
Dkt. Ally Possi, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi amewaagiza wakuu wa idara za Raslimali watu na Utawala wa taasisi zote za Wizara hiyo kuhakikisha wanaendeleza michezo sambamba na kuongeza ushiriki wa wafanyakazi katika michezo ili timu ya Uchukuzi iendelee kushinda katika mashindano mbalimbali ya baadae na kunufaika na faida za michezo kwa afya za wafanyakazi kama inavyoelekezwa na Serikali.
Ameyasema hayo jana tarehe 27 Julai, 2024 jijini Dodoma katika ufunguzi wa Bonanza maalum la Wizara ya Uchukuzi lililoandaliwa na Shirika la Reli Tanzania (TRC) ikiwa ni sehemu ya hamasa ya ufunguzi wa huduma za Treni za umeme za Reli ya Kisasa (SGR) Dar es Salaam hadi Dodoma. ambapo Dkt. Possi alikuwa mgeni Rasmi.
‘Michezo ni sehemu ya maelekezo ya Serikali, tuendeleze michezo ili tuimarishe afya zetu na kuongeza uwezo wetu wa kuchapa kazi. Bonanza linalofuata la Uchukuzi litafanyika jijini Mwanza na mwenyeji wetu atakuwa ni Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL), ni muhimu tujipange mapema na mimi mwenyewe nitashiriki kucheza mchezo wa riadha’. Alisema
Aidha ametoa pongezi kwa TRC na Uongozi wa Klabu wa Uchukuzi kwa kuwezesha bonanza hilo lililoratibiwa vizuri na kuwezesha wafanyakazi waliojitokeza kwa wingi kushiriki michezo mbalimbali iliyoandaliwa ikiwemo mpira wa miguu, mpira wa pete, kuvuta kamba, michezo ya jadi, riadha na mingineyo.
‘Natoa pongezi kwa wenzetu wa TRC na uongozi wa klabu ya uchukuzi na kamati nzima iliyowezesha bonanza hili, kiupekee nampongeza mwenyekiti wa klabu hii Bw. Andrew Magombana, huyu ni mwanamichezo mzoefu na anayo historia nzuri ya kusimamia michezo.’ Aliongeza
Katika bonanza hilo, Dkt. Possi alitoa medali na vikombe kwa washindi wa michezo iliyochezwa ambapo kwa mpira wa miguu timu ya TRC imepokea kombe la mshindi wa kwanza, kwa mchezo wa kuvuta Kamba wanaume, timu ya Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) iliyoshirikiana na timu ya Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) wamepokea kombe la mshindi wa kwanza na Kamba wanawake timu ya wizara ya Uchukuzi imepokea kombe la mshindi wa kwanza.
Katika utoaji wa vikombe hivyo, CPA Habibu J. Suluo, Mkurugenzi Mkuu LATRA amekabidhiwa na Mgeni Rasmi kombe maalum kwa kuwa Mkuu wa Taasisi aliyewezesha wafanyakazi wengi zaidi kuhudhuria bonanza hilo na yeye mwenyewe kushiriki kikamilifu katika michezo mara kwa mara.
Wachezaji wengine waliokabidhiwa medali ni pamoja na Stamil Mbilu wa Wizara ya Uchukuzi aliyekuwa mshindi wa kwanza kwa mbio za magunia wanawake, Abdul Ukenge wa TRC aliyeibuka mshindi wa kwanza kwa riadha mita 100, Lugano Mwasomola wa LATRA aliyeibuka mshindi wa pili riadha mita 100. Pia Mwasomola amekabidhiwa medali ya mfungaji bora wa mchezo wa mpira wa miguu.
Kwa upande wake, CPA Habibu J. Suluo, Mkurugenzi Mkuu wa LATRA ametoa pongezi kwa TRC na Klabu ya Wizara ya Uchukuzi kwa kuandaa bonanza hilo kwa ufanisi mkubwa na amewasihi wanamichezo kuendeleza umoja wao hadi katika utendaji wa kazi za ofisini ili kuongeza tija katika utendaji wa taasisi zao.
‘Mimi nimekuwa nikishiriki michezo hii mwenyewe bila kutuma muwakilishi, hii ni kwa sababu ninaipa michezo kipaumbele kwa kuwa michezo ni afya, michezo ni umoja na hivyo inaimarisha utendaji wa kazi hadi za ofisini.’ Alisema
Katika hatua nyingine, CPA Suluo ameupongeza uongozi wa TRC kwa kazi nzuri inayoendelea kufanyika katika kutoa huduma za treni ya SGR na kuongeza kuwa, LATRA imepanga nauli inayowalinda watumia huduma wenye kipato cha chini wanaolazimika kutumia daraja la kawaida wanaposafiri na treni hizo, kwa madaraja ya juu TRC wanaruhusiwa kutoza nauli yoyote watakayoona inafaa.
‘Tunapongeza mazuri yanayofanyika, Serikali inaendelea kuzifanyia kazi changamoto chache zilizopo. Pia napenda nitoe zawadi ya LATRA kwa wadau wanaotumia usafiri wa mabasi, tumieni Mfumo wa Taarifa kwa Abiria (PIS) unaopatikana kwa kuingiza anwani pis.latra.go.tz utaweza kuona yalipo mabasi yanayokuja katika kituo ulichopo, muda wa kufika katika kituo husika na utaweza kukagua mwendo wa basi kwa kuingiza namba ya basi hilo katika mfumo’. Alifafanua
Pia Dkt. Possi ametoa wito kwa watanzania kutumia usafiri wa treni za SGR kwa kuwa ni huduma nzuri na ya gharama nafuu inayowawezesha watu wenye vipato tofauti tofauti kutumia usafiri huo.
‘Binafsi nimetumia usafiri wa SGR, ni gharama nafuu na haraka hata ukilinganisha na usafiri wa anga, kuna tofauti kubwa ya gharama. Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan inaendelea kuwekeza katika miundombinu tofauti tofauti ya uchukuzi, tunayo haki ya kujipongeza.’ Alisema