Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia Wizara ya Uchukuzi na Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) imeendelea kuboresha huduma za usafiri nchini ambapo kwa usafiri wa mijini kupitia mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (BRT) kwa Kampuni ya Mabasi Yaendayo Haraka (UDART) inahakikisha wanafunzi wanatumia mabasi maalum yanayowawezesha kufika shuleni kwa wakati.
Hayo yamebainishwa na Bw. Gabriel Katanga, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Masoko na Uhusiano kwa Umma UDART Machi 18, 2026 ambapo amesema Kampuni hiyo inatoa huduma maalum ya kubeba wanafunzi jijini Dar es Salaam kupitia awamu ya kwanza ya mradi wa BRT unaojumuisha barabara za Morogoro kutoka Kimara hadi Kivukoni, Kimara Gerezani na Kimara Morocco.
Vilevile amesema kuwa, huduma hiyo maalum imeanzishwa kwa dhumuni la kutatua changamoto ambazo wanafunzi wamekuwa wakikabiliana nazo katika usafiri wa mabasi ya mijini (daladala) kila siku nyakati za asubuhi wakienda shule na nyakati za jioni wakirejea nyumbani.
Bw. Katanga amesema huduma hiyo maalum ina jumla ya mabasi manne, mabasi mawili hutolewa kila siku asubuhi saa 12 kutoka Kimara hadi Kivukoni na Kivukoni hadi Kimara, na mengine mawili hutolewa nyakati za jioni kuanzia saa 11 ili kuhakikisha wanafunzi wanapata usafiri salama, wa uhakika na kufika shuleni kwa wakati.
“Kwetu sisi usalama wa wanafunzi ndio kipaumbele chetu kikuu. Tunahakikisha wasimamizi wapo katika mabasi hayo na vituoni kuwasimamia wanafunzi hao wakiwa ndani ya mabasi na wanapofika kwenye vituo vya mwisho,” amesema Bw. Katanga.
Kwa upande wake Bw. Jumanne Omary, Msimamizi wa Kituo cha Kimara UDART amesema kuwa, wameweka utaratibu maalum ambapo mabasi yanapangwa kwenye ratiba maalum ili kuondoa fujo kwa wanafunzi wanapopanda mabasi hayo na hupanda kwenye mabasi kwa utaratibu mzuri huku wakiwasili shuleni kwa wakati na wanapotoka shuleni kuna magari maalum yanayowasafirisha kwa usalama kule wanapoelekea.
Naye Mwanafunzi Jacqueline Peter ameipongeza Serikali kwa jitihada za kuboresha huduma ya usafiri kwa wanafunzi kupitia huduma ya BRT inayowawezesha wao kufika shuleni na kurudi nyumbani bila kuchelewa. “Kunautofauti kati ya daladala na mabasi ya BRT kwakuwa yamerahisisha maisha yetu na kulinda wanafunzi dhidi ya usafiri wa kiholela, tunaipongeza Serikali kwa uwepo wa miundombinu bora na kuelekeza nauli ya shilingi 200 kwa wanafunzi iliyowezesha huduma hii kuwa nafuu.”
Kwa upande wake Bw. Godfrey Philimon mzazi wa mwanafunzi anayetumia huduma ya usafiri huo amefurahia uwepo wa huduma hiyo ambayo imewarahisishia wazazi kuwalipia nauli ya mabasi hayo na imewapa uhakika watoto wao kufika shuleni salama na kwa wakati.
“Hali ya sasa ni tofauti, hapo awali wanafunzi walikuwa wanajazana sana kituoni hali inayosababisha kuchelewa shuleni lakini sasa ikifika saa 12 hadi saa moja asubuhi hukuti mwanafunzi yeyote kituoni kutokana na uhakika wa huduma ya usafiri huu na pia imetupa furaha sana sisi wazazi, tunamshukuru sana Rais wetu kwa jitihada alizozifanya, pia nauli iliyoelekezwa na LATRA imetupa unafuu sisi wazazi hasa wenye hali ya chini kumudu gharama hizo,” amesema Bw. Philimon.
Huduma hii ya BRT kwa wanafunzi ni mfano wa jitihada zinazotekelezwa na LATRA kwa kushirikiana na wadau kuhakikisha huduma za usafiri kwa wanafunzi jijini Dar es Salaam ni salama, wa uhakika na wenye gharama nafuu.

