CPA, Dkt. Habibu Suluo, Mkurugenzi Mkuu Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) amewaonya baadhi ya wasafirishaji nchini wanaopandisha nauli bila kufuata Sheria, Kanuni na Taratibu zilizowekwa, huku akisisitiza kuwa mamlaka ya kupanga na kurekebisha nauli ipo chini ya Serikali kupitia LATRA kwa mujibu wa Sheria.
CPA, Dkt. Habibu Suluo ametoa onyo hilo wakati wa semina ya mafunzo kwa waandishi wa habari mabalozi wa LATRA iliyofanyika Aprili 1 na 2, 2026, Ukumbi wa Mikutano wa Shule ya Uongozi ya Mwalimu Julius Nyerere, Kibaha mkoani Pwani.
Vilevile amesema, LATRA imepokea malalamiko kutoka kwa wananchi kuhusu baadhi ya watoa huduma kuanza kupandisha nauli kiholela kufuatia kupanda kwa bei ya mafuta ya petrol, hatua inayowaongezea wananchi mzigo wa gharama za maisha.
Amefafanua kuwa, nauli zote hupangwa kwa kuzingatia maoni ya wadau kisha kupitishwa na Bodi ya LATRA na baadaye kutangazwa rasmi kupitia Gazeti la Serikali, na huanza kutumika baada ya siku 14 tangu kutangazwa. Hivyo, mtoa huduma haruhusiwi kubadilisha nauli bila kufuata utaratibu huo wa kisheria.
“Kutokana na hali ya sasa ya bei ya mafuta, tumepanga kufanya mkutano wa wadau tarehe 8 Aprili, 2026 jijini Dar es Salaam ili kusikiliza maoni ya wadau kabla ya kufanya uamuzi kuhusu marekebisho ya nauli, pia kuhakikisha uamuzi utakaofikiwa unazingatia maslahi ya watumiaji wa huduma za usafiri pamoja na uendelevu wa biashara za watoa huduma nchini. Mkutano utakuwa mubashara ili kuruhusu wadau kutoka maeneo mbalimbali kushiriki kupitia mitandao ya kijamii na LATRA Online TV,” ameeleza CPA, Dkt. Suluo.
Aidha, CPA, Dkt. Suluo amefafanua kuwa LATRA ina mamlaka ya kufanya tathmini kwa kutumia taarifa zake za ndani hata kama hakuna maombi rasmi yaliyowasilishwa, kwa kuzingatia Kanuni zilizopo. Iwapo tathmini itabaini kuwa kiwango cha mrejesho wa uwekezaji kimeshuka chini ya asilimia 10, ndipo hoja ya marekebisho ya nauli inaweza kupewa uzito.
Ameongeza kuwa, mtoa huduma anayehitaji kurekebishiwa nauli anatakiwa kuwasilisha maombi rasmi yakionesha kuwa katika kipindi cha miaka mitatu kiwango cha mrejesho wa uwekezaji kimeshuka chini ya asilimia 10, sambamba na kuambatanisha nyaraka muhimu zikiwemo mapendekezo ya nauli mpya, sababu za marekebisho, faida kwa watumiaji, hesabu za gharama na mapato, pamoja na taarifa za fedha zilizokaguliwa na taarifa za utendaji wa kampuni.
LATRA imeahidi kuendelea kusimamia kikamilifu utekelezaji wa Sheria, Kanuni na Taratibu za usafirishaji ili kulinda maslahi ya watumiaji wa huduma za usafiri na kuhakikisha hawabebeshwi gharama zisizo za lazima, huku ikizingatia uendelevu wa sekta ya usafiri ardhini nchini.

