Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

WANAFUNZI NA WAFANYABIASHARA WANUFAIKA NA HUDUMA ZA MOFAT
Imewekwa: 26 Mar, 2026
WANAFUNZI NA WAFANYABIASHARA WANUFAIKA NA HUDUMA ZA MOFAT

Wanafunzi na wafanyabiashara wa samaki jijini Dar es Salaam wameendelea kunufaika na huduma maalum za usafiri zinazotolewa na kampuni ya MOFAT katika mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (BRT) awamu ya pili ambapo huduma hiyo imewezesha wanafunzi kufika shuleni kwa wakati na kuongeza ufanisi kwa wafanyabiashara.

Bw. Ramadhan Ally, Afisa Masoko wa MOFAT amesema hayo Machi 10, 2026 na kubainisha kuwa, huduma hiyo imeanzishwa mahususi ili kukabiliana na changamoto za usafiri kwa wanafunzi na wafanyabiashara wa samaki wanaosafiri kati ya Kivukoni na Mbagala, kwa kuhakikisha wanapata huduma za usafiri zilizo salama, za uhakika na kwa wakati.

“Tuliona ni muhimu kuja na huduma maalum kwa wanafunzi ambapo wanapanda mabasi yao wenyewe bila kuchanganyika na watu wazima. Tunajivunia kufanikisha jambo hili na tunapata mrejesho mzuri kutoka kwa wazazi ambao wanakiri kuwa wameridhika na huduma hii kwa kuwa watoto wao wanafika shuleni kwa wakati bila usumbufu,” ameeleza Bw. Ally.

Ameongeza kuwa, kwa sasa mabasi manne maalum yanawachukua wanafunzi kituoni kuanzia saa 11 alfajiri na kuwarudisha kuanzia saa 10 alasiri. Pia amesema, huduma hiyo imeanza takribani miezi sita iliyopita na inaendelea kuboreshwa kwa kuzingatia maoni ya wadau.

Wakati huo huo, Bw. Ally amesema MOFAT imepanua huduma zake kwa kuwafikia wafanyabiashara wadogo, hususan wa samaki, wanaosafiri kati ya Kivukoni, Mbagala na Ilala, ambapo huduma hiyo hutolewa kwa njia tano kila siku kuanzia asubuhi hadi jioni, na kurahisisha usafirishaji wa bidhaa zao kwa wakati.

Baadhi ya wanafunzi wanaotumia huduma hiyo wamesema awali walikuwa wakipoteza muda mwingi kusubiri mabasi, lakini tangu kuanzishwa kwa huduma hiyo maalum, sasa wanafika shuleni kwa wakati na kurudi nyumbani mapema. Aidha, wamepongeza huduma inayotolewa ikiwemo kulipa nauli inayotakiwa yaani TZS. 200 na kurejeshewa chenji sahihi pindi wanapotoa fedha kubwa.

Kwa upande wake, Bw. Makongoro Timothy, dereva wa MOFAT amesema madereva wanazingatia taratibu zote za usalama barabarani na kutekeleza majukumu yao kwa umakini ili kuhakikisha abiria wanapata huduma bora.

Naye Bi. Salma Omary, mfanyabiashara wa samaki, amesema huduma hiyo imewarahisishia usafiri kwenda Kivukoni kununua samaki na kurejea kwa wakati hivyo kupunguza hasara iliyokuwa ikitokana na kuharibika kwa bidhaa kutokana na ucheleweshaji wa usafiri.

Serikali kupitia Wizara ya Uchukuzi na LATRA inaendelea na jitihada za kuboresha usafiri ardhini nchini ili kuongeza ufanisi na kuhakikisha huduma bora zinatolewa kwa kuzingatia Sheria zilizopo.

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo