Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

MAKONGORO NYERERE AHIMIZA ELIMU, TIKETI MTANDAO
Imewekwa: 15 Sep, 2022
MAKONGORO NYERERE AHIMIZA ELIMU, TIKETI MTANDAO

Na. Salum Pazzy

 

Mkuu wa Mkoa wa Manyara Mhe. Makongoro Nyerere ameiagiza Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) kuendeleza matumizi ya Teknolojia katika udhibiti wa huduma za usafiri ardhini ikiwa ni pamoja na matumizi ya mfumo wa Tiketi Mtandao ili kuongeza tija kwa wasafirishaji, abiria na Serikali kwa ujumla.

 
Ameyasema hayo jana tarehe 14 Septemba, 2022 katika kikao chake na Mkurugenzi Mkuu wa LATRA CPA Habibu J. Suluo kilichofanyika ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Manyara mjini Babati, kilichohudhuriwa na Katibu Tawala Mkoa wa Manyara Bi. Caroline Mthapula na baadhi ya maafisa wa LATRA ikiwa ni sehemu ya ziara ya Mkurugenzi Mkuu wa LATRA mkoani humo.
 

‘Nilipata bahati ya kujifunza zaidi kuhusu mfumo huu ambao nilikuwa nikiusikia, baada ya kukaa na wataalamu nimegundua kuwa mfumo wa Tiketi Mtandao unamsaidia mmiliki wa basi kukusanya mapato yake kwa ufanisi zaidi, unamrahisishia abiria kununua tiketi kwa urahisi na unaisaidia Serikali kukusanya mapato kwa ufanisi’ alisema.

 
Aliongeza kuwa, mfumo huo unasaidia kudhibiti upandishaji holela wa nauli kipindi cha mahitaji makubwa ya huduma ikiwemo kipindi cha sikukuu za mwisho wa mwaka.
 

Aidha, mheshimiwa Nyerere emeiagiza LATRA kuongeza utoaji wa elimu na kuwafikia wadau wengi zaidi kwa kuwa matumizi ya teknolojia ndiyo muafaka wa kuleta mapinduzi katika sekta ya usafiri nchini.

 
‘Tunakoelekea ni abiria kuweza kujihudumia mwenyewe bila kutegemea kuhudumiwa na mtu, labda mizigo ndiyo itahitaji kuhudumiwa, kwa kuwa Tanzania ni sehemu ya dunia, maendeleo hayo hatuwezi kuyaepuka’
 

Amesema kuwa ofisi yake itaendelea kushirikiana na LATRA ambapo ameiagiza LATRA kuendeleza ushirikiano na wadau wote wakiwemo Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani na wasafirishaji ili kuongeza tija katika sekta ya usafirishaji ambayo inatoa ajira nyingi kwa wananchi na kusaidia kufikia malengo ya Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
 
 
Kwa upande wake, CPA Suluo ameahidi kufanyia kazi maelekezo ya Mkuu huyo wa Mkoa na kuendeleza ushirikiano na elimu kwa wadau wote ili kuwezesha Serikali kufikia malengo yake kwa wakati.

 
Katika ziara yake Mkoani Manyara, CPA Suluo alipata fursa ya kutembelea wadau mbalimbali wakiwemo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Manyara ACP George Katabazi na Kaimu Mkuu wa Usalama Barabarani Mkoa wa Manyara ASP Mahenda Kera ambapo walipata fursa ya kujadili masuala mbalimbali ya ushirikiano ikiwemo utekelezaji wa matumizi ya mfumo wa Tiketi Mtandao.

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo