Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

TANZANIA KUADHIMISHA WIKI YA USAFIRI ENDELEVU ARDHINI
Imewekwa: 27 Oct, 2025
TANZANIA KUADHIMISHA WIKI YA USAFIRI ENDELEVU ARDHINI

Kwa mara ya kwanza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Uchukuzi kwa kushirikiana na Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) inaadhimisha Wiki ya Usafiri Endelevu Ardhini itakayofanyika Dar es Salaam Novemba 24 hadi 29, 2025 kwa kaulimbiu ya ‘Nishati Safi na Ubunifu katika Usafirishaji’.

Hayo mebainishwa na Prof. Godius Kahyarara, Katibu Mkuu Wizara ya Uchukuzi hivi karibuni ambapo amesema maadhimisho hayo yataambatana na maonesho yatakayofanyika viwanja vya Mnazi Mmoja pamoja na makongamano yatakayofanyika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) na kuhusisha wadau wa usafirishaji kutoka ndani na nje ya nchi.

 “Nawakaribisha wadau wa sekta ya Uchukuzi katika tukio la kwanza la aina yake na kwa upande wa Tanzania maadhimisho haya ni muhimu kwani yanatoa fursa kwa wadau kushuhudia mageuzi makubwa yaliyotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi mahiri wa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika sekta ya uchukuzi, hususan kwenye uwekezaji wa miundombinu ya kisasa kama reli, bandari na barabara,” amesema Prof. Kahyarara.

Vilevile amesema kuwa, ajenda ya Nishati Safi ni kipaumbele kikubwa cha Serikali ambapo Tanzania imepiga hatua kubwa kupitia miradi ya Reli ya Kisasa (SGR) inayotumia umeme, na uwekezaji mkubwa unaofanyika katika bandari.

“Tanzania ina Reli ndefu zaidi kuliko nchi zote Afrika ambayo inatumia Nishati safi ya umeme kupitia mradi wa SGR unaogharimu zaidi ya shilingi trilioni 40 na utakapokamilika utakuwa na urefu wa kilomita 10,707, ukianzia Dar es Salaam hadi Mwanza, Kigoma, Burundi, DRC, Kigali na Uganda. Sekta ya usafirishaji inachangia takribani asilimia 40 ya mapato ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na asilimia 98 ya biashara za ndani na nje, hivyo ni injini muhimu ya uchumi wetu,” ameeleza Prof. Kahyarara.

Naye CPA Habibu Suluo, Mkurugenzi Mkuu LATRA ameeleza kuwa, uaandaaji wa maonesho yanahusisha utekelezaji wa azimio la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UN) na kwa kutambua juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita katika kufanikisha Mkakati wa Taifa wa matumizi ya Nishati safi.

“Mkumbuke kwamba Rais aliibeba ajenda ya nishati safi na kwa kutimiza hilo kaulimbiu ya mwaka huu inasisitiza jukumu muhimu la mifumo ya usafiri shirikishi, yenye ustahimilivu na rafiki kwa mazingira katika kufanikisha maendeleo endelevu ya nchi, na katika wiki hiyo kutakuwa na maonesho ya sekta ya usafiri, mijadala, semina na mafunzo mbalimbali yatakayohusisha wadau kutoka ndani na nje ya nchi,” ameeleza CPA Suluo.

Kwa upande wake Bw. Plasduce Mbossa, Mkurugenzi Mkuu Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) amesema kuwa, sekta ya bandari inategemea sana ushirikiano na miundombinu ya barabara na reli ili kuongeza ufanisi wa shughuli za usafirishaji nchini.

“Shughuli zetu za bandari zinahitaji kuwa na viunganiko na sehemu ambazo tutawafikia wateja kwa kutumia usafiri wa reli na barabara, mategemeo ni kwamba ujenzi unaoendelea wa reli ukikamilika utaongezea ufanisi zaidi wa bandari zetu kusafirisha mizigo kwa wingi, kwa sasa tunahudumia zaidi ya tani milioni 32 kwa mwaka, mafanikio haya ni matokeo ya uwepo wa njia bora za kuunganisha bandari na masoko ya ndani na nje,” amesema Bw. Mbossa.

Mhandisi Machibya Masanja, ni Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), ambaye ameeleza kuwa, TRC imejizatiti kuhakikisha miundombinu ya reli inarahisisha utoaji wa huduma bora za usafirishaji wa mizigo na abiria.

“Tunashukuru Serikali kwa uwekezaji mkubwa katika mradi wa treni za kisasa (SGR) unaoendelea kwa urefu wa kilomita 2,102 katika awamu ya kwanza. Mradi huu utapunguza gharama za usafirishaji na kuongeza ufanisi. Kaulimbiu ya ‘Nishati Safi na Ubunifu katika Usafirishaji’ inajidhihirisha kwa vitendo kupitia huduma zetu zinazotumia Nishati mbadala ya umeme badala ya mafuta,” amesema Mha. Masanja.

Kimataifa siku ya Usafiri Endelevu Duniani huadhimishwa tarehe 26 Novemba kila mwaka kwa lengo la kutathmini maendeleo ya sekta ya usafiri duniani na kuhimiza matumizi ya teknolojia rafiki kwa mazingira. Maadhimisho haya yanatoa fursa kwa wadau mbalimbali wa usafirishaji hapa nchini kushiriki kwa kuwa na mijadala, kubadilishana uzoefu na kujifunza namna bora ya kutoa huduma bora.

 

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo