Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

HOTUBA YA WAZIRI WA UCHUKUZI MHESHIMIWA PROF. MAKAME MNYAA MBARAWA (MB.), AKIWASILISHA BUNGENI MPANGO NA MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA FEDHA KWA MWAKA WA FEDHA 2024/25
06 May, 2024 Pakua

A: UTANGULIZI


1.    Mheshimiwa Spika, baada ya kupokea taarifa iliyowasilishwa hapa Bungeni na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu iliyochambua utekelezaji wa Bajeti ya Wizara ya Uchukuzi kwa mwaka wa fedha 2023/24 pamoja na Mpango na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya fedha kwa Mwaka wa Fedha 2024/25, ninaomba kutoa hoja kwamba Bunge lako Tukufu sasa likubali kupokea, kujadili na kuidhinisha Mpango na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya fedha ya Wizara ya Uchukuzi kwa mwaka wa fedha 2024/25.

2.    Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa naomba nitumie fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu Mwingi wa Rehema kwa kutujalia kukutana hapa leo tukiwa na afya njema.

3.    Mheshimiwa Spika, utakumbuka kuwa, tarehe 30 Agosti, 2023 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan aliunda Wizara ya Uchukuzi baada ya kugawanywa kwa iliyokuwa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi. Tangu kuundwa kwake, Wizara ya Uchukuzi imeendelea kutekeleza kazi zake kulingana na Hati ya Mgawanyo wa Majukumu iliyotolewa. Kwa heshima kubwa, ninaomba nimshukuru Mheshimiwa Rais kwa kuendelea kuniamini na kuniteua kuwa Waziri wa Uchukuzi. Ninaomba kumhakikishia Mhe. Rais na Bunge lako Tukufu kuwa nitaendelea kutekeleza majukumu yangu kwa uaminifu mkubwa ili
 
kuliletea Taifa letu maendeleo. Kwa muktadha huo, naomba kutoa Hotuba yangu ya kwanza ya Wizara ya Uchukuzi ambayo imejikita katika masuala ya usimamizi na uwezeshaji wa maendeleo ya miundombinu, huduma za uchukuzi na hali ya hewa kwa lengo la kuleta maendeleo endelevu kwa Wananchi. Aidha, napenda kumpongeza Mheshimiwa Innocent Lugha Bashungwa (Mb.) kwa kuteuliwa kuwa Waziri wa Ujenzi baada ya iliyokuwa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kugawanywa.

4.    Mheshimiwa Spika, kwa namna ya kipekee, niruhusu nitumie fursa hii kuungana na Bunge lako Tukufu katika kumpongeza kwa dhati Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuliongoza Taifa letu na kutimiza miaka mitatu (3) katika uongozi wake mahiri ulioleta mafanikio makubwa. Pamoja na juhudi nyingine, Mheshimiwa Rais ameendelea kuweka mkazo na kipaumbele katika kuboresha na kuendeleza miundombinu na huduma za uchukuzi ikiwemo: ujenzi wa reli ya Standard Gauge Railway (SGR); uboreshaji wa bandari; ukarabati na ujenzi wa meli; ujenzi wa boti za utafutaji na uokoaji katika Maziwa Makuu; uendelezaji wa viwanja vya ndege; ununuzi wa mitambo ya kuongozea ndege; ununuzi wa ndege; ununuzi wa rada za hali ya hewa; na ununuzi wa vifaa vya kufundishia katika Vyuo vinavyosimamiwa na Wizara.

5.    Mheshimiwa Spika, naomba kutoa pongezi na shukrani za dhati kwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Isdory Mpango kwa namna anavyoendelea kumsaidia Mheshimiwa Rais katika utendaji na kuongoza nchi yetu kwa ajili ya kuwaletea maendeleo Wananchi na Taifa kwa ujumla. Ni dhahiri kuwa, utendaji wake umeleta chachu kubwa katika utendaji wa Serikali ya Awamu ya Sita.
 
6.    Mheshimiwa Spika, vilevile nimpongeze Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Kiongozi wa shughuli za Serikali Bungeni, Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb.), kwa uongozi wake makini. Kwa hakika kazi anazozifanya katika utekelezaji wa majukumu yake ndani na nje ya Bunge zimekuwa na ufanisi mkubwa katika kusimamia utekelezaji wa shughuli za Serikali.

7.    Mheshimiwa Spika, pia nimpongeze Naibu Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Waziri wa Nishati, Mheshimiwa Dkt. Doto Mashaka Biteko (Mb.) kwa kuaminiwa na kuteuliwa na Mheshimiwa Rais katika nafasi hiyo. Kwa hakika Naibu Waziri Mkuu ameonesha umakini mkubwa katika kutekeleza majukumu yake.

8.    Mheshimiwa Spika, nitumie nafasi hii kukupongeza wewe binafsi kwa kazi kubwa unayoifanya ya kuliongoza Bunge letu Tukufu kwa weledi mkubwa na pia kwa heshima kubwa nakupongeza kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU). Tunakuombea M/Mungu aendelee kukupa afya njema ya kutekeleza majukumu yako ya kitaifa na kimataifa kwa ufanisi.

9.    Mheshimiwa Spika, aidha, nimpongeze Naibu Spika Mheshimiwa Mussa Azzan Zungu (Mb.), kwa kuendelea kutekeleza vyema majukumu yake katika kumsaidia Spika kuliongoza Bunge. Vilevile, nitumie fursa hii kumpongeza Mwenyekiti wa Bunge, Mheshimiwa Najma Murtaza Giga (Mb.), kwa kuendelea kuaminiwa na Waheshimiwa Wabunge kuwa Mwenyekiti wa Bunge letu.

10.    Mheshimiwa Spika, vilevile nawapongeza Mheshimiwa Dkt. Joseph Kizito Mhagama, Mbunge wa Jimbo la Madaba na Mheshimiwa Deo Philip Mwanyika, Mbunge wa Jimbo la Njombe Mjini kwa kuteuliwa kushika nyadhifa za uenyekiti wa Bunge. Pia niwapongeze Mheshimiwa David Mwakiposa Kihenzile (Mb.) na Mheshimiwa Daniel Baran Sillo (Mb.) waliokuwa Wenyeviti wa Bunge kwa kuaminiwa na kuteuliwa kuwa Naibu Mawaziri wa Wizara za: Uchukuzi na Mambo ya Ndani ya Nchi, mtawalia.

11.    Mheshimiwa Spika, kwa dhati kabisa naomba kuishukuru na kuipongeza Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu inayoongozwa na Mwenyekiti wa Kamati Mheshimiwa Selemani Moshi Kakoso (Mb.) na Makamu Mwenyekiti wa Kamati Mheshimiwa Anne Kilango Malecela (Mb.). Sambamba na viongozi hao wa Kamati, niwashukuru Wajumbe wote wa Kamati. Kamati hii imeendelea kutoa maelekezo na ushauri wenye tija kwa Wizara.

12.    Mheshimiwa Spika, kwa simanzi kubwa nichukue fursa hii kutoa pole nyingi kwa Bunge lako Tukufu na Taifa kwa ujumla kufuatia kifo cha Hayati Mhe. Ali Hassan Mwinyi, aliyekuwa Rais wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Awamu ya Pili kilichotokea tarehe 29 Februari, 2024 na kifo cha Hayati Mhe. Edward Ngoyai Lowassa, aliyekuwa Waziri Mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Awamu ya Nne kilichotokea tarehe 10 Februari, 2024. Hakika tutaendelea kujifunza kutokana na utumishi wao katika kulitumikia Taifa. Aidha, nitoe pole kwa Bunge lako Tukufu kufuatia kifo cha Hayati Mhe. Francis Leonard Mtega aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Mbarali, kilichotokea tarehe 1 Julai, 2023 na kifo cha Hayati Mhe. Ahmed Yahya Abdulwakil aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Kwahani kilichotokea tarehe 8 Aprili, 2024. Tutaendelea kuthamini na kuenzi michango yao katika Bunge hili na Taifa kwa ujumla.
 
13.    Mheshimiwa Spika, napenda kuwapongeza watoa hoja wote waliowasilisha hotuba zao kabla yangu. Kipekee nimshukuru Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb), Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa hotuba yake ambayo imetoa hali ya utekelezaji wa ujumla katika utendaji wa Serikali kwa mwaka 2023/24 pamoja na kuonesha dira na mwelekeo wa Taifa letu kwa mwaka 2024/25 katika sekta mbalimbali ikiwemo Sekta ya Uchukuzi.

14.    Mheshimiwa Spika, baada ya kutoa maelezo hayo ya utangulizi, naomba sasa uniruhusu nitoe taarifa ya mapitio ya Utekelezaji wa Mpango na Bajeti ya Wizara ya Uchukuzi kwa mwaka wa fedha 2023/24 pamoja na Mpango na Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa fedha 2024/25.

B: MAPITIO YA UTEKELEZAJI WA MPANGO NA BAJETI YA WIZARA NA TAASISI ZAKE KWA MWAKA WA FEDHA 2023/24

1.    Mheshimiwa Spika, Sekta ya Uchukuzi imeendelea kutoa mchango mkubwa wa ukuaji wa Uchumi kwa Taifa kwa kuwa ni sekta wezeshi katika kuchagiza ukuaji wa sekta nyingine za uzalishaji zikiwemo sekta za kilimo, madini, utalii, viwanda na biashara. Mathalan, katika mwaka 2022 Sekta ya Uchukuzi ilikua kwa asilimia
3.80 na kuchangia katika Pato la Taifa kwa asilimia 6.70. Aidha, Sekta hii ni ya tatu
(3) kwa kuchangia fedha za kigeni kupitia mauzo ya huduma (Trade in Services). Aidha, katika kipindi cha miaka mitatu, mchango wa sekta hii katika fedha za kigeni umeongezeka kwa kiasi kikubwa kutoka Dola za Marekani bilioni 1.6 mwaka 2022 hadi kufikia Dola za Marekani bilioni 2.4 mwaka 2024, sawa na ongezeko la asilimia 50 katika kipindi hicho.
 
2.    Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2023/24, Wizara ya Uchukuzi (Fungu 62) iliidhinishiwa jumla ya Shilingi Trilioni 2.089 kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida na utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo. Kati ya fedha hizo, Shilingi Bilioni 118.215 ni za Matumizi ya Kawaida ya Wizara na Taasisi zake na Shilingi Trilioni 1.971 ni za utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo.

3.    Mheshimiwa Spika, hadi kufikia Machi, 2024 Wizara ilikuwa imepokea jumla ya Shilingi Trilioni 1.827 sawa na asilimia 87.48 ya bajeti yote ya Wizara iliyoidhinishwa. Kati ya fedha hizo zilizopokelewa, Shilingi Bilioni 71.125 ni fedha Za Matumizi ya Kawaida ambazo ni sawa na asilimia 60.16 ya bajeti ya Matumizi ya Kawaida iliyoidhinishwa; na Shilingi Trilioni 1.756 ni fedha za Miradi ya Maendeleo ambazo ni sawa na asilimia 89.12 ya bajeti ya Maendeleo iliyoidhinishwa.

4.    Mheshimiwa Spika, baada ya kupokea fedha hizo, Wizara ya Uchukuzi iliendelea na utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya kimkakati.

Udhibiti wa huduma za Usafiri wa Anga
5.    Mheshimiwa Spika, Wizara kupitia Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) imeendelea kutoa huduma za udhibiti wa usafiri wa anga nchini.

6.    Mheshimiwa Spika, hadi kufikia Machi, 2024, TCAA ilifanya uchunguzi na kusajili ndege 15 ambazo zilipewa vyeti vya ubora (Certificate of Airworthiness). Aidha, jumla ya ndege mbili (2) ziliondolewa kwenye Daftari la Usajili baada ya kumalizika kwa mikataba ya ukodishaji. Ndege nyingine 91 zilikaguliwa na kupewa vyeti vya ubora ili kuendelea kutoa huduma nchini. Ukaguzi huo umewezesha daftari la usajili wa ndege kuwa na jumla ya ndege 419.
 

7.    Mheshimiwa Spika, katika kuongeza wigo wa soko la usafiri wa anga nchini kwa kuvutia Mashirika ya ndege ya kimataifa kutoa huduma za usafiri wa anga pamoja na kuimarisha ushindani katika utoaji wa huduma, Serikali kupitia TCAA imeendelea kusaini mikataba mipya na kuipitia mikataba iliyopo ya usafiri wa Anga (Bilateral Air Services Agreements - BASA) baina ya Tanzania na nchi nyingine. Hadi kufikia Machi 2024, Serikali ilifanikiwa kusaini Hati za Makubaliano tano (5) za nchi za Poland, Suriname, Algeria, Jamhuri ya Czech na Ivory Coast. Makubaliano hayo yaliyosainiwa yanaifanya Tanzania kuwa na Mikataba ya BASA na nchi 85 ikilinganishwa na nchi 80 iliyokuwa imeingiwa hadi kufikia mwaka wa fedha 2022/23. Mikataba ya BASA imewezesha Mashirika 25 ya ndege za kimataifa kutoa huduma nchini.

8.    Mheshimiwa Spika, TCAA pia iliratibu shughuli za usafirishaji wa abiria na mizigo ambapo hadi kufikia Machi, 2024 abiria waliosafiri kwa kutumia usafiri wa anga wameongezeka hadi abiria 5,080,920 ikilinganishwa na abiria 4,105,375 katika kipindi kama hicho cha mwaka 2022/23, ambayo ni sawa na ongezeko la asilimia
23.76. Vilevile, mizigo iliyosafirishwa imeongezeka hadi kufikia tani 27,532 ikilinganishwa na tani 23,070.3 katika kipindi kama hicho mwaka 2022/23 sawa na ongezeko la asilimia 19.33. 
(Utendaji wa utoaji wa huduma za usafiri wa anga na utekelezaji wa miradi kupitia TCAA umeainishwa katika Kitabu cha Hotuba yangu kuanzia uk 14 hadi uk 23).
 
Udhibiti wa Usafiri Ardhini
10.    Mheshimiwa Spika, udhibiti wa Usafiri Ardhini unaojumuisha usafiri kwa njia ya barabara, usafiri wa reli, na usafiri kwa njia ya waya unatekelezwa na Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA).

