Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

LATRA YATOA ONYO YA TAHADHARI KWA ‘NEW FORCE ENTERPRISE’
Imewekwa: 11 Aug, 2023
LATRA YATOA ONYO YA TAHADHARI KWA ‘NEW FORCE ENTERPRISE’

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) imetoa onyo ya tahadhari kwa Kampuni ya New Force kutokana na kuwa na matukio mengi ya ajali ambapo tarehe 7 Agosti, 2023 basi Na. T618DMG lilipata ajali kati ya maeneo ya Ruahambuyuni na Mikumi na sababu ya ajali hiyo ilikuwa ni uzembe wa dereva kutaka kuyapita magari mengine bila kuchukua tahadhari.

Hayo yamesemwa na Bw. Salum Pazzy, Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano kutoka LATRA alipozungumza na waandishi wa habari Agosti 11, 2023 katika ofisi za LATRA Mkoa wa Dar es Salaam.

Ameongeaza kuwa, “hali ya kuendelea kuwepo na matukio ya ajali za barabarani kutokana na uzembe wa madereva katika kampuni ya New Force haikubaliki. Hivyo, Mamlaka inatoa nafasi kwa kampuni hiyo kutafuta suluhisho la sababu za ajali hizo haraka na Mamlaka itaendelea kuifuatilia kampuni hiyo kwa ukaribu. Vinginevyo, Mamlaka haitasita kuchukua hatua zingine za kisheria ikiwa ni pamoja na kufuta leseni za usafirishaji za kampuni hiyo.”

Ikumbukwe kuwa, mnamo tarehe 3 Julai, 2023 Mamlaka ilisitisha ratiba za mabasi 38 ya kampuni hiyo kuanza safari zake saa tisa (9:00) alfajiri na saa kumi na moja (11:00) alfajiri ikiwa ni sehemu ya hatua za kupunguza ajali za barabarani katika kampuni hiyo. Aidha, adhabu hiyo ilitokana na kuwepo kwa mfululizo wa ajali katika kipindi cha wiki nne mfululizo.

Katika hatua nyingine, LATRA imezionya kampuni za mabasi za Kilimanjaro Truck Company Limited, Abood Bus Service, Baraka Classic, Kapricon, Frester na Nyehunge Express kwa kuendelea kukiuka Sheria, Kanuni na Taratibu za usafirishaji.

 

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo