Mhe. Prof. Makame Mbarawa (Mb), Waziri wa Uchukuzi amesema kuwa Serikali kupitia Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) imeendelea kuboresha huduma za usafiri ardhini nchini kupitia matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) hatua inayochangia kuongeza ufanisi na ubora wa utoaji huduma kwa wananchi.
Prof. Mbarawa amesema hayo Mei 13, 2026 alipowasilisha hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Uchukuzi kwa mwaka wa fedha 2026/27 Bungeni Dodoma na kueleza kuwa, katika kipindi cha mwezi Julai, 2025 hadi kufikia mwezi Machi mwaka huu LATRA imeendelea kuboresha usimamizi wa huduma na kupunguza changamoto za kiutendaji na kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa wananchi kupitia mifumo madhubuti ya TEHAMA.
Vilevile amesema, LATRA imeendelea kuimarisha usalama wa abiria kupitia mifumo ya TEHAMA mabapo LATRA inaweza kufuatilia mabasi mengi kwa wakati mmoja kupitia Mfumo wa kufuatilia Mwenendo wa Magari (VTS) na kudhibiti mienendo ya madereva wanapokuwa safarini.
“Jumla ya mabasi 13,843 yameunganishwa kwenye Mfumo wa VTS unaowezesha kufuatilia mwenendo wa mabasi yanapokuwa safarini na kusaidia kudhibiti mwendokasi pamoja na matukio yanayoweza kuhatarisha usalama wa abiria na mali zao,” amesema Prof. Mbarawa.
Aidha amesema, Mamlaka imesajili jumla ya madereva 12,699 kupitia mifumo ya kidigiti, hatua inayosaidia kuhakikisha madereva wanazingatia Sheria, Kanuni na Taratibu za usafirishaji nchini.
Ameongeza kuwa, huduma ya utoaji leseni za usafirishaji kwa vyombo vya moto vinavyodhibitiwa na LATRA imeongezeka kwa kasi ukilinganisha na mwaka uliopita, hali inayochangiwa na ufanisi wa mifumo ya kidigiti inayotumiwa kutoa huduma za LATRA.
“Kuanzia mwezi Julai, 2025 hadi Machi, 2026 LATRA imefanikiwa kutoa jumla ya leseni 388,715 sawa na ongezeko la asilimia 55% ya mwaka uliopita. Leseni hizi hutolewa kupitia Mfumo mama wa Mamlaka ambao ni Mfumo wa Usimamizi wa Taarifa za Barabara na Reli (RRIMS) kwa magari ya abiria, magari ya mizigo na magari ya kukodi,” amesema Prof. Mbarawa.
Serikali kupitia LATRA imeendelea kutumia mifumo ya kidigiti katika kusimamia sekta ya usafiri ardhini ili kuongeza ubora wa huduma na usalama kwa wananchi.