11.    Mheshimiwa Spika, katika kudhibiti mwenendo wa mabasi ya masafa marefu na treni, Serikali kupitia LATRA imeendelea kufuatilia mwenendo wa mabasi na vichwa vya treni kupitia Mfumo wa Ufuatiliaji wa Mwenendo wa Vyombo (Vehicle Tracking System – VTS). Hadi kufikia Machi, 2024 mabasi 10,270 yanayotoa huduma ya usafiri wa masafa marefu na vichwa vya treni 20 (TAZARA - 18 na TRC- 2) vimeunganishwa katika mfumo huo. Matumizi ya mfumo huo yamepunguza ajali zitokanazo na mwendokasi na kuongeza ufanisi wa vyombo vinavyodhibitiwa ambapo kwa mwaka 2022/23 ajali zilipungua hadi kufikia ajali 166 za mabasi ya masafa marefu ikilinganishwa na ajali 179 zilizotokea mwaka 2021/22.

12.    Mheshimiwa Spika, utakumbuka kuwa, tarehe 28 Juni 2023, Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb.), Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, alitangaza hapa Bungeni uamuzi wa Serikali wa kuondoa zuio la mabasi ya abiria kusafiri nyakati za usiku lililowekwa mwaka 1994. Napenda kulitaarifu Bunge lako Tukufu kuwa, Serikali kupitia Wizara ya Uchukuzi na LATRA ilifanya maandalizi na kuanza kutoa ratiba za mabasi kusafiri nyakati za usiku kuanzia tarehe
1 Oktoba, 2023. Hadi kufikia Machi, 2024 jumla ya ratiba za mabasi 798 zimetolewa kwa ajili ya safari za usiku. Ni dhahiri kuwa, Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imeonesha dhamira ya kweli ya kuifungua nchi kiuchumi. (Utendaji wa udhibiti wa usafiri ardhini LATRA umeoneshwa katika Kitabu cha Hotuba yangu katika uk. 23 mpaka uk. 31).

Udhibiti wa Usafiri Majini


13.    Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) imeendelea kutoa huduma za udhibiti wa huduma za bandari, usafiri wa majini Tanzania Bara na kutoa huduma ya biashara ya meli kwa bidhaa mahsusi.

14.    Mheshimiwa Spika, kuhusu usimamizi wa watoa huduma zinazodhibitiwa, Serikali kupitia TASAC imeendelea kutoa leseni na vyeti vya usajili kwa watoa huduma waliokidhi vigezo. Hadi kufikia Machi, 2024 jumla ya watoa huduma 1,722 walisajiliwa na kupewa leseni ikilinganishwa na jumla ya watoa huduma 1,498 katika kipindi kama hicho kwa mwaka 2022/23 sawa na ongezeko la asilimia 14.95.

15.    Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia TASAC katika kipindi cha kuanzia Julai, 2023 hadi Machi, 2024 imeendelea kurasimisha bandari bubu za Tanzania Bara. Katika kutekeleza jukumu hilo, bandari bubu 99 zilikaguliwa na kufanyiwa tathmini ya kina na Serikali kupitia TASAC kwa kushirikishana na Mamlaka mbalimbali za Serekali ambapo bandari 45 zilirasimishwa. Lengo la hatua hii ni kuhakikisha kuwa Serikali inaimarisha ulinzi na usalama katika maeneo ya bandari ili kuboresha utoaji wa huduma.

16.    Mheshimiwa Spika, kuhusu shughuli za utafutaji na uokoaji, Serikali kupitia TASAC imeendelea kuratibu shughuli hizo kupitia Vituo vya Utafutaji na Uokoaji Majini vilivyopo Dar es Salaam na Mwanza (Maritime Rescue and Coordination Centre – MRCC).
 

17.    Mheshimiwa Spika, ili kuboresha usalama wa usafiri katika Ziwa Victoria, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Jamhuri ya Uganda chini ya uratibu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kupitia Kamisheni ya Bonde la Ziwa Victoria zimeendelea kutekeleza Mradi wa Kikanda wa Kuboresha Mawasiliano na Uchukuzi Katika Ziwa Victoria wenye lengo la kuimarisha huduma za utafutaji na uokoaji katika Ziwa. Hadi kufikia Machi, 2024 ujenzi wa Kituo Kikuu cha Kikanda cha Uratibu wa Masuala ya Utafutaji na Uokoaji katika Ziwa Victoria (Regional Maritime Rescue Coordination Centre - RMRCC) umefikia asilimia 26. Aidha, ujenzi wa vituo vidogo vitatu (3) vya utafutaji na uokoaji unaendelea vizuri. (Utendaji wa TASAC umeoneshwa katika Kitabu cha Hotuba yangu kuanzia uk. 32 mpaka uk. 44).

Huduma za Hali ya Hewa
18.    Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imeendelea na utoaji wa huduma na kuratibu shughuli za hali ya hewa nchini. TMA imeendelea kutoa utabiri wa kila siku, wa siku kumi na ule wa muda mrefu pamoja na tahadhari ya matukio ya hali mbaya ya hewa ili kuhakikisha usalama wa watu na mali zao.

19.    Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia TMA imekamilisha ufungaji wa rada za hali ya hewa katika mikoa ya Kigoma na Mbeya na kufikisha jumla ya rada tano (5) za hali ya hewa nchini. Aidha, utengenezaji wa rada nyingine mbili (2) unaendelea na zinatarajiwa kukamilika mwezi Novemba, 2024 na zitafungwa katika mikoa ya Kilimanjaro na Dodoma.(Utendaji wa TMA umeoneshwa katika Kitabu cha Hotuba yangu kuanzia uk. 44 mpaka uk. 50)

Huduma za Bandari


20.    Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imeendelea kusimamia na kutoa huduma zote kibandari katika Bandari zote za TAnzania Bara.

21.    Mheshimiwa Spika, hadi kufikia Machi, 2024 TPA ilihudumia tani milioni
20.72 ya shehena ya mizigo ikilinganishwa na tani milioni 14.56 katika kipindi kama hicho mwaka wa fedha 2022/23, sawa na ongezeko la asilimia 42.31. Aidha, kwa upande wa makasha, TPA ilihudumia makasha 805,167 ikilinganishwa na makasha 688,609 katika kipindi kama hicho mwaka 2022/23 sawa na ongezeko la asilimia 16.92. Ongezeko hilo la shehena ya mizigo na makasha limetokana na mikakati mbalimbali inayoendelea kutekelezwa ikiwa ni pamoja na uboreshaji wa Bandari za Dar es Salaam, Tanga na Mtwara.

22.    Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia, TPA imeendelea kutekeleza miradi ya maendeleo ikiwemo ujenzi na uboreshaji wa bandari nchini pamoja Bandari Kavu. Aidha, TPA imeendelea na juhudi mbalimbali za kuboresha huduma zake ikiwa ni pamoja na kufungua ofisi nje ya nchi; kutafuta masoko; na kufanya ununuzi wa vifaa na mitambo kwa ajili ya kuboresha utoaji wa huduma katika bandari nchini.

23.    Mheshimiwa Spika, kuhusu uboreshaji wa Bandari ya Dar es Salaam, TPA imeendelea kutekeleza kazi mbalimbali ambapo uchimbaji wa kina umefikia mita
15.5 na upanuzi wa lango la kuingia meli ambalo lina una upana wa mita 200. Kwa sasa, Bandari ina uwezo wa kupokea meli kubwa zenye urefu wa mita 305. Aidha, upembuzi yakinifu wa kuboresha Gati Na. 8 – 11 na ujenzi wa Gati Na. 12 - 15 bado unaendelea. Vilevile, mkataba wa kuendeleza miundombinu ya kupokelea mafuta (Single Receiving Terminal - SRT) unaohusisha ujenzi wa matenki 15 ya mafuta (tank farms) pamoja na miundombinu yake, yenye uwezo wa kuhifadhi kiasi cha mita za ujazo 420,000 umesainiwa tarehe 26 Februari, 2024 na maandalizi ya kuanza ujenzi yanaendelea.

24.    Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Wizara ya Uchukuzi imeendelea kushirikisha sekta binafsi katika uendeshaji wa Bandari ya Dar es Salaam kwa baadhi ya maeneo ya bandari kwa kuingia ubia na Kampuni Binafsi katika kuendeleza na kuendesha shughuli za bandari kuanzia Gati Na. 4 hadi 7. Kwa sasa hatua mbalimbali zikiwemo za makabidhiano na mobilization zinaendelea ili kuruhusu utekelezaji rasmi kuanza. Aidha, Serikali inaendelea na taratibu za kumpata Mwekezaji mwingine atakayekuwa na jukumu la kufanya shughuli za uendeshaji kuanzia Gati Namba 8 hadi 11. Lengo ni kuongeza tija katika utendaji wa bandari.(Utendaji wa TPA umeoneshwa katika Kitabu cha Hotuba yangu kuanzia uk. 51 hadi 59).
 
Huduma za Usafiri wa Reli Shirika la Reli Tanzania (TRC)
25.    Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Shirika la Reli Tanzania (TRC) imeendelea kutekeleza majukumu yake ya kusimamia na kuendeleza miundombinu ya reli iliyopo ya Meter Gauge Railway (MGR) yenye urefu wa kilomita 2,706 na kutoa huduma ya usafirishaji wa abiria na mizigo kwa kutumia reli hiyo. Aidha, Serikali inaendelea na ujenzi wa Reli ya Kisasa ya Standard Gauge Railway (SGR) ya ushoroba wa kati kwa awamu zote mbili ambapo awamu ya kwanza ina jumla ya kilomita 1,219 na awamu ya pili ina jumla ya kilometa 1,590 na hivyo kufanya reli mpya ya SGR inayojengwa kuwa na mtandao wenye jumla ya kilomita 2,809 ambazo ni zaidi ya kilomita 103 ikilinganishwa na reli ya MGR ambayo ilijengwa wakati wa Mkoloni. Pamoja na hatua hiyo, Serikali itaendelea na ujenzi wa reli ya SGR kwa maeneo mengine ya Ushoroba wa Kusini na wa Kaskazini kadri ya upatikanaji wa rasilimali fedha.

