
Maafisa usafirishaji Wilayani Kasulu Mkoa wa Kigoma wamesema wapo tayari kujiunga na kuanzisha chama cha ushirika kitakachowawezesha kujiinua kiuchumi na kijamii kwa kuanzisha miradi mbalimbali ya maendeleo.
Maafisa wasafirishaji wamebainisha hayo kwa nyakati tofauti baada ya kupatiwa semina ya umuhimu wa vyama vya ushirika na faida zake iliyoratibiwa na Mhe. Prof. Joyce Ndalichako, Mbunge wa Jimbo la Kasulu Mjini na kutolewa na Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA), Juni 21, 2025 ukumbi wa Shule ya Sekondari Bogwe, Kasulu Mkoani Kigoma.
“Elimu hii imetufumbua fikra kwamba kumbe tunaweza kujiunga, kuchagua viongozi na kuanzisha umoja wetu kupitia chama cha ushirika ambacho tunaweza kufika mbali kimaendeleo na kuepukana na hali ya umasikini,” amesema Bw. Ally Shabari.
“Tunawashukuru LATRA kwa kutupatia elimu hii na tunaahidi kuendelea kupeana elimu kwa wenzetu ambao hawakufanikiwa kufika ili kwa pamoja tuunde ushirika wetu ambao kwa mujibu wa haya tuliyoelezwa na kuyaona kwa wenzetu wa KIBABOT kule Kilimanjaro na UMWAMWA Mwanza, nasi imeyupa mori na morali ya kuanzisha ushirika wetu ili nasi tuweze unufaika na faida mbalimbali zitakazotuwezesha kufika mbali kimaendeleo,” amesema John Mselem.
Akizungumza katika semina hiyo, Mhe. Joyce Ndalichako Mbunge wa Jimbo la Kasulu Mjini amesema kuwa, ameona ni wakati sahihi wa kutumia fursa hiyo inatolewa na Serikali kupitia LATRA na lengo lake ni kuhakikisha maafisa wasafirishaji hao wananufaika na fursa hiyo ya uchumi itakayowawezesha kubadili mustakabali wa maisha yao na familia zao.
“Wataalam wa LATRA wamewapatia elimu hii ya ushirika, Afisa Ushirika nae amewapa taratibu za kuanzisha ushirika, mimi nipo pamoja na nyie kuhakikisha jambo hili linafanikiwa. Lakini pia Jeshi la Polisi limetukumbusha kuhusu kutekeleza majukumu yenu kwa kufuata taratibu za usalama barabarani, wakati tunaendelea na mchakato wa kuanzisha ushirika basi mfuate Sheria zilizopo,” ameeleza Mhe. Ndalichako.
Naye Bw. Salum Pazzy, Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano LATRA, aliyemuwakilisha CPA Habibu Suluo, Mkurugenzi Mkuu LATRA kwenye Semina hiyo amesema kuwa, kazi ya kuendesha bodaboda ni kama kazi nyingine, hivyo amewakumbusha maafisa wasafirishaji hao kuheshimu, kuonesha weledi wanapokuwa wanatekeleza majukumu yao na kutoa huduma bora huku wakizingatia usalama wao na abiria wanaowasafirisha.
Akizungumzia faida za vyama va ushirika kwa maafisa usafirishaji hao, Bw. Pazzy amesema kuwa Mamlaka itawarejeshea kamisheni ya asilimia 20 ya pesa zitakazopatikana baada ya kukata leseni za LATRA kwa kuwa watakuwa ni mawakala wa Mamlaka na watakuwa na nguvu ya kusimamiana wenyewe katika majukumu yao.
Naye SP Patrick Damas amewakumbusha maafisa wasafirishaji hao kuzingatia mwendokasi uliowekwa wa kuendesha pikipiki kwa mwendo usiozidi kilometa 50 kwa saa, kuzingatia alama na ishara za barabarani, chombo kuwa na matairi bora, pikipiki kuwa na vioo vya kutazama nyuma (side mirrors) pamoja na kuacha kutumia simu wakiwa kwenye shughuli zao za usafirishaji.
Kanuni za LATRA za Usafiri wa Magari ya Kukodi, 2020 ilifanyiwa marekebisho Machi, 2023 na kuruhusu LATRA kukasimu madaraka ya kutoa leseni kwa Wakala aliyethibitishwa ambao ni Vyama Ushirika, Taasisi za Umma (LGA), Kampuni na Watu Binafsi.