Bi. Mwadawa Sultan, Kaimu Mkurugenzi Mkuu Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) amesema, mazingira salama na yanayotunzwa vizuri ni msingi muhimu wa maendeleo endelevu ya Taifa, hivyo kila mmoja anawajibika kushiriki kikamilifu katika juhudi za kuyahifadhi mazingira kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
Bi. Mwadawa amesema hayo Juni 5, 2026 alipotembelea banda la LATRA kwenye maonesho ya Wiki ya Mazingira yaliyofanyika Juni 1 hadi 5, 2026 viwanja vya Kituo cha Mikutano cha Jakaya Kikwete jijini Dodoma yenye kaulimbiu isemayo, Dira 2050: Tuwajibike Kuyatunza Mazingira, ambapo LATRA ni miongoni mwa taasisi zinazoshiriki kutoa elimu kwa wadau wa usafiri ardhini kuhusu umuhimu wa utunzaji wa mazingira.
Ameeleza kuwa, wajibu wa LATRA katika kulinda mazingira umeainishwa katika Kifungu cha 6 cha Sheria ya Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini, Sura ya 413, ambacho kinaelekeza Mamlaka kukuza usalama katika sekta zinazodhibitiwa, ikiwemo usalama wa watumiaji wa huduma za usafiri ardhini.
Pia amesema LATRA imeendelea kuhakikisha watoa huduma na watumiaji wa huduma za usafiri ardhini wanazingatia utunzaji wa mazingira kupitia masharti mbalimbali yanayowekwa katika leseni za usafirishaji pamoja na elimu endelevu inayotolewa kwa wadau wa sekta ya usafiri ardhini.
Amebainisha kuwa, mbali na matakwa ya kisheria LATRA imechukua hatua za ziada kwa kutekeleza misingi ya uendelevu katika utekelezaji wa majukumu ya kila siku kupitia Sera ya Mazingira, Jamii na Utawala Bora (ESG), inayolenga kuhakikisha shughuli za Mamlaka zinaendeshwa kwa kuzingatia matumizi bora ya rasilimali na uhifadhi wa mazingira.
“Tunatambua kuwa utunzaji wa mazingira unaanzia ndani ya taasisi zetu, ndio maana tumeendelea kuhimiza matumizi ya mifumo ya kidigiti katika utoaji wa huduma za usafiri ardhini na utekelezaji wa majukumu yetu ili kupunguza matumizi ya karatasi yanayoharibu na kuleta athari katika mazingira yetu,” amesema Bi. Sultan.
LARA kwa kushirikiana na wadau wa usafiri ardhini inaendeleza juhudi za kuboresha huduma za usafiri ardhini, na kuhakikisha inachukua hatua mbalimbali zinazochangia kulinda mazingira kwa manufaa ya vizazi vijavyo.