26.    Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2023/24, Serikali iliahidi kuendelea na ujenzi wa reli ya SGR kwa awamu zote mbili. Napenda kulitaarifu Bunge lako Tukufu kuwa, hadi kufikia Machi 2024, ujenzi wa kipande cha kutoka Dar es Salaam
– Morogoro (km 300) umefikia asilimia 98.93; kipande cha kutoka Morogoro – Makutupora (km 422) umefikia asilimia 96.61; kipande cha kutoka Mwanza – Isaka (km 341) umefikia asilimia 56.21; kipande cha Makutupora - Tabora (368 km) umefikia 14.22%, na Tabora - Isaka (165km) umefikia 5.72%. Kwa upande wa awamu ya pili, kipande cha kutoka Tabora – Kigoma (Km 506) umefikia asilimia 1.81; na ujenzi wa kipande cha Uvinza – Musongati – Gitega (km 282) umeanza ambapo hatua za ununuzi wa Mshauri Elekezi na Mkandarasi zinaendelea.

 

27.    Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza maagizo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuanza uendeshaji wa treni katika reli ya SGR kwa kipande cha Dar es Salaam hadi Dodoma, napenda kulitaarifu Bunge lako Tukufu kuwa, Wizara kupitia TRC inaendelea na majaribio ya miundombinu ya reli kwa ajili ya kuanza utoaji wa huduma hiyo rasmi ifikapo mwezi Julai, 2024. Aidha, majaribio haya yanafanyika kwa lengo la kukidhi takwa la usalama kabla ya kuanza uendeshaji.(Utendaji wa TRC umeoneshwa katika Kitabu cha Hotuba yangu Ukurasa kuanzia 60 hadi uk.76).

Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA)
28.    Mheshimiwa Spika, Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA) inamilikiwa na Serikali mbili za Tanzania na Zambia kwa hisa za asilimia 50 kwa
50. Katika kuendeleza huduma za reli kati ya nchi hizo mbili, TAZARA imeendelea kutekeleza jukumu lake la msingi la kutoa huduma za kusafirisha abiria na mizigo, kulinda na kuimarisha miundombinu ya reli yenye urefu wa jumla ya kilometa 2,153, na maeneo yote yaliyo ndani ya ukanda wa reli.

30.    Mheshimiwa Spika, hadi kufikia Machi 2024, TAZARA ilisafirisha jumla ya tani za mizigo 251,264 ikilinganishwa na tani 235,071 zilizosafirishwa katika kipindi kama hicho cha mwaka wa fedha 2022/23 sawa na ongezeko la asilimia 6.89. Ongezeko hilo limechangiwa na ushirikishaji wa sekta binafsi ya Kampuni Ms Calabash Freight Limited na Ms African Inland Container Depot (AFICD). Utaratibu huu umeiingizia TAZARA mapato ya Shilingi bilioni 8.91 kutokana na Kampuni hizo kulipia tozo.
 
31.    Mheshimiwa Spika, treni za abiria zinazofanya safari kati ya Dar es Salaam na New Kapiri Mposhi na ile inayosafiri kati ya stesheni za Kidatu na Makambako zilisafirisha jumla ya abiria 672,006. Aidha, Treni ya Jijini Dar es Salaam inayofanya safari zake kati ya Stesheni ya TAZARA hadi Stesheni ya Mwakanga - Pugu jijini Dar es Salaam ilisafirisha abiria 1,582,833 ikilinganishwa na abiria 1,447,738 waliosafirishwa katika kipindi kama hicho mwaka wa fedha 2022/23 sawa na ongezeko la asilimia 9.33. 
(Utendaji wa TAZARA umeoneshwa katika Kitabu cha Hotuba yangu kuanzia uk 76 hadi uk.80).

Huduma za Uchukuzi katika Maziwa Makuu
33.    Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL) imeendelea kutoa huduma za usafiri na usafirishaji katika Maziwa Makuu ya Victoria, Tanganyika na Nyasa.

34.    Mheshimiwa Spika, hadi kufikia Machi, 2024 MSCL ilisafirisha abiria 198,080 ikilinganishwa na abiria 170,137 waliosafirishwa katika kipindi kama hicho mwaka wa fedha 2022/23 sawa na ongezeko la asilimia 16.42. Kwa upande wa mizigo, MSCL ilisafirisha tani 33,288.44 ikilinganishwa na tani 18,909 zilizosafirishwa katika kipindi kama hicho mwaka wa fedha 2022/23 sawa na ongezeko la asilimia
76.05. Ongezeko hili limetokana na kukamilika kwa ukarabati na kuanza kazi kwa meli ya MV. Umoja ambayo ilianza kutoa huduma mwezi Oktoba, 2023 katika Ziwa Victoria kati ya Bandari ya Mwanza Kusini na Bandari za Port bell na Jinja, Uganda.
 
