Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

PROF. MBARAWA AITAKA BODI YA WAKURUGENZI LATRA KUISIMAMIA MENEJIMENTI YA MAMLAKA
Imewekwa: 11 Jul, 2023
PROF. MBARAWA AITAKA BODI YA WAKURUGENZI LATRA KUISIMAMIA MENEJIMENTI YA MAMLAKA

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhe. Prof. Makame Mnyaa Mbarawa (Mb) ameitaka Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) kuisimamia Menejimenti ya Mamlaka hiyo ili itekeleze vyema majukumu yake kwa mujibu wa Sheria, Kanuni na Taratibu zilizopo.

Mhe. Prof. Mbarawa amesema hayo alipokuwa akizindua Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) inayoongozwa na Mwenyekiti Prof. Ahmed Mohamed Ame pamoja na wajumbe wengine sita akiwemo, Bi. Neema Joseph Ringo, Bw. Nuru Mohamed Ngoma, Mha. Michael Paul Kisaka, Bw. Allen Thobias Marwa, Wakili Tumaini Elisamia Silaa pamoja na Mha. Lucian Mafikiri Henry Kilewo

Uzinduzi wa Bodi hiyo umefanyika Julai 11, 2023 katika ofisi za LATRA Mkoa wa Dar es Salaam na kuhudhuriwa na wajumbe wa Bodi mpya, waliomaliza muda wake, Menejimenti ya LATRA pamoja na waandishi wa habari.

“Jukumu kubwa la Bodi ni kuisimamia Menejimenti, sio kufanya kazi za Menejimenti. Bodi ipate mafunzo ya kutosha (Induction Program) na kufanya ziara za kujifunza ili kutekeleza vyema majukumu yake,” ameeleza Prof. Mbarawa.

Vilevile, Mhe. Mbarawa ameielekeza Bodi hiyo kusimamia mapato na matumizi ya Mamlaka na kuhakikisha mchango wa asilimia 15 ya mapato ghafi yanawasilishwa kwenye Mfuko wa Mkuu wa Serikali kwa mujibu wa Sheria na taratibu zilizopo.

Aidha, maelekezo mengine aliyoyatoa Mhe. Prof. Mbarawa kwenye hotuba yake ni pamoja na Kuweka utaratibu wa Mamlaka kukutana na wadau wake kila mwaka na kutoa elimu juu ya shughuli za Mamlaka pamoja na kushirikisha kikamilifu wadau wa Mamlaka hususan sekta binafsi kabla ya Mamlaka haijafanya maamuzi yanayoathiri utoaji wa huduma zinazodhibitiwa,

Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Uchukuzi)- Bw. Gabriel Migire, Bw. Ahmed Mbegu amewapongeza wajumbe wa Bodi iliyomaliza muda wake kwa kuiwezesha LATRA kupata mafanikio yaliyopo na amesema ofisi ya Katibu Mkuu Uchukuzi inaiahidi Bodi mpya kupata ushirikiano pale utakapohitajika.

Naye Mkurugenzi Mkuu LATRA CPA Habibu Suluo amemshukuru Mhe. Mbarawa kwa kuzindua Bodi ya Wakurugenzi na ameahidi kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa Sheria na Kanuni zilizopo huku akizingatia kwa weledi, umahiri na mshikamano na Bodi hiyo pamoja na wadau wote wa sekta ya udhibiti usafiri ardhini nchini.

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo