Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

WAONGOZA WATALII NCHINI WATAKIWA KUWA NA LESENI HAI YA LATRA
Imewekwa: 24 Apr, 2023
WAONGOZA WATALII NCHINI WATAKIWA KUWA NA LESENI HAI YA LATRA

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) imetoa wito kwa waongoza watalii nchini kuwa na Leseni hai ya usafirishaji abiria ambayo ni maalumu kwa magari ya watalii, ili kuepusha usumbufu kwa madereva na watalii kwa jumla.

Wito huo umetolewa na Bw. Johansen Kahatano, Mkurugenzi Udhibiti Usafiri wa Barabara kutoka LATRA kwenye mkutano wa mafunzo kwa waongoza watalii nchini ulioandaliwa na LATRA kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha. Mkutano huo umefanyika katika ukumbi wa Mt. Carolus uliopo Jijini Arusha April 20, 2023.

Akizungumza baada ya mkutano huo Bw. Kahatano amesema, kwa kuwa tayari waongazaji watalii wamefahamu umuhimu wa kuwa na leseni ya LATRA, ni vyema wakajitokeza wote kukata leseni hiyo ili kuboresha Sekta ya Utalii nchini.

"Kimsingi Waongozaji Watalii wamefahamu uhusiano uliopo baina yetu hivyo nawasihi wawe na leseni hai za LATRA. Ni vizuri wakajituma wenyewe na kukata leseni hizo ili kuepusha usumbufu wawapo safarini au kwa watalii kwa jumla, kwa maana tumewaelekeza pia jinsi ya kuangalia kama leseni zao zipo hai kwa njia ya mtandao," amesema Bw. Kahatano.

Vilevile amewahimiza wamiliki wa vyombo vya usafiri kibiashara kutumia huduma za LATRA ambazo zinapatikana kwa njia ya mtandao na kuepuka kuwatumia watu wa kati "VISHOKA" ambao wanafanya huduma za LATRA zionekane ni za gharama zaidi kuliko uhalisia.

"Huduma za LATRA zinatolewa kwa njia ya mtandao, mtu anaweza kuomba leseni mpaka kupatiwa namba ya malipo akiwa nyumbani kwake au ofisini, hivyo akawa na safari moja tu ya kufika ofisini kwetu na kuchukua leseni yake. Badala ya kutumia watu wa kati "VISHOKA" wanaweza kujihudumia wenyewe mahali walipo na kupunguza gharama za maisha," ameongeza Bw. Kahatano.

Naye Katibu Tawala Mkoa wa Arusha Bw. Misaille Musa ameitaka LATRA kukaa pamoja na Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) pamoja na Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA)  ili kujadili na kupata ufumbuzi wa taka zinazozalishwa na mabasi pamoja na daladala katika Jiji la Arusha.

Akiyazungumzia mafunzo hayo waliyopatiwa Bi. Elizabeth Ayo, Mwenyekiti wa Chama cha Mawakala wa Utalii Wanawake Tanzania (TAWTO) amesema anaamini tasnia ya Utalii nchini inakwenda kubadilika kama mapendekezo yakifanyiwa kazi na kila mmoja akitimiza wajibu wake.

Mkutano huo ulioandaliwa na LATRA kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa umehudhuriwa na wadau mbalimbali wakiwemo Jeshi la Polisi, Shirika la Hifadhi ya Taifa Tanzania (TANAPA), Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na waongoza watalii ambao ndio waliopatiwa mafunzo.

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo