Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

HOTUBA YA MKURUGENZI MKUU KATIKA UZINDUZI WA MAFUNZO YA WAHUDUMU/ MAKONDAKTA WA VYOMBO VYA USAFIRI ARDHINI
22 Nov, 2023 Pakua

Ndugu Wawakilishi wa Taasisi za Mafunzo (CBE & NIT),

Wenyeviti na Viongozi wa Vyama vya Wasafirishaji Mliopo;

Menejimenti na Wafanyakazi wa LATRA Mliopo,

Wadau wa Huduma za Usafiri Kibiashara Mliopo;

Ndugu Wanahabari,

Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana..

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA…..

 

Awali ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema, kwa kutujaalia afya njema na fursa ya kujumuika hapa leo kwa lengo la kuandika historia mpya katika Nchi yetu ya kuzindua mafunzo ya wahudumu wa vyombo vya usafiri ardhini. Inapendeza sana kuwaona wadau wetu mmefika hapa, hususan wadau wetu ambao ni wahudumu wa vyombo vya usafiri ardhini, hii ni bishara njema.

 

 Pili, kwa niaba ya Bodi ya Wakurugenzi, Menejimenti na Wafanyakazi wote wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA), natoa shukrani za dhati kwa viongozi wetu, Mhe. Prof. Makame Mbarawa (Mb), Waziri wa Uchukuzi, Mhe. David Kihenzile (Mb), Naibu Waziri wa Uchukuzi, Prof. Godius W. Kahyarara, Katibu Mkuu, Wizara ya Uchukuzi na Dkt. Ally Possi, Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Uchukuzi kwa kazi kubwa wayoifanya katika Wizara yetu hususan katika kusimamia utekelezaji wa miradi ya kimkakati kwa maendeleo ya Taifa letu na kwa namna wanavyotuongoza vyema katika kutekeleza majukumu yetu kwa mujibu wa Sheria, Taratibu na Kanuni zilizopo. Viongozi wetu hawa wanafanikiwa kwa kuwa nao wanaongozwa vyema kabisa na Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wakizingatia falsafa ya 4R (Reconciliation, Resilience, Reform and Rebuild).

 

Tatu, na kwa thamani ya kipekee zaidi, niwashukuru sana Wakuu wa Vyuo (Chuo cha Elimu ya Biashara – CBE na Chuo cha Taifa cha Usafirishaji – NIT) pamoja na wahadhiri wao kwa kukubali ombi letu la kuandaa Mtaala wa kutoa mafunzo ya  Wahudumu wa Usafiri Ardhini kwa ubora na kuboresha huduma za usafiri ardhini. Mtaala huo ulizinduliwa na Naibu Waziri wa Uchukuzi tarehe 1 Julai, 2023 na leo tunaandika historia nyingine ya kuanza kwa mafunzo mafupi katika viwango vyenye ubora katika Nchi yetu. Asanteni sana CBE, asanteni sana NIT.

 

Nne, nawashukuru sana wadau wetu wote mliohudhuria hapa na wanaotufuatilia kwenye kwenye vyombo vya habari na mitandao ya kijamii kwa kukubali mwaliko wetu na kujumuika nasi siku hii muhimu na kushuhudia shughuli hii muhimu ya uzinduzi wa mafunzo kwa wahudumu wa vyombo vya usafiri ardhini.  Nafahamu kuwa mnayo majukumu mengi na makubwa yenye maslahi makubwa kwa Taifa, hata hivyo mmeweza kutenga muda wenu na kufika hapa ili kushuhudia jambo hili ambalo pia ni la maslahi makubwa kwa Watanzania na Taifa letu kwa jumla katika kuboresha huduma za usafiri ardhini.  Asanteni sana.

 

Wageni Waalikwa, Wanahabari, Mabibi na Mabwana,

Naomba niwakumbushe kuwa LATRA inatekeleza majukumu yake kwa mujibu wa Sheria ya Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini, Sura ya 413. Kifungu cha (5)(1) cha Sheria hiyo inaeleza majukumu yetu kuwa ni:

