
Mhe. Mwanahamisi Munkunda, Mkuu wa Wilaya ya Mwanga Mkoa wa Kilimanjaro, ameipongeza Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) kwa kuongeza fursa za ajira kwa maafisa usafirishaji wa pikipiki za magurudumu mawili na matatu kupitia Vyama vya Ushirika wa Akiba na Mikopo (SACCOS).
Mhe. Munkunda ametoa pongezi hizo Juni 6, 2025 ofisini kwake alipotembelewa na DCP Johansen Kahatano, Mkurugenzi Udhibiti Usafiri wa Barabara LATRA pamoja na viongozi wa Chama cha Ushirika wa Akiba na Mikopo cha Wamiliki na Madereva wa Pikipiki za Magurudumu Mawili na Matatu Mkoani Kilimanjaro (KIBABOT SACCOSS).
“Nawapongeza sana kwa jitihada za kutengeneza ajira kwa vijana kwa kuhakikisha wanaunda vyama vya ushirika na kizuri zaidi mnawapatia asilimia 20 ya kamisheni kutoka kwenye ada za leseni zinazopatikana kwa kufanya kazi ya uwakala wa LATRA, jambo hili ni zuri sana na mnatekeleza kwa vitendo maono ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha vijana wanapata ajira, wanainuka kiuchumi na wanaachana na utegemezi,” amesema Mhe. Munkunda.
Ameongeza kuwa, LATRA inafanya mabadiliko makubwa ya uendeshaji na udhibiti katika sekta ya usafiri ardhini kwa kushirikiana na wadau na kwa sasa inaonesha wazi kuwa sekta imeboreshwa na huduma zinatolewa kwa uwazi, uweledi na ufanisi huku wadau wakifurahia ushirikishwaji katika masuala mbalimbali yanayohusu sekta yao.
Pia, amewapongeza viongozi wa KIBABOT SACCOSS kwa kukubali na kufanyia kazi wazo la LATRA la kuanzisha ushirika ambao umekuwa wenye tija kwao kwa kuwawezesha kuinuana kijamii, kiuchumi na kuongeza fursa za uwekezaji kama ushirika pamoja na kupata fursa ya kukopeshana na kukopesheka kwa maendeleo ya wanachama na ushirika kwa jumla.
“Mmeniambia mnatanua wigo wa SACCOS yenu, natamani Wilaya ya Mwanga iwe ya kwanza kuwa na tawi la KIBABOT SACCOS, na maafisa wasafirishaji wa hapa wapo tayari kwa hilo nasi tunawaunga mkono,” amesisitiza Mhe. Munkunda.
Mamlaka inafanya jitihada za kuwahimiza wamiliki na madereva wa pikipiki za magurudumu mawili (bodaboda) na pikipiki za magurudumu matatu (bajaji) kujiunga pamoja na kuanzisha vyama vya ushirika ili kuboresha hali zao za maisha kijamii na kiuchumi.