35.    Mheshimiwa Spika Aidha, ujenzi wa Meli ya MV. Mwanza Hapa Kazi Tu umekamilika kwa asilimia 95 na tayari meli hiyo imefanyiwa majaribio ziwani ya mifumo na mitambo.

36.    Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia MSCL ilisaini Mkataba wa ujenzi wa meli mpya ya kubeba mizigo ya tani 3,000 katika Ziwa Victoria. Pia ilisaini mikataba 2 ya ujenzi wa meli ya mizigo ya tani 3500; na ujenzi wa kiwanda cha kujengea meli katika Ziwa Tanganyika. Ujenzi wa kiwanda hiki ni hatua muhimu ya kujivunia kwa Taifa letu kwa kuwa ni mara ya kwanza kujenga kiwanda cha aina hii hapa nchini ambapo kwa miaka ya nyuma meli nyingi zilikuwa zinatengenezwa nje ya nchi. Vilevile mradi wa ukarabati wa Mv. Liemba tayari umesainiwa.

(Utendaji wa MSCL umeoneshwa katika Kitabu cha Hotuba yangu kuanzia uk.81 hadi 86).

Huduma za Viwanja vya Ndege
37.    Mheshimiwa Spika, Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) ina jukumu la kuendesha na kuendeleza Viwanja vya Ndege 58 vya Serikali vilivyopo Tanzania Bara. Hadi kufikia Machi 2024, TAA ilihudumia jumla ya abiria 3,202,573 ikiwa ni sawa na ongezeko la asilimia 8.58 ikilinganishwa na abiria 2,949,508 waliohudumiwa katika kipindi kama hicho mwaka wa fedha 2022/23.

38.    Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha ulinzi na usalama katika viwanja vya ndege nchini kwa kuzingatia miongozo ya kitaifa na kimataifa, hadi kufikia Machi 2024, TAA ilikamilisha ujenzi wa uzio wa usalama wenye urefu wa kilometa 7.2 na ufungaji wa mfumo wa taa za kuongozea ndege (AGL) katika Kiwanja cha Ndege cha Dodoma. Aidha, ujenzi wa uzio wa usalama pamoja na ufungaji wa mfumo wa
 
kamera za usalama (CCTV) katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere umekamilika kwa asilimia 100.

39.    Mheshimiwa Spika, kwa kutambua umuhimu wa kuwa na viwanja vya ndege vyenye ubora, TAA imeendelea na uboreshaji wa Kiwanja cha Ndege cha Arusha ambapo ujenzi wa jengo jipya la abiria umekamilika kwa asilimia 98. Majengo mapya ya abiria katika viwanja vya ndege vya Kahama na Kilwa Masoko; yamekamilika wakati ujenzi wa jengo jipya la abiria katika Kiwanja cha Ndege cha Mpanda umekamilika kwa asilimia 97. Aidha, Usanifu wa Kina wa Jengo la Mnara wa Kuongozea Ndege katika Kiwanja cha Ndege cha Bukoba umekamilika na taratibu za ununuzi wa Mkandarasi zinaendelea.

40.    Mheshimiwa Spika, kupitia Hotuba yangu ya bajeti ya mwaka jana nililiarifu Bunge lako Tukufu kuwa, jukumu la ujenzi wa viwanja vya ndege litarijeshwa rasmi TAA kwa utaratibu maalum ambao hutoathiri miradi iliyokuwa imeanza kutekelezwa na TANROADS. Naomba kulitaarifu Bunge lako Tukufu kuwa jukumu hilo sasa limerejeshwa na linatekelezwa na TAA kwa miradi mipya na miradi iliyo chini ya asilimia 40 ya utekelezaji. Baada ya uamuzi huo, TAA imeendelea na utekelezaji wa miradi ya ujenzi na ukarabati wa viwanja vya ndege vya Moshi, Lindi, Mtwara, Mwanza na JNIA (Jengo la Pili la Abiria – TB II).

41.    Mheshimiwa Spika, katika jitihada za Serikali za kukuza fursa za ajira na uhaulishaji wa teknolojia (technological transfer) kwa wazawa, Serikali kupitia TAA imewezesha uwekezaji wa kiwanda cha uunganishaji na utengenezaji wa ndege ndogo katika Kiwanja cha Ndege cha Morogoro kupitia Kampuni ya Airplane Africa Limited. Kampuni hiyo inafanya kazi ya kuunganisha na kutengeneza ndege za kubeba abiria wawili (2) ambazo ni aina ya “Skyleader”. Kwa sasa kiwanda hicho
 
ni cha pekee Afrika Mashariki ambapo kina matawi katika nchi za Urusi, Jamhuri ya Czech, Ujerumani na China.

