Mhe. Prof. Makame Mbarawa (Mb), Waziri wa Uchukuzi, amesema Serikali ya Awamu ya Sita inaendelea kuwekeza katika miradi mikubwa ya reli, bandari na usafiri wa majini ili kujenga mfumo jumuishi wa uchukuzi (Integrated Transport System) utakaorahisisha usafirishaji wa abiria na mizigo, kuongeza ufanisi wa huduma za usafiri na kuchochea ukuaji wa uchumi wa Taifa.
Prof. Mbarawa amesema hayo Julai 20, 2026 katika Bandari ya Kigoma, wakati wa hafla iliyoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ya uzinduzi wa meli nne za mizigo katika Ziwa Tanganyika, uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa Gati la Abiria na Mizigo katika Bandari ya Kigoma, pamoja na uwekaji wa jiwe la msingi la mradi wa ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) kipande cha sita kutoka Tabora hadi Kigoma.
Amesema uwekezaji huo ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuiwezesha Tanzania kuwa kitovu cha biashara na usafirishaji katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati kupitia mfumo unaounganisha reli, bandari na viwanja vya ndege ili kuongeza ufanisi wa usafirishaji wa watu na mizigo.
"Miradi hii yote kwa pamoja inaonesha dhamira ya Serikali ya kujenga mfumo jumuishi wa uchukuzi ambapo reli ya kisasa, bandari na usafiri wa anga vinafanya kazi kwa kushirikiana. Utekelezaji wa miradi hii utaifanya Kigoma kuwa kitovu cha usafirishaji kinachounganisha Ziwa Tanganyika, Ushoroba wa Kati na nchi za Afrika Mashariki na Kati," amesema Prof. Mbarawa.
Ameeleza kuwa mradi wa Reli ya Kisasa (SGR) kutoka Tabora hadi Kigoma wenye urefu wa kilometa 506 utaunganisha Bandari ya Dar es Salaam na mikoa ya Magharibi pamoja na masoko ya nchi jirani kupitia reli yenye uwezo mkubwa wa kusafirisha abiria na mizigo kwa haraka, usalama na gharama nafuu.
Aidha, amesema utekelezaji wa mradi huo utaongeza ushindani wa uchumi wa Taifa, kurahisisha usafirishaji wa abiria na mizigo, pamoja na kufungua fursa mpya za uwekezaji, biashara na ajira ndani na nje ya nchi.
Pia amesema, Wizara ya Uchukuzi, kwa kushirikiana na taasisi zilizo chini yake, itaendelea kusimamia utekelezaji wa miradi yote ya kimkakati kwa weledi, kuhakikisha inakamilika kwa wakati, kwa viwango vinavyotakiwa na kwa kuzingatia thamani ya fedha za umma ili kuendelea kuimarisha sekta ya uchukuzi na kuchochea maendeleo ya uchumi wa Taifa.
Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) imeshiriki katika hafla hiyo ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa jukumu la kudhibiti huduma za usafiri wa reli ambapo LATRA inasimamia usalama, ufanisi na ubora wa miundombinu ya Reli nchini.

