Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

MABASI 2,033 YAMEUNGANISHWA KWENYE MFUMO WA TIKETI MTANDAO
Imewekwa: 18 Aug, 2022
MABASI 2,033 YAMEUNGANISHWA KWENYE MFUMO WA TIKETI MTANDAO

Na. Mambwana Jumbe

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) CPA Habibu Suluo amesema jumla ya mabasi 2,033 yanayomilikiwa na kampuni 308 za usafirishaji abiria yameshaunganishwa kwenye mfumo wa Tiketi Mtandao kupitia watoa huduma (vendors).

CPA Suluo amesema hayo leo Agosti 18, 2022 kwenye mkutano na waandishi wa habari uliofanyika ofisi za Makao makuu ya Mamlaka zilizopo Dar es Salaam.

“Hadi kufikia jana tarehe 17, Agosti, 2022, Jumla ya mabasi 7,649 yamesajiliwa kwenye Mfumo wa Ufuatiliaji Mwenendo wa Magari- VTS ambapo mabasi 3,916 yameonekana yapo barabarani (active). Mafanikio haya ni sawa na asilimia 52 ukilinganisha na asilimia 37 ilivyokuwa Julai 31, 2022”, ameeleza CPA Suluo.

Amesema kuwa Mfumo wa tiketi mtandao ulikuwa katika kipindi cha majaribio kuanzia Aprili mosi 2022 hadi Juni 30, 2022. Tarehe mosi Julai, Mamlaka ilitoa muda wa nyongeza wa miezi miwili hadi tarehe 31 Agosti, 2022, ulioambatana na kufanya ukaguzi na kutoa elimu kwa wasafirishaji waliokuwa na changamoto tofauti tofauti ili kuhakikisha mabasi yote yaunganishwe kwenye mfumo huo.

Tunawapongeza wasafirishaji na wadau wote walioshiriki kutimiza takwa la kisheria la mabasi husika kutumia mfumo wa Tiketi Mtandao. Nitumie nafasi hii pia kuwakumbusha wadau kuwa tunaenda kuuchukua hatua stahiki, ikiwa ni pamoja na kutoa adhabu ya faini na/au kusitisha huduma ya mabasi yote ambayo yatashindwa kutimiza takwa hili la kisheria ifikapo tarehe 1 Septemba, 2022,” amesema.

Aidha, CPA Suluo amesema kuanzia wiki ijayo, yeye pamoja na watumishi wa Mamlaka watakuwa barabarani kutoa elimu kwa wadau wa usafirishaji ili ikifika Septemba 01, kusiwe na mdau ambaye atakuwa na sababu ya kuwa hana taarifa kuhusu utekelezaji wa tiketi mtandao nchini.

Aliongeza kuwa, Mamlaka imetekeleza maboresho ya mfumo wa Tiketi Mtandao kwa kushirikiana na wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Uchukuzi), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Chama cha Wamiliki wa Mabasi (TABOA), Kituo cha Taifa cha Kuhifadhi Kumbukumbu Kimtandao (NIDC), Watoa Huduma za Tiketi za Kielektroniki na wadau wengine wa Serikalini na sekta binafsi.

Vilevile, CPA Suluo amesema kuwa Mamlaka inawakumbusha wamiliki wa mabasi kuhakikisha kuwa tiketi inataarifa zote muhimu, ikiwemo: Jina la abiria, namba ya basi, tarehe na muda wa safari, kituo cha kuanzia na kumalizia safari, nauli iliyolipwa, anwani na namba za simu za msafirishaji na namba ya tiketi husika”, amefafanua.

Alifafanua kuwa taarifa sahihi za abiria katika mfumo wa Tiketi Mtandao ni muhimu kwa kuwa zinaweta kumbukumbu sahihi za safari husika na iwapo kukitokea tatizo itakuwa rahisi kuthibitisha taarifa za safari hiyo.

Taarifa za Tiketi Mtandao zinaweza kumsaidia abiria kwa namna tofauti, kwa mfano ikitokea ajali na abiria kupata madhara, itakuwa rahisi abira huyu kupata stahiki zake ikiwa ni pamoja na malipo ya bima”

Naye Mkurugenzi wa Udhibiti Usafiri wa Barabara Bw. Johansen Kahatano amesema kuwa LATRA inawashauri abiria kutumia huduma za mabasi yanayotumia mfumo wa Tiketi Mtandao kwani mfumo huo una faida nyingi kwa abiria, wasafirishaji na Serikali.  Pia abiria atumiapo mabasi yanayotumia mfumo wa Tiketi Mtandao ataepuka usumbufu pale ambapo mabasi yasiyotoa tiketi hizo zitakapozuiliwa kutoa huduma.

“Jambo hili ni la kwetu sote na tunawasihi abiria kuwa mstari wa mbele kwenye kudai tiketi za kielektroni kwenye mabasi. Abiria ukipewa tiketi ya makaratasi kataa na dai ile ya kielekroni, kumbuka tiketi yako ndio mkataba wako na gari ulilopanda’” amesisitiza Bw. Kahatano.

Naye Meneja Mradi wa Tiketi Mtandao CPA Tadei Mwita amesisitiza kuwa mara baada ya kukata tiketi mtandao, abiria ataipata tiketi hiyo kwa njia ya ujumbe mfupi wa maandishi unaotumwa kwenye simu yake au atapatiwa karatasi maalumu  iliyochapishwa kwenye mashine ya kutolea tiketi.

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo