Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

MAGOMBANA: HUDUMA ZA USAFIRI ARDHINI ZINAONGOZWA NA SHERIA
Imewekwa: 08 Apr, 2026
MAGOMBANA: HUDUMA ZA USAFIRI ARDHINI ZINAONGOZWA NA SHERIA

Bw. Andrew Magombana, Mkurugenzi Msaidizi Usafiri kwa njia ya Barabara kutoka Wizara ya Uchukuzi amesema huduma za usafiri ardhini nchini zinaongozwa na Sheria, Kanuni na Taratibu ambapo katika masuala ya kupanga na kufanya mapitio ya nauli za usafiri wa umma kwa njia ya barabara, utaratibu unataka kwanza kupata maoni ya wadau.

Bw. Magombana aliyemuawakilisha Prof. Godius Kahyarara, Katibu Mkuu Wizara ya Uchukuzi  amesema hayo alipofungua rasmi mkutano wa wadau kuhusu mchakato wa mapitio ya nauli za usafiri wa umma kwa njia ya barabara uliofanyika Aprili 8, 2026 ukumbi wa Karimjee, Dar es Salaam.

Mkutano wa leo ni jukwaa la kusikilizana. Serikali ipo hapa kusikia, kuchambua, na kupata uelewa wa pamoja juu ya nini kifanyike hasa endapo bei za mafuta zitaendelea kupanda au kutengamaa. Niwahimize mtoe maoni yenye ushahidi, hoja zenye kujenga, na mapendekezo yanayoangalia mustakabali wa sekta nzima, si maslahi binafsi”, amesema Bw. Magombana.

Vilevile amesema Serikali itaendelea kuhakikisha utulivu wa kiuchumi katika sekta ya uchukuzi kupitia sera makini, uratibu na usimamizi madhubuti, na kwa kushirikiana kwa karibu na wadau wote.

“Serikali itaendelea kuhakikisha huduma za uchukuzi zinafanyika vizuri kwa kuzingatia Sheria zilizopo. Leo tunachukua maoni ya wadau na Mhe. Waziri wa Uchukuzi kama Sheria inavyomruhusu ataangalia hatua za kuchukua baada ya LATRA kuwasilisha maoni kwake,” ameeleza Bw. Magombana.

Mkutano huo umehudhuriwa na wadau wa usafiri ardhini kutoka vyama vya wasafirishaji, watumiaji wa huduma za usafiri, Baraza la Watumiaji wa Huduma za Usafiri Ardhini (LATRA CCC) pamoja na viongozi wa LATRA. Wadau hao walifanya mawasilisho yao kuhusu marejeo ya nauli na kwa wale walioshindwa kushiriki wanaweza kuwasilisha maoni yao ndani ya siku 14 hadi tarehe 22 Aprili, 2026 kwa baruapepe info@latra.go.tz

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo