Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

MHE. NG'WILABUZU -TUNZENI MIUNDOMBINU YA RELI
Imewekwa: 19 Aug, 2022
MHE. NG'WILABUZU -TUNZENI MIUNDOMBINU YA RELI

Na. Mambwana Jumbe

Mkuu wa Wilaya ya Ilala Mhe. Ng'wilabuzu Ndatwa Ludigija amewataka wakazi wa mkoa wa Dar es Salaam kuwa mabalozi wa dhati katika kuilinda na kuitunza miundombinu ya reli hapa nchini.  

Mhe. Ludigija amesema hayo leo Agosti 19, 2022 alifungua mkutano wa wadau wa kukusanya maoni kuhusu viwango vya nauli za treni za abiria kwa mkoa wa Dar es Slaam ulioandaliwa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA).

Aidha, Mhe. Ludigija amesema Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa kwa umahiri na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan inafanya juhudi za kipekee na inatekeleza kazi kubwa ya kuitunza miundombinu ya reli na kuboresha huduma za reli hapa nchini hivyo ni wajibu wa kila mmoja kuhakikisha anaitunza miundombiu hiyo kwa manufaa mapana ya Taifa.

“Niwapongeze sana LATRA kwa kuwashirikisha wadau na hili ndilo jambo ambalo Rais wetu Samia Suluhu Hassan anasisitiza kila mara kwa kuwa huu ndio msingi wa Utawala Bora na hata nauli zitakazokuja kutangazwa hapo baadae zitakuwa zimezingatia maoni ya wadau wa sekta hii ya reli hapa nchini.”

Vilevile Mhe. Ludigija amesema kuwa,  kazi ya kukusanya maoni inayofanywa na LATRA ni kwa mujibu wa Sheria hivyo, amewasihi wadau hao kuzingatia umuhimu wa kazi hiyo na watimize wajibu wao kwa kuwa wanawakilisha wadau wengine ambao kutokana na sababu mbalimbali wameshindwa kuhudhuria mkutano huo.

Aidha, Mhe. Ludigija amewapongeza watumishi wa LATRA kwa kutekeleza majukumu yao kwa weledi na ufanisi huku wakitatua changamoto zinazojitokeza kwenye sekta wanazosimamia   “Ni miaka mitatu tu tangu taasisi hii iundwe lakini imekuwa ni miongozi mwa taasisi za mfano, binafsi nakupongeza sana Mkurugenzi Mkuu kwa kuwa na timu inayofanya kazi vizuri na inayojituma”.

Naye Mkurugenzi Mkuu LATRA CPA Habibu Suluo amesema kwa Mujibu wa Kifungu cha 19 cha Sheria ya LATRA, Sura Na. 413 na Kanuni za Tozo (The Land Transport RegulatoryAuthority (Tariff) Regulations) za Mwaka 2020, LATRA ina jukumu la  kupanga na kufanya mapitio ya tozo (nauli) ya huduma zinazodhibitiwa katika usafiri wa ardhini (barabara, reli na waya).

CPA Suluo ameongeza kuwa ili LATRA iweze kupanga tozo (nauli), mtoa huduma anayedhibitiwa anapaswa kuwasilisha maombi kwa LATRA. Baada ya kupokea maombi, LATRA humpa mtoa huduma nafasi ya kuwasilisha mapendekezo yake kwa wadau na pia kuwapa fursa wadau kutoa maoni yao juu ya mapendekezo yatakayowasilishwa. Hivyo, LATRA ilipokea maombi ya TRC ili apewe nafasi ya kuwasilisha kwa wadau na leo ndio wameanza mchakato huo.

“Natoa wito kwa wadau mbalimbali kuitumia vizuri nafasi hii, ili kuwawezesha wataalamu wetu wafanye kazi yao kwa ufanisi na weledi wa hali ya juu”, ameeleza CPA Suluo

CPA Suluo ameongeza kuwa, kwa wadau ambao wangependa kuwasilisha maoni yao kwa maandishi wanayo nafasi ya kuwasilisha katika Ofisi ya Mkurugenzi Mkuu S.L.P. 3093, Dar es Salaam iliyopo katika Jengo la Mamlaka, Barabara ya Nkrumah kabla ya tarehe 31 Agosti, 2022, na maoni yanaweza kutumwa kwa barua pepe kupitia anuani hizi: info@latra.go.tz na dg@latra.go.tz

Hivi karibuni Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) ilipokea maombi kutoka Shirika la Reli Tanzania (TRC) ikiomba ongezeko la nauli kwa asilimia 15 kwa abiria wanaotumia usafiri wa treni Tanzania Bara. LATRA itafanya mikutano mengine kwa mikoa ya Kigoma, Mwanza na Arusha ili kuwafikia wadau na kupata maoni zaidi kuhusu pendekezo la nauli hizo.

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo