Mhe. David Mwakiposa Kihenzile (Mb) Naibu Waziri Uchukuzi amewakaribisha wadau wa sekta ya usafiri ardhini kuwekeza kwenye sekta ya usafirishaji kwa kuwa nchi ni salama na mazingira ya uwekezaji yameboreshwa.
Mhe. Kihenzile amesema hayo Novemba 24, 2025 alipofungua maonesho ya Maadhimisho ya kwanza ya Wiki ya Usafiri Endelevu Ardhini yanayofanyika viwanja vya Mnazi Mmoja Dar es Salaam.
“Nchi yetu ni salama na tunahitaji wawekezaji wa ndani na nje ya nchi ili wawe sehemu ya ustawishaji wa sekta ya usafiri ardhini nchini na kwa kufanya hivyo watakuwa wameunga mkono jitihada za Serikali za kuboresha na kurahisisha huduma za usafiri na usafirishaji nchini,” amesema Mhe. Kihenzile.
Vilevile amewasihi watanzania kuipenda na kuithamini nchi yao huku wakitunza miundombinu ya usafirishaji iliyojengwa na iliyoboreshwa na Serikali kupitia uwekezaji mkubwa uliofanyika kwa nia njema ya kushughulikia changamoto za usafiri nchini.
“Serikali imewekeza fedha nyingi katika ujenzi wa miundombinu ya usafirishaji hivyo ni jukumu la kila mwananchi kuilinda na kuitunza kwa kuwa inasaidia katika kukuza uchumi. Kuharibu miundombinu iliyopo kunaleta athari sio kwa Serikali pekee bali kwa wananchi na wasafirishaji ambao wamewekeza katika huduma za usafiri na usafirishaji na hivyo kurudisha nyuma maendeleo,” ameeleza Mhe. Kihenzile.
Maonesho ya Maadhimisho ya kwanza ya Wiki ya Usafiri Endelevu Ardhini yanafanyika Novemba 24 hadi 29, 2025 katika viwanja vya Mnazi Mmoja Dar es Salaam ambapo wadau wa usafirishaji kutoka ndani na nje ya nchi wanatoa elimu ya majukumu yao pamoja na huduma kwa wananchi.

