Mhe. Mihayo Juma Nhunga, Mwenyekiti wa Kamati ya Miundombinu, Ardhi na TEHAMA ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar, pamoja na wajumbe wa Kamati hiyo, wamepongeza ubunifu na ufanisi wa mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) inayotumiwa na Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA), wakieleza kuwa imeleta mageuzi makubwa katika udhibiti wa sekta ya usafiri ardhini na utoaji wa huduma kwa wadau.
Pongezi hizo zimetolewa kwenye kikao cha pamoja kilichowakutanisha wajumbe wa Kamati hiyo, watumishi wa Mamlaka ya Usafiri na Usalama Barabarani Zanzibar (ZARTSA) pamoja na baadhi ya wajumbe wa Menejimenti ya LATRA, kufuatia ziara ya Kamati hiyo Makao Makuu ya LATRA, Dodoma ili kujifunza, kubadilishana uzoefu wa kiutendaji na kuimarisha ushirikiano katika usimamizi na udhibiti wa sekta ya usafiri ardhini.
Akizungumza katika kikao hicho, Mhe. Nhunga amesema LATRA imeonesha mfano wa kuigwa kwa kubuni na kutengeneza mifumo kwa kutumia wataalamu wa ndani wa TEHAMA, hatua ambayo imewezesha mifumo hiyo kuendana na mazingira halisi na mahitaji ya sekta.
"Mmefanya jambo la kupongezwa kwa kuwaamini na kuwatumia wataalamu wa ndani kutengeneza mifumo inayokidhi mahitaji ya Mamlaka na sekta kwa jumla. Huu ni mfano mzuri unaopaswa kuigwa," amesema Mhe. Nhunga.
Vilevile amesema, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaendelea kuwekeza katika matumizi ya teknolojia ili kuimarisha usalama barabarani, ikiwemo kuanzisha mfumo wa kisasa wa kamera za barabarani utakaowezesha kubaini makosa mbalimbali ya usalama barabarani.
"Tunatarajia kuanza kutumia mfumo wa kamera za kisasa utakaobaini mwendokasi wa vyombo vya moto na maegesho yasiyo sahihi. Atakayefanya kosa atapokea ujumbe mfupi wa maandishi ndani ya dakika tano kulingana na usajili wa namba ya gari husika. Tunaamini teknolojia kama hizi zitasaidia kuongeza uzingatiaji wa Sheria za usalama barabarani na ikiwa LATRA itaona inafaa, inaweza pia kutumia uzoefu huu katika maeneo inayoyasimamia," ameeleza Mhe. Nhunga.
Akizungumza kwa niaba ya CPA Dkt. Habibu Suluo, Mkurugenzi Mkuu LATRA, Bw. Abdallah Mhagama, Mkurugenzi Udhibiti Uchumi, amesema mifumo ya TEHAMA inayotumiwa na LATRA imeongeza ufanisi wa utoaji wa huduma, imeongeza uwazi, imepunguza gharama za uendeshaji na kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa wadau wa sekta ya usafiri ardhini.
Amesema kwa sasa huduma za LATRA zinapatikana kwa njia ya mtandao, hivyo imewaondolea watoa huduma na watumiaji wa huduma kadhia ya kulazima kufika ofisi za Mamlaka ili kupata huduma mbalimbali.
"Kwa sasa huduma zetu zinapatikana kidigiti mathalan mteja anaweza kuomba leseni, kufanya malipo na kupata leseni yake popote alipo bila kufika ofisini. Hii imeongeza ufanisi wa huduma na kuokoa muda kwa wateja wetu," amesema Bw. Mhagama.
Amebainisha kuwa matumizi ya mifumo ya kidigiti yamechangia pia juhudi za utunzaji wa mazingira kwa kupunguza matumizi ya karatasi, "Leo hii msafirishaji hahitaji tena kuchapisha leseni yake. Anaweza kuihifadhi kwenye simu janja, huku ukaguzi wa uhalali wa leseni ukifanyika kwa njia ya mtandao kupitia LATRA App. Hii imepunguza matumizi ya karatasi na kuunga mkono ajenda ya maendeleo endelevu," amefafanua.
Ameongeza kuwa, LATRA imeendelea kutekeleza maelekezo ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kuhakikisha mifumo ya kidigiti inaunganishwa na mifumo ya taasisi nyingine za Serikali ili kurahisisha ubadilishanaji wa taarifa, kuongeza uwazi na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.
LATRA itaendelea kuwekeza katika ubunifu na matumizi ya teknolojia za kisasa ili kuboresha huduma zake, kuimarisha usimamizi wa sekta ya usafiri ardhini na kuhakikisha huduma zinapatikana kwa ufanisi, usalama na uhakika saa 24.

