Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

UWAMWA RASMI WAKALA WA LATRA
Imewekwa: 25 Jun, 2025
UWAMWA RASMI WAKALA WA LATRA

Bw. Elikana Balandya, Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza amekabidhi Cheti cha Uwakala wa kutoa leseni za Mamlaka ya Udhibiti Usafiri ardhini (LATRA) kwa Ushirika wa Wasafirishaji Mkoa wa Mwanza (UWAMWA) Juni 24, 2025, ukumbi wa mikutano wa Mahatma Gandhi, Mwanza.

Akikabidhi Cheti hicho kwa niaba ya Mhe. Said Mohamed Mtanda Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Bw. Balandya amewapongeza wanachama wa UWAMWA kwa hatua hiyo kubwa waliyofikia na amewataka kujisimamia na kuhakikisha wasafirishaji hao wanakuwa na leseni za LATRA na pia amewasihi kutumia vizuri asilimia 20 ya gawio watakalolipata kutokana na leseni watakazozikata ili kuwaletea maendeleo.

Vilevile amewaeleza wasafirishaji hao kuwa, Serikali inahamasisha kuundwa kwa vyama vya ushirika vya watoa huduma za usafiri kama mkakati madhubuti wa kuwawezesha wadau kushirikiana, kupata mikopo kwa urahisi, kuongeza nguvu ya sauti yao katika maamuzi, kuwawezesha kutoa huduma kwa ufanisi na kuzingatia uweledi na kurahisisha uratibu wa shughuli zao.

Wakati huhuo Bw. Balandya amezindua rasmi magari maalumu ya UWAMWA yatakayokuwa yanawachukua wanafunzi wa shule za umma asubuhi na jioni ambapo wazazi watatakiwa kuweka nauli za wanafunzi hao kwenye kadi itakayotumika wakati wote wa kuwasafirisha wanafunzi hao.

Akizungumza kwa niaba ya CPA Habibu Suluo, Mkurugenzi Mkuu LATRA, DCP Johansen Kahatano, Mkurugenzi Udhibiti Usafiri wa Barabara amesema Cheti hicho kitaruhusu UWAMWA kutoa aina sita za leseni za vyombo vya moto vya kukodi ambazo  ni  leseni za Pikipiki za Magurudumu Mawili,   Leseni za Pikipiki za Magurudumu Matatu, Leseni za Taksi za kawaida, Leseni za Taksi Mtandao, Leseni za Magari Maalumu ya Kukodi pamoja na Leseni za Kuitisha Mtandaoni Usafiri wa Kuchangia

“Sisi kama Mamlaka tunataka kuondoka kwenye utaratibu wa kudhibiti mtu mmoja mmoja na kwenda kwenye mfumo wa udhibiti kupitia vyama vya ushirika au kampuni ambapo wasafirishaji watainuana kiuchumi lakini pia watakuwa wanasimamiana kuhakikisha wanatekeleza majukumu kwa mujibu wa Sheria na utaratibu uliopo huku wakizingatia masharti ya leseni za usafirishaji walizonazo,” ameeleza DCP Kahatano.

Naye Bw. Jabir John Magele Mwenyekiti wa UWAMWA amesema anaishukuru LATRA kwa kuwapatia cheti cha uwakala wa utoaji wa leseni za LATRA kwa vyombo vya moto vya kukodi kibiashara kwani cheti hicho kinaashiria urasmi wa UWAMWA kama wakala wa LATRA.

“Naishukuru LATRA kwa kutupatia cheti cha uwakala, cheti hiki kinaenda kuwa chachu ya utendaji kazi wetu ambao matunda yake ni kutuinua kiuchumi kupitia gawio la 20% tutakayorejeshewa na LATRA kutokana na  leseni tutakazozikata kwa wanachama wetu,” ameeleza Bw. Magele.

Akizungumzia mabasi ya kuchukua wanafunzi wa shule za umma, Bw. Mgele ameeleza kuwa, wao kama UWAMWA wameanza na magari 10 kwa sasa yatakayotoa huduma hiyo ikiwa ni sehemu ya mchango wao katika kutatua changamoto za usafiri kwa wanafunzi I mkoani Mwanza.

Makabidhiano ya cheti hicho yamefanyika wakati wa Mkutano wa Wadau wa Usafirishaji ulioandaliwa na LATRA na kuhudhuriwa UWAMWA, Mabalozi wa Usalama Barabarani (RSA), Muwakilishi wa Umoja wa Wasafirishaji Jiji la Arusha (UWADAJA) pamoja na wadau wengine wa usafirishaji Mkoa wa Mwanza ambapo walizungumza masuala mbalimbali kwa mustakabali mzuri wa  umoja wao na ustawi wa sekta ya usafiri ardhini mkoani hapo na nchini kwa jumla

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo