Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

PROF. KAHYARARA AIPA KONGOLE LATRA KWA KUIMARISHA HUDUMA ZA USAFIRI KUPITIA TEHAMA
Imewekwa: 07 Aug, 2026
PROF. KAHYARARA AIPA KONGOLE LATRA KWA KUIMARISHA HUDUMA ZA USAFIRI KUPITIA TEHAMA

Prof. Godius Kahyarara, Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, ameipongeza Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) kwa matumizi ya mifumo ya kisasa ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ambayo imeendelea kuimarisha utoaji wa huduma za usafiri, kuongeza uwazi, ufanisi na kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa wananchi.

Prof. Kahyarara ametoa pongezi hizo Agosti 7, 2026 alipotembelea banda la LATRA katika Maonesho ya Kimataifa ya Kilimo (Nanenane), viwanja vya John S. Malecela, jijini Dodoma ambapo akiwa katika banda hilo, alipata fursa ya kujionea mifumo mbalimbali ya kidigiti inayotumiwa na Mamlaka katika kusimamia sekta ya usafiri ardhini na kuhudumia wadau kwa ufanisi zaidi.

Akizungumza baada ya kupokea maelezo kuhusu mifumo hiyo, Prof. Kahyarara amesema matumizi ya TEHAMA ni msingi muhimu wa kuboresha utendaji wa taasisi za umma na kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora, za haraka na zenye uwazi. Ameeleza kuwa, juhudi za LATRA katika kuwekeza kwenye mifumo ya kidigiti zinaendana na dira ya Serikali ya kujenga uchumi wa kidigiti na kuongeza ubora wa huduma kwa wananchi.

Bw. Salum Pazzy, Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano LATRA amemueleza Prof. Kahyarara kuwa Mifumo ya TEHAMA ya LATRA inayotumika na iliyochangia kuleta mapinduzi katika sekta ya usafiri ardhini ni Mfumo wa Safari Tiketi, Mfumo wa Taarifa kwa Abiria (PIS), Mfumo Tumizi wa LATRA App, Mfumo wa Usimamizi wa Taarifa za Reli na Barabara (RRIMS), Mfumo wa Kutahini Madereva (DTS) pamoja na Mfumo wa Kufuatilia Mwenendo wa Magari (VTS).

Akitoa taarifa kuhusu ushiriki wa LATRA katika maonesho hayo, Bw. Pazzy amesema  Mamlaka imeshiriki maonesho hayo tangu Agosti 1, 2026, kwa lengo la kuwafikia wananchi na wadau mbalimbali kwa kutoa elimu kuhusu majukumu ya LATRA pamoja na mifumo ya TEHAMA inayorahisisha upatikanaji wa huduma za usafiri na usafirishaji.

"Tangu kuanza kwa maonesho haya, tumekuwa tukitoa elimu kwa wananchi kuhusu majukumu ya Mamlaka na kuwafahamisha namna mifumo yetu ya kidigiti inavyorahisisha upatikanaji wa huduma, kuongeza uwazi katika utoaji wa huduma na kuimarisha usimamizi wa sekta ya usafiri ardhini nchini," amesema Bw. Pazzy.

Ameongeza kuwa, ushiriki wa LATRA katika maonesho hayo ni sehemu ya mkakati wa Mamlaka wa kuendelea kusogeza huduma karibu na wananchi, kupokea maoni na mapendekezo yao, kujibu maswali yanayohusu sekta ya usafiri na kuhamasisha matumizi ya mifumo ya TEHAMA iliyobuniwa na kutumiwa na LATRA.

Vilevile amesema, kupitia maonesho hayo, wananchi wamepata fursa ya kujifunza kwa vitendo namna mifumo ya TEHAMA ya LATRA inavyorahisisha upatikanaji wa huduma, kuimarisha usimamizi wa sekta ya usafiri na kuchangia utekelezaji wa dhamira ya Serikali ya kutumia teknolojia kuboresha utoaji wa huduma kwa umma.

Kwa kuendelea kuwekeza katika mifumo ya kisasa ya TEHAMA, LATRA inaimarisha dhamira yake ya kujenga sekta ya usafiri iliyo salama, yenye ufanisi, uwazi na inayokidhi mahitaji ya wananchi na wadau. Ushiriki wa Mamlaka katika Maonesho ya Nanenane unaendelea kuwa jukwaa muhimu la kuelimisha umma, kusogeza huduma karibu na wananchi na kuonesha mchango wa teknolojia katika kuboresha utoaji wa huduma za usafiri ardhini, sambamba na maono ya Serikali ya kujenga uchumi wa kidigiti na huduma za umma zenye ubora.

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo

slot gacor