Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

MAGOMBANA: MAONI YA WADAU NI MUHIMU KUBORESHA KANUNI ZA UCHOVU WA MADEREVA
Imewekwa: 20 Mar, 2026
MAGOMBANA: MAONI YA WADAU NI MUHIMU KUBORESHA KANUNI ZA UCHOVU WA MADEREVA

Bw. Andrew Magombana, Mkurugenzi Msaidizi Usafiri kwa Njia ya Barabara, Wizara ya Uchukuzi, amesema kuwa maoni ya wadau ni nyenzo muhimu katika kuboresha Kanuni za Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) za Usimamizi wa Madhara ya Uchovu wa Madereva za Mwaka 2026.

Amesema hayo alipomuwakilisha Prof. Godius Kahyarara, Katibu Mkuu Wizara ya Uchukuzi, katika mkutano wa kutoa elimu na kupokea maoni ya viongozi wa vyama vya madereva na viongozi wa vyama vya malori Tanzania na wamiliki wa kampuni za usafiri wa malori nchini kuhusu rasimu ya kanuni hizo Machi 17, 2026 ofisi za LATRA, Dar es Salaam,

Bw. Magombana amesema kanuni hizo zinalenga kuhakikisha madereva wa vyombo vya moto kibiashara wanaendesha wakiwa na utimamu wa mwili na akili, hatua itakayochangia kupunguza ajali za barabarani na kulinda maisha ya abiria.

“Kanuni hizi zinalenga kuhakikisha madereva wanafanya kazi wakiwa na afya bora ya mwili na akili. Tukifanikiwa kudhibiti uendeshaji katika hali ya uchovu, tutakuwa tumepunguza kwa kiasi kikubwa ajali za barabarani pamoja na usumbufu kwa abiria,” amesema Bw. Magombana.

Aidha, amesisitiza kuwa ushirikishwaji wa wadau unaiwezesha Serikali kupata maoni yenye tija kutoka kwa wadau wanaofahamu hali halisi ya sekta ya usafiri, jambo linalochangia kuboresha sera na kanuni mbalimbali.

Kwa upande wake, Bi. Esnath Mwakyembe, Kaimu Meneja wa Uthibitishaji Madereva na Usajili wa Wahudumu, akimuwakilisha CPA Dkt. Habibu Suluo, Mkurugenzi Mkuu  LATRA, amesema Mamlaka imewahimiza viongozi wa vyama vya madereva kuwashirikisha wanachama wao kikamilifu ili kutoa maoni kuhusu rasimu hiyo.

“Tumetoa elimu na kufungua fursa ya wadau kutoa maoni yao. Tunawasihi viongozi kuhakikisha wanawafikia madereva wote ili kushiriki kikamilifu katika uboreshaji wa kanuni hizi. Mamlaka itaendelea kupokea maoni kwa kipindi cha siku 14 kuanzia Machi 17, 2026,” amesema Bi. Mwakyembe.

Naye Bw. Greyson Wimile, Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Malori Tanzania (CHAWAMATA), amesema chama hicho kimepokea rasimu za Kanuni hizo na kiko tayari kushirikisha wanachama wake pamoja na wataalamu wa Sheria ili kuwasilisha mapendekezo yatakayosaidia kuboresha Kanuni hizo ndani ya muda uliotolewa.

Kwa upande wake Bw. Michael Likingo, Meneja wa Mafunzo kwa Madereva kutoka kampuni ya Superstar, amesema ni muhimu kwa wamiliki wa malori kuweka mifumo madhubuti ya usalama, ikiwemo utoaji wa mafunzo endelevu kwa madereva pamoja na matumizi ya teknolojia za kufuatilia mienendo ya madereva wanapokuwa safarini kwani ni muhimu katika kutatua madhara yanayosababishwa na uchovu wa dereva.

Rasimu ya Kanuni za Usimamizi wa Madhara ya Uchovu wa Madereva inaweka msisitizo katika kuimarisha usalama barabarani kupitia udhibiti wa uchovu kwa madereva, hatua inayotarajiwa kupunguza ajali, kulinda maisha ya abiria na kuongeza ufanisi katika sekta ya usafiri ardhini.

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo