Wasafirishaji wa mabasi ya mijini (Daladala) yanayotumia barabara ya Kilwa jijini Dar es Salaam, wameanza utekelezaji wa utaratibu wa daladala kupita katika Kituo kikuu cha Mabasi Yaendayo Haraka (BRT) njia ya Mbagala, Dar es Salaam.
Hatua hiyo ni utekelezaji wa agizo lililotolewa na CPA, Dkt. Habibu Juma Suluo, Mkurugenzi Mkuu Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA), Juni 15, 2026 alipotembela Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka Awamu ya I na II ambapo alisema kuanzia Julai Mosi, 2026 daladala zote zinazotumia barabara ya Kilwa zitatakiwa kutumia kituo cha Mabasi Yaendayo Haraka, maarufu kama Mwendokasi kushusha na kupakilia abiria. Aidha, hazitaruhusiwa kushusha au kupakia abiria katika barabara zilizo sambamba na barabara za Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (BRT).
Nia njema ya maboresho haya imepokelewa kwa mikono miwili na madereva pamoja na makondakta wa daladala katika eneo la Mbagala. Bw. Norbert Mdegela, mmoja wa madereva wa daladala, ameishukuru Serikali kwa kuwezesha upatikanaji wa huduma ya mwendokasi na kuongeza kuwa utaratibu huo unalinda ajira zao kwani haukuwaondoa barabarani bali umewajengea mazingira bora ya kubadilishana abiria na mabasi ya BRT
“Jambo lolote linapoanza huwa linaonekana gumu hasa ukizingatia sisi tulishazoea kushusha abiria nje lakini muda unavyokwenda tutazoea na kuona ni jambo la kawaida kwa kuwa lina manufaa kwetu sisi sote. Jambo hili ni zuri kwa kuwa sisi daladala tunashusha abiria wanaoenda katikati ya jiji na tunapakia wanaoshuka kwenye mwendokasi,” amesema Bw. Mdegela.
Naye Bw. Samson Juma, Kondakta wa daladala Mbagala amesema kuwa, jambo la kuingia ndani ya Kituo cha Mwendokasi ni zuri kwa kuwa linaongeza usalama wa abiria na amewasihi makondakta na madereva kuingiza daladala kituoni na kuendelea na shughuli za usafirishaji bila bughudha.
Kwa upande wao, watumiaji wa usafiri huo wameonesha kufurahishwa na utaratibu huo unaounganisha huduma zote za usafiri katika eneo moja salama. Bi. Marietha Joseph, mmoja wa abiria, ameeleza kuwa, hatua hiyo imerahisisha upatikanaji wa usafiri wa daladala na mwendokasi kwa wakati mmoja bila kulazimika kutoka nje ya kituo.
“Nimeshukuru sana huduma iliyoletwa ya kushuka kwenye mwendokasi na kupanda kwenye daladala, kwa kweli hii imekuwa rahisi sana kwetu kupata huduma hizi eneo moja na litaongeza usalama kwetu sisi abiria kwa kuwa tunashuka na kupanda eneo lililo salama,” ameeleza Bi. Marietha.
Bw. Khalfani Saidi ni abiria na ameeleza kuwa, huduma ya daladala kuingia ndani ya kituo cha mwendokasi imeleta unafuu na kuondoa usumbufu waliokuwa wakiupata awali, ikiwemo daladala kuwashusha mbali na kituo hicho jambo lililowalazimu kutembea umbali mrefu kufika kituo cha mwendokasi
Sambamba na kuanza kwa utaratibu huo tarehe 1 Julai, 2026, maafisa wa LATRA wamekuwepo eneo la tukio kutoa elimu kwa vitendo kwa madereva, makondakta, na abiria ili kujenga uelewa wa pamoja wa jinsi ya kutumia miundombinu hiyo ya kisasa kwa ufanisi na usalama mkubwa.
Bw. Pateli Ngereza, Kaimu Meneja Leseni Usafiri wa Barabara LATRA amebainisha kuwa, uwepo wa maafisa hao unalenga kuhakikisha kuwa hakuna daladala inayoshusha nje ya maeneo yaliyoidhinishwa.
“Tupo hapa kusimamia utekelezaji na kuhakikisha daladala zote zinashusha ndani ya kituo. Tunaamini utaratibu huu utaleta tija, utaimarisha usalama wa abiria, na utarahisisha mzunguko wa kibiashara kwa wamiliki wa daladala.”
Naye Bw. Ashelly Mwihambi, Afisa Mfawidhi Ofisi ya LATRA Mbagala amesema kuwa, daladala kuingia ndani ya Kituo cha Mwendokasi kunaunganisha huduma kati ya wanaotoa huduma ya mwendokasi na usafiri wa daladala huku abiria akipata huduma kwa urahisi.
“Hii inamrahisishia abiria kupata huduma ya usafiri kwa haraka pindi anaposhuka kwenye basi la mwendokasi kwakuwa hatolazimika kwenda nje ya kituo bali atapata daladala lililopo ndani ya kituo cha mwendokasi, Pia, ndani ya kituo kuna usafiri wa pikipiki za magurudumu mawili (bodaboda) na pikipiki za magurudumu matatu (bajaji) ambavyo navyo vitakuwa vinashusha abiria na kupakia abiria kituoni hapo,” amesema Bw. Mwihambi