  1. Kutekeleza majukumu ya sheria za kisekta;
  2. Kutoa, kuhuisha, au kufuta leseni;
  3. Kwa mujibu wa sheria za kisekta:
    1. Kusimamia viwango  vya ubora wa huduma  na usalama katika sekta zinazodhibitiwa;
    2. Kusimamia viwango na masharti ya utoaji huduma zinazodhibitiwa;
    3. Kudhibiti viwango vya tozo za huduma
  4. Kuratibu shughuli za usalama wa usafiri wa ardhini;
  5. Kusajili wahudumu na kuthibitisha madereva wa sekta zinazodhibitiwa;
  6. Kuhakikisha kuwa treni na magari ya abiria yana ubora unaotakiwa;
  7. Kufuatilia mwenendo wa utendaji kazi wa sekta zinazodhibitiwa kwa kuangalia kiwango cha uwekezaji, gharama za kutoa huduma, ufanisi na ueneaji wa huduma;
  8. Kuwezesha utatuzi wa migogoro na malalamiko; na
  9. Kuelimisha umma kuhusu kazi na wajibu wa Mamlaka.
  10. Kushauriana na taasisi nyingine za kiudhibiti zinazotekeleza majukumu yanayofanana na yetu Tanzania Bara au kwingineko
  11. Kutekeleza majukumu mengine kwa mujibu wa Sheria hii au Sheria nyingine, kama itakavyoelekezwa.

 

Wageni Waalikwa, Wanahabari, Mabibi na Mabwana,

Leo tumejumuika kutekeleza jukumu lililo katika kifungu cha 5(1)(e) cha Sheria ya Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini Sura ya 413, ambapo Mamlaka ina jukumu la Kusajili Wahudumu na Kuthibitisha Madereva wa vyombo vya moto vinavyotoa huduma za usafiri kibiashara. Jukumu hili tulilopewa LATRA kwa mujibu wa sheria, linalenga kuhakikisha kuwa Watanzania wanapata huduma bora za usafiri ardhini zinazotolewa na wahudumu weledi waliopata mafunzo sahihi yenye kujumuisha kujua Sheria ya LATRA na Kanuni zake, Sheria ya Usalama Barabarani na Kanuni zake, huduma bora kwa mteja (abiria), jinsi ya kutoa huduma ya kwanza iwapo abiria atapatwa na changamoto zinazohitaji msaada huo, usalama wa watu na mali, na utunzaji wa mizigo

 

Wageni Waalikwa, Wanahabari, Mabibi na Mabwana,

Ili kutekeleza jukumu la Kusajili Wahudumu na Kuthibitisha Madereva wa Vyombo vya Moto vinavyotoa Huduma za Usafiri Kibiashara kwa usafiri wa barabara na reli, Waziri mwenye dhamana ya Uchukuzi alitoa Kanuni  mbili (2) zifuatazo:

 

  1. Kanuni za Uthibitishaji Madereva wa Treni na Usajili wa Wahudumu wa Treni, yaani The Land Transport Regulatory Authority (Certification of Train Drivers and Registration of Train Crew), Regulations, 2020, zilizotangazwa katika Gazeti la Serikali (GN) Na. 80 la tarehe 7 Februari, 2020.  Hata hivyo, Kanuni hii haijaanza kutekelezwa, wataalamu wetu wa sekta ndogo ya reli bado wako kwenye maandalizi ya utaratibu utakaotumika.

 

  1. Kanuni za Uthibitishaji Madereva wa Magari ya Kibiashara na Usajili wa Wahudumu, yaani The Land Transport Regulatory Authority (Certification of Commercial Vehicle Drivers and Registration of Crew), Regulations, 2020, zilizotangazwa katika Gazeti la Serikali (GN) Na. 81 la tarehe 7 Februari, 2020.  Hatua hii iliiwezesha Mamlaka kuanza kutekeleza jukumu la uthibitishaji wa Madereva tarehe 1 Juni, 2022 na tumepanga kuanza rasmi Usajili wa Wahudumu mwezi Januari, 2024 baada ya walengwa kushiriki mafunzo na kupata vyeti baada ya kufanya mitihani na kufaulu.

 

Wageni Waalikwa, Wanahabari, Mabibi na Mabwana,

Uamuzi wa Mamlaka wa kutoa mafunzo kwa wahudumu kabla ya kuwasajili unatokana na kukosekana kwa wahudumu waliopata mafunzo rasmi katika sekta ya usafiri ardhini, na pia kukosekana kwa uelewa wa Sheria na Kanuni za huduma za usafiri unaosababisha kuwepo kwa malalamiko mengi kutoka kwa abiria kuhusu mienendo isiyofaa wahuduma wanapokuwa katika utekelezaji wa majukumu yao.

 

Hivyo, katika mafunzo haya, mkazo utawekwa kwenye kufahamu Sheria, Taratibu, Kanuni na Kujali Wateja (Customer Care). Kanuni itayosisitizwa ni hii inayohusu Usajili wa Wahudumu ili wajue majukumu yao na pale wasipotimiza majukumu yao wafahamu wanatenda kosa lenye kustahili adhabu.

 

Wageni Waalikwa, Wanahabari, Mabibi na Mabwana,

Kufuatia malalamiko hayo kutoka kwa watumiaji wa huduma za usafiri wa abiria nchini, na  kuwepo kwa Kanuni za Uthibitishaji Madereva na Usajili wa Wahudumu wa Vyombo vya Moto Kibiashara, Mamlaka kwa kushirikiana na wasafirishaji ikiwemo Vyama vya Wamiliki wa Mabasi ya masafa marefu na mijini (TABOA na DARCOBOA) na wadau wengine wa sekta ya usafirishaji nchini mwezi Septemba, 2022 tulikamilisha kuandaa mwongozo wa uandaaji mitaala itakayotumika kutoa mafunzo kwa kundi hilo kwa kuzingatia mahitaji ya kisheria, mahitaji ya jamii na watoa huduma za usafiri nchini. Mwongozo huo umetumiwa na vyuo washirika katika kuandaa mitaala iliyozinduliwa rasmi tarehe 1 Julai, 2023 ili vyuo hivyo vianze kutoa mafunzo kwa kundi linalokusudiwa na baadae Mamlaka ikamilishe jukumu la kuwasajili wahudumu wa magari ya kibiashara na kutoa vitambulisho kwa mujibu wa Kanuni.

 

Wageni Waalikwa, Wanahabari, Mabibi na Mabwana,

Kwa kuwa Mamlaka inawajali wahudumu wa vyombo vya abiria na tunapenda wafaulu kwa wingi, naomba nitumie fursa hii kuwahimiza na kuwasihi wahudumu/makondakta watakapoanza masomo, kuzingatia masomo yao, kusoma kwa bidii na baada ya kufaulu kufika LATRA kwa ajili ya kusajiliwa.  Usajili utafanyika kupitia mfumo wetu wa kidigiti (rrims.latra.go.tz) na kila muombaji atatakiwa kuwa na namba ya Kitambulisho cha Taifa (NIDA), Cheti cha mafunzo kutoka CBE au NIT na Cheti cha Uchunguzi wa Afya ili waweze kusajiliwa.

 

Vilevile nitumie nafasi hii kuwajulisha watoa huduma za usafiri nchini kwamba, Moja ya masharti ya Kanuni za Uthibitishaji wa Madereva na Usajili wa Wahudumu za mwaka 2020 ni kila mhudumu anayefanya kazi kwenye chombo cha usafiri kibiashara hususan magari ya abiria, kuhakikisha kuwa ana Kadi ya Usajili iliyotolewa na Mamlaka. Sharti hilo, limeainishwa kwenye Kanuni ya 20(1)(d).

 

Wageni Waalikwa, Wanahabari, Mabibi na Mabwana,

Kuna faida nyingi za wahudumu wetu kuhudhuria mafunzo na kisha kusajiliwa na LATRA. Faida hizo ni pamoja na:

  • Wamiliki kupata wasimamizi mahiri na weledi wa kazi waliyopewa;
  • Wahudumu kufanya kazi kwa weledi, umakini na ufanisi zaidi;
  • Kuboresha huduma za usafiri ardhini hususana wa abiria nchini;
  • Abiria kuvutiwa na huduma nzuri inayotolewa na kupata amani safarini;
  • Kurasimisha kazi ya wahudumu iheshimike kama zilivyo kazi nyingine;
  • Kulinda mitaji ya wamiliki wa vyombo na vipato vya wahudumu;
  • Kuwezesha taasisi zinazoshughulikia masuala ya ajira kuwa na taarifa sahihi zinazowezesha kusimamia maslahi ya wahudumu katika ajira;  na
  • Kuongeza nidhamu na uwajibikaji kwa wahudumu na watumiaji wa huduma.

 

Aidha, zipo hasara zinazoweza kutokana na adhabu (faini) na hivyo, kuongeza gharama za uendeshaji. Mafunzo haya yatasaidia wahudumu na pia madereva na wamiliki kuepuka faini zitokanazo na ukiukwaji wa Kanuni. Baadhi ya makosa na adhabu zilizotajwa kwenye Kanuni husika ni kama ifuatavyo:

 

 

 

A: Madereva

Kosa

Faini (Sh.)

Kuendesha gari bila kusajiliwa na kuthibitishwa na LATRA

50,000

Kwenda mwendo kasi zaidi ya ule wa kisheria

50,000

Kuzidisha abiria zaidi ya idadi inayoruhusiwa kwenye chombo

30,000

Kuendesha gari wakati mlango wa abiria upo wazi

30,000

Kutozingatia ratiba ya gari iliyotolewa na Mamlaka

50,000

Kupeleka gari kwenye ruti ambayo haikuainishwa kwenye leseni

30,000

Kukatisha safari kwa kutowafikisha abiria kwenye kituo cha mwisho

50,000

Kuendesha gari isiyokuwa na leseni ya LATRA au Bima

50,000

Kuendesha gari bila kuvaa sare (uniform)

30,000

Kuendesha gari bila kuwa na kitambulisho (identity card)

30,000

Kuendesha gari pamoja na kutumia simu ya mkononi

50,000

Kutotii amri halali ya Polisi au Afisa wa Mamlaka (LATRA)

50,000

Kumtendea mabaya au kunyanyasa abiria

30,000

Kuwazuia makusudi watumiaji wengine wa barabara

30,000

Kubeba wanyama hai au bidhaa hatarishi kwenye gari

30,000

 

B: Wahudumu/Makondakta

Kosa

Faini (Sh.)

Kuwa Mhudumu/Kondakta bila ya Kusajiliwa na LATRA

20,000

Kubeba bidhaa hatarishi kwenye gari

20,000

Kuzidisha abiria zaidi ya idadi inayoruhusiwa kwenye chombo

20,000

Kutovaa sare (uniform) nadhifu

20,000

Kutotangazia abiria masuala ya usalama kabla ya safari kuanza

20,000

Kushindwa kusimamia chombo cha kutunza taka ndani ya basi

20,000

Kutotoa tiketi za kielektroniki (tiketi mtandao) kwa abiria

20,000

Kushindwa kuwajali na kutoa huduma bora kwa abiria

20,000

Kutumia lugha mbaya na chafu kwa abiria

20,000

Kutoweka alama (tag) kwenye mzigo wa abiria

20,000

 

Wageni Waalikwa, Wanahabari, Mabibi na Mabwana,

Tunashukuru kwamba maandalizi ya kuanza utekelezaji wa kutoa mafunzo kwa upande wa vyuo vya CBE na NIT yamekamilika na maandalizi ya usajili wahudumu kwa upande wa LATRA pia yamekamilika. Mchakato uliowezesha kukamilika kwa maandalizi haya umezingatia misingi ya utawala bora kwa kuwashirikisha wadau wetu muhimu katika mchakato huo na kufikia maamuzi kwa pamoja. Kama yapo mapungufu, bado tuna nafasi za maboresho kwa pamoja.

Mamlaka inawasihi wamiliki wa vyombo vya usafiri kibiashara kuhakikisha wahudumu / makondakta wao wote wanapata mafunzo haya kabla ya kusajiliwa LATRA. Mamlaka itangaza tarehe ya mwisho ya usajili ambapo, baada ya tarehe hiyo kupita, hatutatoa leseni kwa chombo chochote cha usafiri wa umma bila kuwa na watoa huduma/makondakta waliosajiliwa LATRA. Hivyo, tusingoje kutangaziwa tukaanza kukimbizana, tuanze sasa, tuwahi fursa za kuboresha huduma tupate wateja/abiri zaidi na tufanye vizuri zaidi kila siku.

 

 

Wageni Waalikwa, Wanahabari, Mabibi na Mabwana,

Kwa kutambua na kuthamini mchango wa wadau wetu wa usafiri wa abiria na kwa namna walivyoshiriki kwenye mchakato huu hadi kufikia siku ya leo, Mamlaka imeamua kuwadhamini kwa kulipa ada za mafunzo kwa washiriki kumi (10) (CBE – 5 na NIT-5) kwa kampuni/wamiliki 10 wa mwanzo waliowasilisha orodha ya wahudumu / makondakta wao waliokuwa tayari kuanza mafunzo haya. Taratibu za kuanza tutaelezwa na vyuo husika.

 

Wageni Waalikwa, Wanahabari, Mabibi na Mabwana,

Baada ya kusema haya, naomba sasa nitamke kwamba, leo Jumatano, tarehe 22 Novemba, 2023, nimezindua kuanza rasmi kwa mafunzo ya wahudumu/ makondakta wa vyombo vinavyotoa huduma za usafiri kibiashara. Mafunzo hayo yatatolewa kwa kuzingatia mitaala ya CBE na NIT iliyozinguliwa rasmi na Mheshimiwa Naibu Waziri wa Uchukuzi, tarehe 1 Julai, 2023.

 

Asanteni kwa kunisikiliza

CPA Habibu J. Suluo

MKURUGENZI MKUU - LATRA

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo