
Mhe. Khamis Hamza Khamis (Mb), Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) amekoshwa na pikipiki za magurudumu matatu (bajaji) kwa kuwa zinatumia nishati safi ya umeme na zinasaidia utunzaji wa mazingira.
Mhe. Khamis amesema hayo Juni 04, 2025 alipotembelea banda la LATRA na kupatiwa elimu ya jinsi pikipiki za magurudumu matatu (bajaji) zinazotumia umeme zinavyotunza mazingira kwenye maonesho ya Wiki ya Mazingira iliyofanyika jijini Dodoma, viwanja vya Kituo cha Mikutano cha Jakaya Kikwete.
Vilevile Mhe. Khamis ametoa rai kwa wadau kununua pikipipiki hizo kwa kuwa ni rahisi kutumia, ni rafiki kwa mazingira na zitasaidia kuinua vipato vyao kwa kuwa gharama za uendeshaji wake ni mdogo ukilinganisha na zile zilizozoeleka
Akitoa elimu ya pikipiki hizo, Bw. Geoffrey Silanda, Meneja Uratibu Usalama na Mazingira LATRA amesema kuwa, pikipiki hizo zinawekwa chaji kwa saa tatu na kwenda umbali wa kilomita 100 huku zikitumia umeme wa TZS. 3,000 tu.
“Uwepo wa pikipiki za magurudumu mawili na matatu zinazotumia umeme zinachagizwa na mapinduzi makubwa ya Teknolojia katika sekta ya usafiri nchini yanayoleta tija na kuongeza ufanisi wa utoaji wa huduma kwa wananchi na kuleta unafuu wa uendeshaji kwa wasafirishaji”, amesema Bw. Silanda.
Naye Bi. Mercy Kitomari kutoka Kampuni ya TRI amesema kuwa, kampuni hiyo inazo pikipiki za magurumu mawili (bodaboda), magurudumu matatu (bajaji) na maguta yanayotumia umeme yataanza kupatikana nchini hivi karibuni.
LATRA inatekeleza kwa vitendo maono na maelekezo ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye anasisitiza ushirikiano wa Taasisi za Serikali na zisizo za Kiserikali ambapo katika maonesho ya Wiki ya Mazingira yaliyofanyika jijini Dodoma, Mamlaka kwa kushirikiana na Kampuni ya TRI inayomilikiwa na wazawa, wameonesha pikipiki za magurumu matatu zinazotumia umeme ambazo zinaongeza fursa kwa watoa huduma wa usafiri ardhini nchini.