Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

WAZIRI MBARAWA: i-BUTTON ISAIDIE KUDHIBITI AJALI
Imewekwa: 25 Oct, 2024
WAZIRI MBARAWA: i-BUTTON ISAIDIE KUDHIBITI AJALI

Mhe. Prof. Makame Mnyaa Mbarawa (Mb), Waziri wa Uchukuzi ameitaka Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) kuhakikisha matumizi ya kitufe cha utambuzi wa dereva (i-button) wanachopatiwa madereva waliothibitishwa na LATRA yanasaidia kudhibiti ajali nchini.

Mhe. Mbarawa amesema hayo Oktoba 23, 2024 alipotembelea banda la LATRA katika maonesho ambayo ni sehemu ya Mkutano wa 17 wa Mwaka wa Kutathmini Utendaji kazi wa Sekta ya Uchukuzi yanayofanyika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC).

“Ni muhimu muhakikishe dereva anakitumia kwa usahihi kitufe chake na inapaswa kitufe kiwe kinawatumia taarifa pindi dereva anapoendesha zaidi ya muda unaotakiwa ambao ni saa 08 kwa mujibu wa Sheria zilizopo ili mchukue hatua,”ameeleza Mhe. Mbarawa.

Kwa upande wake, CPA Habibu Suluo, Mkurugenzi Mkuu LATRA amesema LATRA inawathibitisha madereva wa vyombo vya moto kibiashara ili kuhakikisha kunakuwa na madereva wenye uweledi na wanaozifahamu Sheria, Kanuni na Taratibu za usafiri ardhini.

“Tukiwa na madereva wenye uweledi, nayo itasaidia kupunguza tatizo la ajali, kwa sasa tunawasajili na kuwathibitisha kimtandao kupitia mfumo wa kuwatahini madereva DTS, na wale wanaofaulu tunawapatia vyeti na kitufe cha i-button ambacho wanakitumia mwanzo wa safari mpaka mwisho wa safari yao, na sisi tunafuatilia kwa ukaribu matumizi sahihi ya kifaa hicho,” amefafanua CPA Suluo

Pia amemueleza Mhe. Mbarawa kuwa, changamoto kubwa inayosababisha ajali kwa sasa ni uchovu wa madereva na amesema LATRA inaamini kuwa ikipata msukumo wa Serikali wa kuwaagiza madereva wote lazima wathibitishwe na watumie vitufe vya utambuzi, itasaidia sana katika kudhibiti ajali zinazogharimu nguvu kazi ya Taifa na maisha ya Watanzania kwa jumla.

Vilevile amesema LATRA itaendelea kudhibiti usafiri ardhini ikiwa ni pamoja na kuongeza kasi ya matumizi ya mifumo TEHAMA ambayo inarahisisha ufuatiliaji wa sekta zinazodhibitiwa.

Aidha, CPA Suluo amesema miongoni mwa Mifumo ya TEHAMA inayotumiwa na LATRA ni Mfumo wa Taarifa kwa Abiria (PIS) ambao umetokana na Mfumo wa Kufuatilia Mwenendo wa Magari (VTS) na unamuwezeshe mwananchi kuwa na taarifa kwa ukaribu zaidi kuhusiana na mwenendo wa mabasi yanayowasili katika vituo mbalimbali nchini.

“PIS ni mfumo kwa njia ya tovuti (web based) unaopatikana kwa simu janja au kwa kompyuta kupitia anwani ya https://pis.latra.go.tz/ lakini pia upo katika runinga zilizofungwa kwenye stendi ya mabasi Magufuli Dar es Salaam na stendi ya mabasi nanenane jijini Dodoma,” alisema.

Vilevile amesema kuwa, marekebisho ya Sheria yaliyofanyika mwezi Machi Mwaka huu yameleta mabadiliko makubwa katika utoaji wa leseni za LATRA na sasa Mamlaka imeanza na Chama cha Ushirika cha Madereva na Wamiliki wa Bodaboda na Bajaji Mkoani Kilimanjaro (KIBABOT SACCOS) na tayari ni wakala wa LATRA na  anatoa leseni za Bajaji na Bodaboda kwa Mkoa wa Kilimanjaro, pia LATRA imefanya maboresho kwenye Mfumo wa Usimamizi wa Taarifa za  Barabara na Reli (RRIMS) ambao unamuwezesha mtoa huduma kupata leseni kiganjani mwake bila ulazima wa kufika ofisini.

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo