Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

KAMATI YA PIC YAITAKA LATRA KUWADHIBITI WANAOCHEZEA VTD
Imewekwa: 17 Feb, 2026
KAMATI YA PIC YAITAKA LATRA KUWADHIBITI WANAOCHEZEA VTD

Mhe. Mha. Johnston Mutasingwa (Mb) Kaimu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu (PIC) ameitaka Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) kuwadhibiti na kuwachukulia hatua kali za kisheria wanaochezea Kifaa cha Kufuatilia Mwenendo wa Magari (VTD) kinachotuma taarifa kwenye Mfumo wa Kufuatilia Mwenendo wa Magari (VTS) kwakuwa wanahatarisha maisha ya wananchi wanaotumia usafiri wa umma.

Mhe. Mutasingwa amebainisha hayo Februari 16, 2026 wakati wajumbe wa Kamati ya PIC walipotembelea ofisi za LATRA Mkoa wa Dar es Salaam ikiwa ni sehemu ya ziara maalum ya kujifunza jinsi LATRA inavyotekeleza majukumu yake kwa mujibu wa Sheria.

“Tumesikitika kuona bado wapo baadhi ya watu wanaochezea mfumo wa VTS hivyo tumeielekeza LATRA kuwafuatilia na kuwadhibiti kwa kuwa wanawaweka hatiani watu wasio na hatia, lakini pia tumewasihi kufanya kazi kwa uweledi, uzalendo na kutimiza majukumu yake kwa ufanisi kwa kuwa LATRA inajukumu kubwa la kulinda uhai wa wananchi wanaotumia usafiri wa umma na kufuatilia vyombo vya moto wanavyovidhibiti,” amesema Mhe. Mutasingwa.

Aidha, Kamati hiyo imeipongeza LATRA kwa kazi nzuri ya kuimarisha mifumo ya udhibiti   ambayo imesaidia kupunguza ajali, “Tunaipongeza Serikali kupitia LATRA kwa kazi nzuri ambayo wanaifanya ya udhibiti ajali kwa njia ya mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA). Tumejionea kazi kubwa inayofanywa hasa uimarishaji wa mifumo ya udhibiti mwendokasi, ambayo ni muhimu sana katika kuimarisha usalama.”

Katika hatua nyingine, Kamati ya PIC aimeiagiza LATRA kushirikiana na vyombo vyingine vya udhibiti na usalama barabarani ili kuhakikisha usafiri ardhini unakuwa bora na salama huku wadau wakitekeleza majukumu yao kwa mujibu wa Sheria, Kanuni na Taratibu zilizowekwa.

Naye CPA, Dkt. Habibu Suluo, Mkurugenzi Mkuu LATRA aliieleza Kamati hiyo kuwa, LATRA imekuwa ikiwafikia wadau wake na kushirikiana nao katika masuala mbalimbali yanayohusu sekta ya usafiri ardhini na wataendelea kushirikiana nao ili kuwa na sekta bora inayoendana na kasi ya mabadiliko ya teknolojia na inayokidhi matakwa ya Serikali, wananchi na wasafirishaji kwa jumla.

Ziara hiyo ya siku moja imetoa fursa kwa wajumbe wa Kamati ya PIC kujionea jinsi LATRA inavyotumia mifumo ya TEHAMA kuhudumia wadau wake na pia walishuhudia moja kwa moja utahini wa madereva wa vyombo vya moto kibiashara unavyofanyika, hatua inayolenga kuhakikisha madereva wanazingatia Sheria Kanuni na Taratibu za usalama barabarani. Ziara hiyo ilitoa nafasi ya kubadilishana uzoefu na kuimarisha ushirikiano kati ya Kamati na LATRA katika kuendeleza sekta ya usafiri nchini.

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo