
Mhe. Deus Sangu (Mb), Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora ameisihi Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) kuendelea kutoa elimu kwa wananchi ili kuwaongezea uelewa wa majukumu ya Mamlaka.
Mhe. Sangu amebainisha hayo alipotembelea banda la LATRA kwenye Maonesho ya Kitaifa ya Wiki ya Utumishi wa Umma Juni 20, 2025 viwanja vya Chinangali Park, Dodoma ambapo alielezwa jinsi Mamlaka inavyodhibiti sekta ya usafiri ardhini kwa kutumia mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA).
“Wananchi wanahitaji kuipata elimu hii kwa kina, hivyo ongezeni wigo wa utoaji elimu ili muwafikie wananchi ambao ndio watumiaji wa huduma za usafiri ardhini pamoja na mifumo mnayoendelea kuibuni na kuitumia,” amesema Mhe. Sangu.
Pia, Mhe. Sangu ameipongeza LATRA kwa utendaji kazi mzuri ulioleta mapinduzi makubwa ya uendeshaji na usimamizi wa sekta ya usafiri ardhini ikiwa ni pamoja na kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora kwa wakati kupitia mifumo ya TEHAMA.
“Mnafanya kazi nzuri sana, nimeziona kazi zenu na nimebahatika kushuhudia Mfumo wa Kufuatilia Mwenendo wa Magari (VTS) katika ofisi zenu pale Mikocheni, Dar es Salaam namna unavyofanya kazi na hakika VTS umesaidia kwa kiasi kikubwa kudhibiti ajali nchini,” ameeleza Mhe. Sangu.
Naye Bw. Ezekiel Emmanuel, Afisa Mfawidhi LATRA Mkoa wa Dodoma ameeleza namna LATRA inavyorahisisha upatikanaji wa huduma kwa wananchi kupitia Mfumo wa Usimamizi wa Taarifa za Barabara na Reli (RRIMS) unaopatikana kwa anwani ya https://rrims.latra.go.tz/ .
“Kwasasa msafirishaji anachapa leseni yake popote pale alipo kupitia akaunti yake ya maombi ya leseni ya RRIMS bila yeye kufika katika ofisi za LATRA, na hii inaokoa muda na gharama kwa msafirishaji,” amefafanua Bw. Emmanuel.
Vilevile amebainisha Mfumo wa Taarifa kwa Abiria (PIS) pis.latra.go.tz/ kuwa umerahisisha upatikanaji wa huduma kwa wananchi kwakuwa mwananchi sasa anapata taarifa ya safari popote alipo kupitia simu janja yake na mfumo huo umewekwa kwenye runinga za stendi ya mabasi iliyopo nanenane Dodoma na Stendi ya mabadi Magufuli jijini Dar es Salaam.
Mamlaka inashiriki vyema kutoa elimu kwa wananchi kuhusu shughuli zake za kiudhibiti katika Maonesho ya Kitaifa ya Wiki ya Utumishi kwa Umma yanayofanyika kuanzia Juni 16 hadi 23, 2025 katika viwanja vya Chinangali Park Jijini Dodoma.