Bw. Agustus Fungo, Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano LATRA amewataka wasafirishaji nchini kuzingatia Sheria ya Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini sura ya 413 na masharti ya leseni za usafirishaji wanazopewa na Mamlaka ili kuhakikisha huduma za usafiri zinatolewa kwa usawa na kuzingatia haki za abiria wakiwemo wanafunzi.
Bw. Fungo amesema hayo Mei 21, 2026 kufuatia tukio lililosambaa mtandaoni likimuonesha kondakta wa gari lenye namba za usajili T665EDU linalofanya safari kuanzia Mbezi hadi Mnazi Mmoja kupitia barabara ya Morogoro akimzuia mwanafunzi kupanda gari hilo, jambo ambalo lipo kinyume na masharti ya leseni za usafirishaji abiria.
Bw. Fungo amesema kitendo cha kuwazuia wanafunzi kupanda mabasi ya mjini (daladala) hakikubaliki na kimekuwa kikilalamikiwa mara kwa mara na wazazi na wanafunzi hadi kufikia hatua ya kumuandikia Waziri wa Uchukuzi barua ili hatua zichukuliwe dhidi ya vitendo hivyo.
“Tunawashukuru wananchi walioweza kurekodi tukio hili na kulisambaza mtandaoni kwani limetusaidia kuliona na kuchukua hatua stahiki, ni jukumu la kila mmoja wetu kulinda usalama na haki katika vyombo vya usafiri, LATRA itaendelea kuchukua hatua madhubuti kwa wasafirishaji watakaokiuka Sheria na masharti ya leseni zao ili vitendo kama hivyo visitokee tena”, amesema Bw. Fungo.
Ameongeza kuwa, Mamlaka humpa msafirishaji leseni kwa masharti maalum hivyo anapaswa kuzingatia Sheria na masharti hayo wakati wote wa utoaji huduma ikiwemo kutombagua mwanafunzi kwa kuwa ana haki ya kusafiri kama abiria wengine kwa sababu naye hulipa nauli stahiki.
Kwa upande wake Bw. Laurent Macharo, dereva wa daladala amesema kuwa, baada ya Mamlaka kubaini tukio hilo waliitwa na kupewa elimu ambayo imewasaidia kuelewa wajibu wao pamoja na Sheria zinazopaswa kuzingatiwa wanapotoa huduma ya usafiri wa umma.
"Nimepata elimu kubwa kutoka LATRA ambayo itanisaidia hata kuwafundisha wenzangu nini tunapaswa kutekeleza tunapotoa huduma hasa kwa wanafunzi, kitendo cha kuwazuia wanafunzi kupanda magari sio kitendo kizuri kwani hata sisi madereva tuna watoto wetu ambao ni wanafunzi wanaotegemea usafiri wa umma," amesema Bw. Macharo.
Aidha, amesema hataruhusu tena tukio la aina hiyo kutokea kwenye gari lake na kusisitiza kuwa makondakta wanapaswa kuwajali wanafunzi wanaotumia usafiri wa umma kila siku.
Naye Bw. Jafari Issa, kondakta wa daladala, amekiri kutenda kosa hilo na ameeleza kuwa, amepatiwa elimu iliyomsaidia kutambua wajibu wake anapotekeleza majukumu yake ya ukondakta. Pia amewashauri makondakta wengine kutowazuia wanafunzi kupanda magari wanapohitaji usafiri.
LATRA imejiwekea utaratibu wa kupokea maoni, malalamiko na changamoto za usafiri kutoka kwa wananchi wanaotumia usafiri wa umma na huduma za usafiri ardhini nchini na kuzishughulikia kwa wakati. Yeyote atakayebaini tukio la uvunjifu wa Sheria awasiliane na Mamlaka kupitia namba 0800110019 au 0800110020 bila malipo, pia rekodi ushahidi wa matukio ya vitendo vinavyoaishiria rushwa kupitia simu janja na kutuma kwa WhatsApp namba 0681 300 800 au kufika katika ofisi za LATRA zilizopo katika mikoa yote Tanzania Bara.

