Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

MHE. KIHENZILE AIPA TANO LATRA, MFUMO WA PIS
Imewekwa: 08 Aug, 2024
MHE. KIHENZILE AIPA TANO LATRA, MFUMO WA PIS

Mhe. David Kihenzile (Mb), Naibu Waziri wa Uchukuzi ameipongeza Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) kwa kubuni Mfumo wa Taarifa kwa Abiria - PIS unaopatokana kwa anwani ya  pis.latra.go.tz/ unaowasaidia abiria na wadau wa usafiri nchini kufahamu taarifa za mabasi yanayoelekea vituo vya mabasi vilivyo karibu yao na kuwawezesha wadau hao kufahamu mwendokasi na mahala lilipo basi husika.

Mhe. Kihenzile ametoa pongezi hizo Agosti 08, 2024, viwanja vya Nzuguni Dodoma alipotembelea banda la LATRA kwenye Maonesho ya Kilimo ya Kimataifa ya Nane Nane na kujionea jinsi Mamlaka hiyo inavyotekeleza majukumu yake ya kiudhibiti kwa mujibu wa Sheria, Taratibu na Kanuni zilizopo.

“Mnastahili pongezi kwa kubuni Mfumo huu ambao unatoa taarifa muhimu kwa abiria ikiwemo kufahamu mwendokasi wa basi husika pamoja na vituo mbalimbali vya mabasi vilivyopo nchini,” amesema Mhe. Kihenzile.

Naye Bw. Gerson Msigwa, Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, alipozulu katika banda la LATRA alifurahishwa na jinsi Mamlaka hiyo inavyotumia fursa za Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kwa kubuni mifumo madhubuti inayosaidia katika udhibiti wa sekta ya usafiri ardhini pamoja na kurahisisha utoaji wa huduma na taarifa muhimu kwa abiria na wasafirishaji kwa jumla.

Miongoni mwa mifumo aliyoizungumzia ni Mfumo wa PIS ambapo baada ya kupatiwa maelezo ya jinsi mfumo huo unavyofanya kazi, Bw Msigwa alisema kuwa, kutokana na umuhimu wa mfumo huo kwa wananchi, ni vema Mamlaka ikaongeza juhudi za kuutangaza zaidi ili uweze kufahamika kwa wananchi ambao ndio walengwa wakuu wa mfumo ukizingatia kuwa ni mfumo rahisi kuutumia.

Kwa upande wake, Mha. Eliud Kataraihya, Mkuu wa Kitengo cha TEHAMA - LATRA amesema Mamlaka itaendelea kubuni na kutumia mifumo ya TEHAMA na kuhakikisha inasomana kama ilivyoelekezwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania.

Mamlaka imeshiriki katika Maonesho ya Nane Nane jijini Dodoma kwa kutoa elimu ya kazi na majukumu ya Mamlaka pamoja na kuonesha Mifumo mbalimbali ya TEHAMA inayotumika na Mamlaka hiyo ikiwemo Mfumo wa PIS, Mfumo wa Kufuatilia Mwenendo wa Magari (VTS), Mfumo Tumizi wa LATRA App, Mfumo wa Tiketi Mtandao pamoja na Mfumo wa Utoaji wa Leseni (RRIMS).

 

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo