Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

Hotuba ya Mhe. Dkt. Charles Msonde wakati wa Mkutano wa Wadau Mei 26, 2022
26 May, 2022 Pakua
 • Ndugu Mkurugenzi Mkuu wa LATRA, Bwana Gilliard Ngewe
 • Dkt. Edwin Mhede, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART),
 • Ndugu Kaimu Katibu Mtendaji wa Baraza la Ushauri la Watumiaji Huduma za Usafiri Ardhini,
 • Ndugu Wakuu na wawakilishi wa taasisi mbalimbali za Serikali,
 • Viongozi wa Chama cha Kutetea Abiria,
 • Ndugu wadau mbalimbali mliojumuika hapa
 • Ndugu wanahabari,
 • Wageni waalikwa mabibi na mabwana

Ninawasalimu kwa jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania....

Kazi - iendelee!!

Awali ya yote, namshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa Rehema kwa kuendelea kutupa uhai na kuibariki Nchi Yetu yetu, chini ya uongozi mahiri wa Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Pia nashukuru kwa heshima niliyopewa ya kuwa mgeni Rasmi katika ufunguzi wa mkutano huu wa wadau unaolenga kupokea maoni kuhusu nauli za mabasi yaendayo haraka (BRT) - katika jiji la Dar es Salaam.

Ndugu wageni waalikwa,

Ni vyema kujielimisha kuwa, Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka ulianzishwa kupitia Notisi ya Serikali, Namba 120 ya tarehe 25 Mei 2007 na kuzinduliwa rasmi tarehe 16 Juni 2008 kwa lengo la kuwezesha utekelezaji wa majukumu  makuu matatu:

 1. Kusimamia utekelezaji na uendeshaji wa Mfumo wa Mabasi Yaendayo Haraka katika Jiji la Dar es Salaam;
 2. Kuweka mpangilio makini wa matumizi ya barabara kuu (trunker roads) na ndogo (feeder roads) kwa watumiaji wote ili kupunguza msongamano ; na
 3. Kuhakikisha kuwepo kwa Menejimenti ya Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka yenye kuleta tija na ufanisi.

Ndugu wageni waalikwa,

Kumekuwa na juhudi za muda mrefu kwa upande wa serikali ya Tanzania kusanifu na kujenga miundombinu muhimu ya usafirishaji na uboreshaji wa huduma ya usafiri kwa ujumla ili kuwezesha biashara ya ndani na ya kimataifa.

Sote tunatambua kuwa usafiri wa umma ni mhimili wa maendeleo ya jumla nchini na Duniani kote. Ni dhahiri kuwa ni sekta muhimu ya maendeleo ambayo ni chachu ya ukuaji kijamii na kiuchumi na ni miongoni mwa sekta zinazo chukua sehemu kubwa ya uwekezaji wa Serikalini nchini.

Sekta ya usafiri wa umma mjini imesaidia kutengamanisha ushindani, kukuza biashara, utalii na uwekezaji wa kigeni, na inachangia mapato ya serikali.

Ndugu wageni waalikwa,

Ninatambua kuwa Serikali kupitia Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART) inayo mikakati ya kuboresha huduma kwa watumiaji wa makundi mbali mbali, ikiwa ni pamoja na Wanafunzi, Watu wenye mahitaji maalumu pamoja na akina mama. Hivyo, kuhakikisha usafiri wa Mabasi Yaendayo Haraka unakuwa rafiki kwa watumiaji wote.

Aidha, nimefahamishwa kuwa Wakala una nia ya kukuza viwango vya ushindani na kuvutia soko, ambapo unakwenda kuboresha huduma kwa kuanzisha mabasi yenye viyoyozi, yenye mfumo wa Euro IV, ikiwa ni pamoja na kuleta mfumo wa kisasa wa ukusanyaji nauli sambamba na mfumo wa taarifa kwa abiria pamoja na huduma ya internet bila malipo vituoni.

Ndugu wageni waalikwa,

Kama alivyo eleza Mkurugenzi Mkuu wa LATRA kuwa jukumu la mdhibiti kushirikisha wadau kabla ya kufikia maamuzi ni kwa mujibu wa Sheria, hii inatupa faraja kuona utekelezaji wa sheria za nchi unafanyika kikamilifu.

Nafahamu kuwa moja kati ya misingi ya utawala bora ni ushirikishwaji, nasi kama wadau kwa upande wa Serikali tunafurahi kushuhudia wadau wakishiriki kikamilifu na kwa idadi kubwa kiasi hiki kutoa maoni yao kabla ya maamuzi kufanyika.

Aidha, nakubaliana na kauli ya Mkurugenzi Mkuu wa LATRA kuwa huduma ya usafiri ni huduma ya lazima katika jamii. Hivyo napenda kutoa wito kwetu wadau tuwe mabalozi wa dhati katika kujadili na kutoa maoni kwa hoja jengefu bila kuwa na jazba.

Pia, nimefurahi kusikia kuwa wadau ambao hawakuweza kufika hapa wanaweza kuendelea kuwasilisha maoni yao kwa maandishi hadi tarehe 7 mwezi Juni mwaka huu.

Natoa rai kwa wadau mbalimbali kuitumia vizuri fursa hii, ili kuwawezesha wataalamu wetu kufanya kazi yao kwa ufanisi na kutuletea matokeo mazuri.

Ndugu wageni waalikwa,

Napenda kutumia fursa hii kuwakumbusha watanzania mnaonisikia hapa na kupitia vyombo vya habari kuwa tushiriki kikamilifu katika kuwezesha kazi inayoendelea ya kuweka anwani za makazi na kujiandaa kuhesabiwa wakati wa Sensa ya watu na makazi inayotarajiwa kufanyika tarehe 23 mwezi Agosti Mwaka huu. Tumeshuhudia elimu ikitolewa kwa njia mbalimbali, nasi wananchi tunalo jukumu la kuipokea elimu hiyo na kuifanyia kazi kwa maslahi mapana ya taifa letu.

Ndugu wageni waalikwa,

Kwa kuwa mkutano huu ni wa kwenu kujadili na kutoa maoni, mimi kazi yangu ni kufungua mkutano huu. Hivyo, sitokuwa na mengi zaidi ya kusema.

Kwa hayo machache, napenda kutamka rasmi kuwa mkutano wa wadau kutoa maoni ya nauli za mabasi umefunguliwa rasmi.

Asanteni kwa kunisikiliza

 

Prof. Riziki Silas Shemdoe,

Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais -Tamisemi,

26 Mei, 2022

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo