
Watoa huduma wa tiketi mtandao wametakiwa kuunganisha mifumo yao na Mfumo wa Tiketi Mtandao wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) na Mfumo wa TRA EFDMS wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ifikapo mwishoni mwa mwezi wa kumi mwaka 2024.
Hayo yamebainishwa na DCP Johansen Kahatano, Mkurugenzi Udhibiti Usafiri wa Barabara LATRA kwenye kikao cha pamoja kati ya LATRA, TRA, Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) Jeshi la Polisi, Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA), Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (TABOA) pamoja na watoa huduma wa tiketi mtandao nchini kilichofanyika Oktoba 11, 2024 Ofisi za LATRA Mkoa wa Dar es Salaam.
“Mpaka kufikia leo Oktoba 11, 2024, watoa huduma wa tiketi mtandao tisa (9) wameunganisha mifumo yao TRA na wanne (4) wameunganisha na mfumo wa LATRA na tumekubaliana kuwa ifikapo mwisho wa mwezi huu, wote wawe wameunganisha mifumo yao na mifumo ya Serikali,” amesema DCP Kahatano
Vilvile DCP Kahatano amesema kuwa, jambo la pili walilokubaliana ni mifumo ya watoa huduma hao iwe na uwezo wa kukusanya tozo za Serikali na za kwao wenyewe yaani watoa huduma waweze kupata malipo yao moja kwa moja badala ya kusubiri kwenda kudai kwa wasafirishaji.
Aidha, DCP Kahatano ameongeza kuwa, wamekubaliana kwa pamoja TRA itoe notisi ya kuwataka wasafirishaji kuwasilisha taarifa za magari yao ili tiketi ya basi ikitoka iwe na alama ya TRA itakayomtambua msafirishaji na kuonesha uhalali wa kulipa kodi.
Naye Bw. James Lumbwete, Katibu Mtendaji TABOA amesema kikao kilikuwa kizuri na chenye manufaa kwa sababu masuala ya msingi yanayohusu mfumo wa tiketi mtandao yamejadiliwa na wanaelewa kwamba ili sekta ikue inahitaji mifumo ambayo inarahisisha utoaji wa huduma.
“Sisi TABOA tumewasilisha mapendekezo yetu na tunaamini kupitia ushirikiano huu mzuri uliopo, kila kitu kitafanyiwa kazi na kitakuwa sawa, mfumo utatumika vizuri na hautokuwa na shaka lolote,” ameeleza Bw. Lumbwete.
Kwa upande wake Bw. Finehasi Lema, Mwenyekiti wa watoa huduma wa tiketi mtandao nchini amesema wapo tayari kukamilisha taratibu za kuunganisha mifumo yao LATRA na TRA na wanaendelea kuhimizana ili kufikia malengo yaliyowekwa.