Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

WATOA HUDUMA ZA TIKETI MTANDAO WASIOSAJILIWA MARUFUKU JULAI 01, 2025
Imewekwa: 14 Jun, 2025
WATOA HUDUMA ZA TIKETI MTANDAO WASIOSAJILIWA MARUFUKU JULAI 01, 2025

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) imesema ifikapo Julai 01, 2025 watoa huduma wa Tiketi Mtandao wasiounganisha mifumo yao na Mfumo wa Safari Tiketi wa LATRA na Mfumo wa TRA EFDMS wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) hawatoruhusiwa kuendelea kutoa huduma hiyo.

Hayo yamebainishwa na Bw. Salum Pazzy, Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano (LATRA) wakati wa ukaguzi wa kawaida wa utekelezaji wa masharti ya leseni za usafirishaji abiria uliofanyika Stendi ya Mabasi Msamvu iliyopo mjini Morogoro, Juni 14, 2025.

Bw. Pazzy amesema kuwa, hatua hiyo ni sehemu ya mkakati wa kuimarisha usimamizi wa sekta ya usafiri ardhini, kuongeza uwazi katika ukusanyaji wa mapato na kuhakikisha abiria wanapata huduma kwa mujibu wa Sheria na Taratibu zilizopo.

“Hadi sasa watoa huduma wachache kati ya 15 waliokamilisha usajili na kuunganisha mifumo yao na mifumo ya Serikali na Julai 01, 2025 tutatoa orodha ya watoa huduma walioidhinishwa na Serikali ili wafahamike na wasafirishaji na hao ndio watakuwa wanatambulika kutoa huduma hiyo,” ameeleza Bw. Pazzy.

Vilevile amesema, kwa mujibu wa Sheria, wasafirishaji wanaruhusiwa kumiliki mifumo yao wenyewe ya mauzo ya tiketi mtandao na pia wanaweza kuchagua watoa huduma wa tiketi mtandao waliodhinishwa na LATRA ambao kwa mujibu wa Kanuni za Tiketi Mtandao, wanapaswa kupewa cheti kutoa huduma hiyo.

Aidha, Bw. Pazzy amewataja watoa huduma hao 15 wa Tiketi Mtandao kuwa ni Logix Co Limited, Itule Company Limited, Busbora Company Limited, Duarani Innovate Limited, Web Corporation Tanzania Limited, Hashtech Tanzania Limited, Otapp Agency Company Limited, Sepa Tech Limited,Iyishe Company Ltd - Adventure Connection,Global Light & Company Limited, Mkombozi Infotech Company Limitedl, Meerkatz - Kidia One, Abood Bus Services, Borita Company Limited pamoja na  Exabytes Africa Ltd.

LATRA kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani. wanaendelea na ukaguzi wa mabasi ya abiria kote nchini unaohusisha ufuatiliaji wa uhalali wa leseni za usafirishaji, matumizi ya mikanda ya usalama, uwekaji wa alama kwenye mizigo ya abiria na uzingatiaji wa matumizi ya Tiketi Mtandao.

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo