Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

MAAFISA USAFIRISHAJI WILAYANI KASULU WAASWA KUZINGATIA SHERIA
Imewekwa: 21 Jun, 2025
MAAFISA USAFIRISHAJI WILAYANI KASULU WAASWA KUZINGATIA SHERIA

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) imewasihi maafisa wasafirishaji Wilayani Kasulu, Mkoa wa Kigoma kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu za usalama barabarani pamoja na Miongozo ya usafirishaji nchini.

Hayo yameelezwa na Bw. Salum Pazzy, Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano LATRA, aliyemuwakilisha CPA Habibu Suluo, Mkurugenzi Mkuu LATRA kwenye Semina kwa Maafisa Wasafirishaji iliyolenga kuwapatia elimu ya vyama vya ushirika iliyofanyika Juni 21, 2025, ukumbi wa Shule ya Sekondari Bogwe, Wilayani Kasulu, Kigoma.

“Kazi yenu ya usafirishaji ni kama kazi nyingine, mnapaswa kujali uhai wenu na wa watu wengine kwa kufuata Sheria zilizopo. Pia, mnapaswa kuwa na leseni za usafirishaji ili mtekeleze kazi zenu kwa uhuru, kujiamini na hatimaye kujipatia kipato kitakachoendesha maisha yenu,” amesema Bw. Pazzy.

Ameongeza kuwa, suala la usalama wao kama wasafirishaji pamoja na abiria wanaowasafirisha ni muhimu, hivyo wanapaswa kuhakikisha wanakuwa na kofia ngumu wanapakia abiria mmoja kwenye pikipiki, kuvaa mavazi na viatu vinanayokidhi usalama wao wakiwa kwenye kazi zao za usafirishaji.

Naye Bw. Addo Msigala, Afisa Mfawidhi LATRA Mkoa wa Kigoma amewaeleza maafisa wasafirishaji hao kuwa, Wilaya ya Kasulu ina pikipiki zaidi ya 3,000 lakini waliokata leseni LATRA ni 302 jambo ambalo linaonesha hali ya ukataji wa leseni Wilayani hapo kuwa mdogo na hivyo amewaasa kubadilika na kukata leseni hizo kupitia ofisi ya Posta ambao ni Mawakala wa ukataji leseni za LATRA Wilayani hapo.

Akitoa elimu ya usalama barabarani SP Damas Patrick, Mkuu wa Usalama Barabarani Wilayani Kasulu amewasihi maafisa wasafirishaji hao kutopandisha mtoto chini ya miaka 9 kwenye pikipiki bila kuwa na mtu mzima kwa kuwa ni kosa kisheria na inahatarisha usalama wa mtoto.

Vilevile SP Patrick amewakumbusha maafisa wasafirishaji hao kuzingatia mwendokasi uliowekwa wa kuendesha pikipiki kwa mwendo usiozidi kilometa 50 kwa saa, kuzingatia alama na ishara za barabarani, chombo kuwa na matairi bora, pikipiki kuwa na vioo vya kutazama nyuma (side mirrors) pamoja na kuacha kutumia simu wakiwa kwenye shughuli zao za usafirishaji.

Semina hiyo imeratibiwa na Mhe. Joyce Ndalichako, Mbunge wa Jimbo la Kasulu Mjini na kuhudhuriwa na maafisa wasafirishaji waliopatiwa elimu ya usalama barabarani, ukataji wa leseni za LATRA, Hali ya huduma za usafirishaji Wilayani Kasulu, Elimu ya vyama vya ushirika, faida zake, taratibu za kujiunga na vyama vya ushirika. 

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo