya uchunguzi na kuanzia Ijumaa 13 Septemba, 2024 mabasi ya kampuni hiyo hayatoruhusiwa kutoa huduma yoyote hadi pale uchunguzi utakapokamilika.
CPA Suluo amewasihi na kuwakumbusha watoa huduma za usafiri kuzingatia Sheria na Kanuni katika utoaji wa huduma kwa umma akiwataka kuajiri wahudumu wenye weledi na umahiri na wawapeleke katika mafunzo yanayoendelea kutolewa mikoa mbalimbali kupitia Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) na Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT).
Naye ACP Nassoro Sisiwayah, Mkuu wa Oparesheni wa Kikosi cha Usalama Barabarani Tanzania, amesema Jeshi la Polisi litahakikisha linafanya uchunguzi wa kina juu sababu za mabasi hayo ya Katarama kuendelea kufanya makosa licha ya kuonywa mara kwa mara na LATRA na kuahidi kuchukua hatua baada ya kukamilisha uchunguzi huo.
“Sisi Jeshi la Polisi tutafungua jalada la uchunguzi na uchunguzi utafanyika na kuhoji kupata majibu kamili na endapo tutabaini ni jinai basi tutafungua kesi na aliyefanya kosa hili na wahusika wote watafikishwa mahakamani” amesema ACP Sisiwayah.
Katika hatua nyingine CPA Suluo amesema kuwa, Mamlaka inaendelea kuwasihi wananchi kufuatilia mwenendo wa magari kupitia mfumo wa Taarifa kwa Abiria (PIS) unaopatikana kwa anwani ya https://pis.latra.go.tz kwa kutumia simu janja au kompyuta ili kujua mwendo kasi wa mabasi na kuisaidia Mamlaka kwa kutoa taarifa za mabasi ambayo yatakuwa yanaendesha mwendo hatarishi kupitia namba zinazopatika wakati wote saa 24 ambazo ni 0800110019 au 0800110020.