Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

MHE. MWAKIBETE: LATRA ENDELEENI KUCHUKUA HATUA
Imewekwa: 05 Aug, 2023
MHE. MWAKIBETE: LATRA ENDELEENI KUCHUKUA HATUA

Mhe. Atupele Fred Mwakibete (Mb), Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi (Uchukuzi) ameitaka Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) kuendelea kuchukua hatua dhidi ya wasafirishaji na madereva wanaokiuka Sheria, kanuni na taratibu za usafirishaji kwa magari ya abiria na magari ya mizigo.

Mhe. Mwakibete ameyasema hayo tarehe 1 Agosti, 2023 alipotembelea banda la LATRA katika Maonesho ya Kimataifa ya Wakulima Nanenane viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya ambapo ameipongeza Mamlaka hiyo kwa kazi nzuri ya udhibiti wa huduma za usafiri wa abiria na mizigo kwa kutumia mifumo ya TEHAMA, kuchukua hatua stahiki kwa wasafirishaji wanaokiuka Sheria na kutoa elimu kwa Umma kwa kuwafikia wadau kwa njia mbalimbali.

“Niwapongeze LATRA kwa kuendelea kuwa Mamlaka inayoweza kudhibiti huduma za usafiri ardhini, nimeona namna ambavyo mnachukua hatua za kiudhibiti hususan katika kutoa adhabu kwa kampuni na madereva ambao hawazingatii taratibu ambazo tumejiwekea wenyewe. Hii inapunguza ajali ambazo zinaepukika, dereva anapozidisha ukomo wa mwendo au kuyapita magari mengine sehemu ambazo hairuhusiwi, anakuwa anatengeneza ajali,” alisema.

Aliongeza kuwa anafahamu wapo baadhi ya watu ambao wanachezea Mfumo wa Kufuatilia Mwenendo wa Magari (VTS) na kusababisha gari husika kutoonekana katika mfumo, kwa kufanya hivyo anakuwa anakusudia kufanya kosa hivyo lazima mamlaka ichukue hatua kwa wasafirishaji na madereva wa aina hiyo.

Aidha ameisihi LATRA kuendelea na kazi ya  kuthibitisha madereva na kusajili wahudumu kama ilivyopangwa na kuwa utekelezaji huo ni muhimu kwa kuwa unaiwezesha Serikali kusimamia huduma za usafiri na usalama wa usafiri kwa ufanisi zaidi. Mhe. Mwakibete alisisitiza kuwa Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi itaendelea kushirikiana na LATRA na wako tayari kutatua changamoto zitakazokwamisha utekelezaji wa majukumu ya mamlaka hiyo.

“Kupita mifumo ya TEHAMA ikiwemo huu wa kufuatilia mwenendo wa mabasi inarahisisha kuchuka hatua sahihi kwa wakati, kila anayefanya makosa aadhibiwe kwa makosa yake, kwa bahati nzuri mimi ni Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Usalama Barabarani, Mwenyekiti wetu ni Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, hivyo mtuletee mambo ambayo mnaona yanawapa changamoto tuyafanyie maamuzi na sisi tutaitisha vikao vya maamuzi kwa haraka,” alisema.

Alisisitiza kuwa, kila mdau anapaswa kutimiza wajibu wake kuepusha ajali ili kuokoa maisha ya watanzania kwa kuwa huduma ya usafiri ni huduma ya lazima na inanafasi kubwa katika uchumi wa nchi yetu hivyo LATRA iendelee kutoa elimu katika matamasha na vyombo mbalimbali vya habari ili kufikisha elimu kwa wadau wengi zaidi.

Naye Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano LATRA bw. Salum Pazzy alisema kuwa, LATRA imejipanga kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi kipitia mifumo ya TEHAMA ambapo huduma za utoaji wa leseni, kusimamia viwango vya huduma za usafiri wa abiria na mizigo kibiashara, uthibitishaji wa madereva na usajili wa wahudumu wa vyombo vya usafiri vya kibiashara unawezeshwa kupitia mifumo mbalimbali ikiwemo mfumo wa VTS, Mfumo wa Kutahini Madereva na Mfumo tumizi wa LATRA (LATRA App) unaowawezesha abiria kujua viwango vya nauli vilivyoidhinishwa na LATRA kwa mabasi ya njia ndefu na mabasi ya mijini.

“LATRA imejipanga kutoa elimu kwa wadau na kuongeza tija kupitia mifumo ya TEHAMA ikiwemo mfumo tumizi wa LATRA ambao unaopatikana katika tovuti ya LATRA na kupitia ‘Play Store’ ambapo abiria anaweza kuupakua kwa simu janja na kupata taarifa mbalimbali za abiria ikiwemo kujua viwango vya nauli na kuhakiki uhai wa leseni za LATRA. Kwa siku za usoni mfumo huu utamuwezesha abiria aliyekata tiketi kujua basi analotarajia kupanda lilipo,” alisema.

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo