Prof. Makame Mbarawa (Mb), Waziri wa Uchukuzi amesema kuwa, tiketi za kielektroni zimeendelea kuwanufaisha abiria wanaotumia huduma za usafiri wa mabasi ya mijini na nchi jirani kwa kuwawezesha kununua tiketi zao za safari kwa urahisi kwa njia ya mtandao kupitia Mfumo Jumuishi wa Utoaji Tiketi (CeTS) unaojulikana kwa jina la Safari Tiketi unaopatikana kwa njia ya tovuti tiketi.latra.go.tz/ au kwa kupakua kwenye simu janja bila kukumbana na changamoto za ulanguzi wa nauli.
Prof. Mbarawa amesema hayo Mei 13, 2026 Bungeni Dodoma alipowasilisha hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Uchukuzi kwa mwaka wa fedha 2026/27 na kueleza kuwa, hadi kufikia mwezi Machi 2026 zaidi ya abiria milioni 21 wamefanikiwa kununua tiketi zao kwa njia ya mtandao kupitia Mfumo wa Safari Tiketi unaorahisisha ukataji wa tiketi na kutunza taarifa sahihi za abiria.
Prof. Mbarawa amesema, matumizi ya tiketi za kielektroni imewawezesha abiria kununua tiketi zao kwa urahisi kupitia simu za mkononi na majukwaa ya kidigiti na kupunguza changamoto zilizokuwa zikikabili sekta ya usafiri, ikiwemo msongamano wa abiria vituoni, ucheleweshaji wa safari pamoja na mianya ya upotevu wa mapato, hali iliyoongeza ufanisi na uwazi katika usimamizi wa huduma za usafiri ardhini.
Ameongeza kuwa, hadi kufikia Machi mwaka huu, jumla ya mabasi 8,126 yalikuwa yameunganishwa kwenye mfumo wa Safari Tiketi, hatua iliyowezesha abiria wengi kupata huduma kwa urahisi zaidi bila usumbufu wa kupata tiketi kwa njia za kawaida.
Vilevile amesema, LATRA imeendelea kusimamia utekelezaji wa matumizi ya tiketi za kielektroni kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa sekta ya usafiri, hatua inayolenga kuhakikisha teknolojia inakuwa sehemu muhimu ya kuboresha huduma kwa wananchi, kuongeza tija, kuimarisha ukusanyaji wa taarifa muhimu za safari pamoja na kulinda haki za abiria na watoa huduma.
LATRA imeendelea kuwasihi wananchi kutumia tiketi za kielektroni wanapopanga safari zao ili kuhakikisha wanapata huduma salama, za uhakika na kuepuka kutozwa nauli zisizoidhinishwa.

