Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) kwa kushirikiana na Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) imeendelea kuimarisha ushirikiano wake na wadau wa sekta ya usafiri ardhini, kwa lengo la kuongeza uelewa wa masuala ya bima na kuhakikisha taarifa za bima zinapatikana kupitia Mfumo wa tiketi mtandao ili kulinda haki za abiria na kuwawezesha abiria kupata fidia pindi wanapopata majanga au changamoto wanapokuwa safarini.
Akizungumza katika kikao kilichohusisha wadau wa sekta ya usafiri Ardhini kilichofanyika Februari 17, 2026 Ukumbi wa Mikutano ofisi za LATRA, Dar es Salaam, Bw. Salum Pazzy, Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano LATRA, amesema ni muhimu kwa kila tiketi ya safari anayopatiwa abiria kuwa na taarifa za kampuni ya bima na maboresho yanayotarajiwa kutekelezwa katika mfumo wa tiketi za mtandao yanalenga kuhakikisha taarifa hizo zinakuwepo na zinaonekana wazi kwa abiria ili waweze kuzitambua kwa urahisi.
Ameongeza kuwa, mara kadhaa LATRA imekuwa ikipokea malalamiko mbalimbali kutoka kwa watumiaji wa huduma za usafiri ardhini yanayohusu masuala ya bima na kutokana na ushirikiano mzuri uliokuwepo na TIRA, malalamiko hayo yamekuwa yakishughulikiwa kwa taratibu zilizowekwa.
“Mamlaka imekuwa ikipokea malalamiko yanayohusu masuala ya bima kutoka kwa watumiaji wa huduma za usafiri ardhini, na kwa kushirikiana na TIRA tumekuwa tukiyatatua kwa pamoja. Ushirikiano huu ni endelevu na umeanza tangu hatua za awali za uundaji wa mfumo wa tiketi za mtandao. Maboresho tunayoyafanya yanalenga kumwezesha abiria kufahamu kama tiketi aliyokata ina taarifa za bima na ni kampuni ipi inahusika, ili aweze kupata fidia pindi atakapokumbwa na changamoto kama ajali akiwa safarini,” amesema Bw. Pazzy.
Kwa upande wake, Bw. Christopher Geofrey Mapunda, Mkurugenzi wa Leseni na Msimamizi wa Bima Mtawanyo wa TIRA, amesema kikao hicho kimeandaliwa mahsusi kwa ajili ya kutoa elimu kwa wadau wa sekta ya usafirishaji kuhusu umuhimu wa kuweka jina la kampuni ya bima kwenye tiketi mtandao anayopatiwa abiria.
“Serikali imelenga kuhakikisha tiketi zote za usafiri zinakuwa na taarifa za kampuni ya bima ili, ikitokea ajali au dharura, mwananchi aweze kufahamu hatua za kuchukua na wapi pakuanzia katika kudai haki yake, TIRA itaendelea kusimamia utekelezaji wa miongozo ya bima ili kuhakikisha kampuni za bima zinatekeleza wajibu wao kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa na Serikali, huku ikiendelea kuboresha mifumo ya upokeaji na ushughulikiaji wa malalamiko kutoka kwa wananchi,” amesema Bw. Mapunda.
Akizungumza kwa niaba ya wadau wa usafirishaji, Bw. Joseph Didas, Mkurugenzi wa Kampuni ya Mabasi ya Esther Luxury Coach, amesema kikao hicho kimekuwa na manufaa makubwa kwao kupitia elimu waliyoipata na ametoa pongezi kwa maboresho yanayoenda kufanyika kwa kuwa yatasaidia kuongeza imani kwa wasafirishaji na kulinda haki za abiria.
LATRA imeendelea kushirikisha wadau wa sekta ya usafiri ardhini nchini katika kila hatua ya maboresho ya huduma zinazoenda kutekelezwa kwa lengo la kuhakikisha huduma za usafiri zinakuwa salama, bora na zenye kuzingatia haki za watumiaji.

