
CPA Habibu Suluo, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) amesema katika Miaka Minne ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, LATRA inajivunia kubuni na kukuza matumizi ya mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kwenye utoaji wa huduma za usafiri ardhini nchini.
CPA Suluo amebainisha hayo kwenye mkutano na Wahariri na Waandishi wa Habari ulioratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina Aprili 14, 2025, Chuo cha Taifa cha Utalii Dar es Salaam.
CPA Suluo ameitaja mifumo iliyobuniwa na inayotumiwa na LATRA kuwa ni Mfumo wa Usimamizi wa Taarifa za Reli na Barabara (Railway and Road Information Management System - RRIMS), Mfumo wa Kufuatilia Mwenendo wa Magari (VTS), Mfumo Tumizi wa LATRA (LATRA App), Mfumo Jumuishi wa Utoaji Tiketi (CeTS) unaofahamika kwa jina la Safari Tiketi, Mfumo Shirikishi wa Huduma kwa Wateja pamoja na Mfumo wa e-Mrejesho.
“Mfumo wa RRIMS unawezesha utoaji leseni, usajili madereva, malipo na taarifa za udhibiti uliounganishwa na mifumo ya taasisi nyingine za serikali kama vile TRA, TIRA, NIDA, GePG na BRELA ili kurahisisha uhakiki wa taarifa za mteja. Pia, unamwezesha msafirishaji kufanya maombi ya leseni na huduma zake pamoja na kuchapa leseni iliyoidhinishwa ndani ya saa 24 bila uhitaji wa kufika ofisi za LATRA, na hivyo kupunguza kwa kiwango kikubwa usumbufu na muda wa kupata huduma,” ameeleza CPA Suluo.
Kwa upande wa Mfumo wa VTS, CPA Suluo amesema kuwa ni mfumo unaosimamia usalama wa huduma unaotumia ‘Satelite’, Kifaa cha Kufuatilia Mwenendo wa Magari (VTD), Mtandao wa Mawasiliano na Vifaa vya Uhifadhi Data Taarifa (GPS Data Servers) vinavyofanya kazi kwa pamoja ili kutuma taarifa za mwenendo wa safari za chombo husika.
“Kufikia Machi 2025, jumla ya magari 11,826 yalikuwa yameunganishwa kwenye mfumo ambapo kati ya hayo, magari 8,969 yanayotuma taarifa kwenye mfumo mpaka sasa. Katika magari yasiyotuma taarifa, baadhi hayapo barabarani kutokana na sababu mbalimbali kama vile Matengenezo ya muda mrefu, ajali, kuungua moto na baadhi yamebadili njia na kuhamia kwenye njia ambazo hazina uhitaji wa kufunga VTS,” ameeleza CPA Suluo.
Pia, ameutaja Mfumo Tumizi wa LATRA (LATRA App) unaopatikana kwenye simujanja ‘Play Store’ za aina ya Android, unamuwezesha mwananchi kupata taarifa za nauli za mabasi, kutambua uhalali wa leseni za magari na adhabu, hivyo kumuwezesha abiria kuepuka kutumia gari lenye changamoto ili kujiepusha na usumbufu.
CPA Suluo amesema LATRA kwa kushirikisna na wadau wametengenza Mfumo Jumuishi wa Utoaji Tiketi (CeTS) au Safari Tiketi uliounganishwa na mifumo mingine ya utoaji tiketi ukiwemo wa TRC na mifumo ya tiketi za mabasi ili kurahisisha ukataji tiketi na kutunza taarifa za abiria ambapo ukikamilika utaelekezwa kwenye mabasi ya mijini (daladala) na usafiri wa kukodi.
“Tangu kuanza kuunganisha mifumo ya Tiketi za Kielektroni kwenye CeTS, tarehe 02/08/2024 hadi tarehe 31/03/2025, taarifa zetu zinaonesha jumla ya abiria (miamala ya tiketi za kielektroniki) 13,429,549 ilifanyika kwenye CeTS. Idadi hii ni sawa na wastani wa abiria (miamala) 58,137 zinaonekana kwa siku, sawa na wastani wa abiria (miamala) 1,744,100 kwa mwezi katika kipindi hicho cha siku 231, takriban miezi nane tangu kuanza kutumia mfumo huu,” amefafanua CPA Suluo.
Vilevile amesema LATRA inapokea na kushughulikia malalamiko ya wananchi na kuyashughulikia kutumia Mfumo Jumuishi wa Huduma kwa Wateja ambapo mwananchi anaweza kupiga simu bila malipo kwa namba 0800110019 au 0800110020 na pamoja na Mfumo wa Kutuma, Kupokea na Kufuatilia Malalamiko, Mapendekezo, Maulizo na Pongezi (eMrejesho) unaopatikana kwa anwani https://emrejesho.gov.go.tz/ kwa kupakua mfumo tumizi wa e-Mrejesho au kwa kutumia simu kwa njia ya msimbo (USSD) au kwa kupitia tovuti ya LATRA www.latra.go.tz sehemu ya tovuti mashuhuri.
LATRA itaendelea kubuni mifumo ya TEHAMA kwa kuwa inarahisishisha utendaji kazi, inaboresha na kurahisisha utoaji wa huduma kwa wadau pamoja na kuwapunguzia muda na gharama za kupata huduma wanazozihitaji.