Mhe. Prof. Makame Mnyaa Mbarawa (Mb), Waziri wa Uchukuzi ameiagiza Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) kuongeza kasi ya uthibitishaji madereva na usajili wa wahudumu wa mabasi ya mijini nchini ili kuboresha huduma za kijamii, hususan huduma za wanafunzi katika vyombo vya usafiri wa umma ili kuwawezesha kupata elimu katika mazingira rafiki na yenye staha.
Agizo hilo amelitoa Februari 4, 2026 jijini Dodoma alipozungumza na vyombo vya habari baada ya malalamiko yaliyotolewa na mwanafunzi wa kidato cha kwanza, Mariana Eric Mirindima, aliyebainisha changamoto wanazokutana nazo wanafunzi wanapotumia usafiri wa mabasi ya mijini (daladala), ikiwa ni pamoja na kuchelewa kufika shuleni, kunyimwa huduma na usalama mdogo kutokana na baadhi ya watoa huduma kushindwa kuwahudumia wanafunzi kwa wakati unaofaa.
“Ninaiagiza Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) Kuhakikisha zoezi la kuthibitisha madereva na kusajili wahudumu (makondakta) kwenye mabasi linafanywa kwa kasi katika miji yote chini, na kutoa adhabu kali kwa mujibu wa Sheria kwa madereva na makondakta watakaobainika kuwanyanyasa wanafunzi na kuimarisha udhibiti wa nauli maalumu za wanafunzi, staha ya huduma na usalama wao kwa wakati wote,” amesema Prof. Mbarawa.
Vilevile amesema, katika kukabiliana na changamoto za usafiri kwa wanafunzi mijini, Serikali imeweka mipango na mikakati mbalimbali ikiwa ni pamoja na kutekeleza Sheria na Kanuni za kuthibitisha madereva na kusajili wahudumu wa vyombo vya usafiri wa mabasi na treni, kuanzisha huduma za mabasi maalumu yaendayo haraka kwa ajili ya wanafunzi, kurasimisha na kusimamia utozaji wa nauli maalumu ya shilingi 200 kwa wanafunzi katika mabasi yaendayo haraka na daladala na kutenga mabehewa maalum kwa ajili ya wanafunzi kwenye treni za mijini jijini Dar es Salaam.
Pia, Prof. Mbarawa amesema LATRA kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi wafanye ukaguzi wa mara kwa mara na wa kushtukiza kwenye vituo vya daladala hasa nyakati za asubuhi na jioni kuhakikisha wanafunzi wanapata usafiri.
Ameongeza kuwa, Serikali inaendelea kusisitiza ushirikiano wa wadau wote ili kujenga mfumo wa usafiri wa umma unaolinda haki, usalama na ustawi wa wanafunzi na watu wote nchini na amewasihi Watanzania, na abiria kwa jumla, kushirikiana kuwatetea wanafunzi wanaponyanyaswa na mtu yeyote.
Mamlaka inaendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi na wadau wote wa usafiri nchini kujenga mfumo wa usafiri wa umma unaolinda haki, usalama na ustawi wa wanafunzi na watu wote nchini. Pia, mwananchi anaweza kutuma ushahidi wa picha au sauti wa vitendo vinavyokiuka Sheria, Kanuni na Taratibu za usafiri ardhini kwa namba ya LATRA WhatsApp 0681 300 800

