CPA Habibu Suluo, Mkurugenzi Mkuu Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) amesema Mamlaka imetoa nafasi 150 kwa mabasi yenye uwezo wa kubeba abiria 26 na kuendelea kutokana na changamoto za usafiri wa mabasi yaendayo haraka maarufu kama mwendokasi kwa njia ya BRT 1 yanayoenda Kimara ili kuongeza huduma za usafiri kwa wananchi kupitia njia hiyo.
CPA Habibu Suluo amebainisha hayo Novemba 5, 2025 Dar es Salaam alipozungumza na waandishi wa habari ambapo amesema wasafirishaji wanapaswa kutuma maombi ya kupata kibali kwenye Mfumo wa Usimamizi wa Taarifa za Barabara na Reli (RRIMS) kutoa huduma za usafirishaji kupitia njia ya Morogoro kuanzia Mbezi Luis kwenda Posta, Mnazi Mmoja, Muhimbili na Makumbusho.
Ameongeza kuwa, vibali vitakavyotolewa ni vya muda mfupi wakati marekebisho ya miundombinu yanasubiriwa kukamilika ili kurejesha huduma za usafiri kama ilivyokuwa mwazo.
“Mamlaka inatoa vibali kwa muda wa miezi mitatu kwa sababu tunatarajia kwa kipindi hiki Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART) watakuwa wamekamilisha marekebisho ya miundombinu iliyoharibika na kwa njia ya mbagala BRT 2 ambayo ilitolewa kwa muwekezaji MOFAT njia hii haina uharibifu mkubwa wa miundombinu katika mifumo ya ukataji tiketi, marekebisho haya yatakamilika ndani ya muda mfupi na wenzetu DART wakiwa tayari MOFAT atarejea kuendelea kutoa huduma,” ameeleza CPA Suluo.
Akizungumzia huduma za usafiri huo kwa njia ya Mbagala, CPA Suluo amesema kuwa, Mamlaka haitotoa tangazo la kuwakaribisha wasafirishaji wa mabasi ya mijini kutoa huduma njia ya Mbagala kwa kuwa tayari idadi ya magari yaliyopo yanajitosheleza na MOFAT akirejea huduma zitaendelea kwa kuwa hali tayari ilishakuwa nzuri.
Novemba 4, 2025 Mhe. Albert Chalamila, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam aliiagiza LATRA kutoa vibali vya muda mfupi kwa mabasi ya mijini ili ziweze kutoa huduma kwa njia ambazo zilikuwa zikitegemea usafiri wa mabasi yaendayo haraka kati ya Gerezani – Kimara na Gerezani – Mbagala.