Huduma katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Kilimanjaro (KIA)


42.    Mheshimiwa Spika, katika hotuba yangu ya bajeti kwa mwaka 2023/24 niliahidi kuwa Serikali inaendelea na taratibu za kurejesha shughuli za uendeshaji wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Kilimanjaro (KIA) kwa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) kutoka KADCO. Napenda kulitaarifu rasmi Bunge lako Tukufu kuwa Serikali imekamilisha urejeshwaji wa Kiwanja cha KIA kwa TAA kutoka KADCO,na kiwanja hicho kwa sasa kinaendeshwa na TAA.

(Utendaji wa TAA umeoneshwa katika Kitabu cha Hotuba yangu kuanzia uk 86 hadi 98).

Huduma za Usafiri wa Anga


44.    Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuboresha utendaji wa Shirika la Ndege, Tanzania (ATCL) kwa kununua ndege mpya na kuboresha miundombinu wezeshi ya kutolea huduma ikiwa ni pamoja na majengo na karakana. Hadi kufikia Machi 2024, Serikali ilikamilisha malipo ya ndege tatu (3): ndege 2 za Boeing 737- 9 Max tayari zilishawasili nchini na zinafanya kazi na 1 ya Boeing 787-8 Dreamliner itawawasili mwishoni mwa mwezi huu. Kuwasili kwa ndege hizi kutaifanya ATCL kuwa na jumla ya ndege 16.

45.    Mheshimiwa Spika, katika kuendelea kuongeza wigo wa huduma zake, ATCL imeendelea kutoa huduma ya usafiri wa anga katika vituo 24 ambapo vituo 13 ni vya
 
ndani na vituo 11 ni vya nje ya nchi. Vituo vya ndani ya nchi ni Arusha, Bukoba, Dar es Salaam, Dodoma, Geita, Kilimanjaro, Kigoma, Songwe, Mpanda, Mwanza, Songea, Tabora na Zanzibar. Vituo vya nje ya nchi ni Bujumbura, Dubai, Entebbe, Hahaya, Guangzhou, Harare, Lubumbashi, Lusaka, Mumbai, Nairobi na Ndola.

46.    Mheshimiwa Spika, uboreshaji wa ATCL umeongeza utendaji wa ATCL ambapo hadi kufikia Machi, 2024, ATCL ilisafirisha abiria 850,660 ikilinganishwa na abiria 826,594 waliosafirishwa katika kipindi kama hicho mwaka wa fedha 2022/23 sawa na ongezeko la asilimia 2.91. Vilevile, ATCL iliweza kusafirisha jumla ya tani 5,034.2 za mizigo ndani na nje ya nchi ikilinganishwa na tani 2,680.9 katika kipindi kama hicho mwaka wa fedha 2022/23 sawa na ongezeko la asilimia
87.78. Ongezeko hilo limetokana na kuanza kufanya kazi kwa ndege ya mizigo aina ya Boeing 767-300F yenye uwezo wa kubeba tani 54.

(Utendaji wa ATCL umeainishwa katika Kitabu cha Hotuba yangu kuanzia uk.98 hadi uk. 107)

B. 1: VYUO VYA MAFUNZO YA KISEKTA


47.    Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza azma ya Serikali ya kujenga uwezo na kutumia wataalam wa ndani pamoja na kupunguza gharama za kusomesha wataalam nje ya nchi. Serikali kupitia vyuo vya kisekta vinavyosimamiwa na Wizara ya Uchukuzi, imeendelea kutoa mafunzo katika nyanja mbalimbali za mafunzo ya usafiri wa anga, usafiri ardhini na usafiri majini kwa lengo la kuzalisha wataalam wanaotoa huduma katika Sekta ya Uchukuzi.
 
(Utendaji wa Vyuo vya Mafunzo vya Kisekta umeoneshwa katika Kitabu cha Hotuba yangu kuanzia uk.107 hadi uk. 122)

B. 2: MAFANIKIO YA MIAKA MITATU (3) YA SERIKALI YA AWAMU YA SITA KATIKA SEKTA YA UCHUKUZI

50.    Mheshimiwa Spika, napenda kulijulisha Bunge lako Tukufu kwamba miradi ya maendeleo ya sekta ya uchukuzi ni miongoni mwa miradi ambayo katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeendelea kutekelezwa bila kusuasua na kwa ufanisi mkubwa. Katika kipindi hicho, Wizara imeendelea kutekeleza miradi ya maendeleo ya kimkakati inayojumuisha: miradi ya reli; viwanja vya ndege; uboreshaji wa Kampuni ya Ndege Tanzania; ujenzi na uboreshaji wa bandari; ujenzi na ukarabati wa meli katika maziwa makuu; ufungaji wa rada za hali ya hewa; na uboreshaji wa vyuo vya mafunzo vya kisekta.

51.    Mheshimiwa Spika, kwa muhtasari yapo mafanikio mengi na makubwa yaliyopatikana ndani ya kipindi kifupi cha miaka mitatu ya Uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita. Mafanikio hayo ni pamoja na: kuongeza wigo wa Reli ya SGR kwa kuifanya kuwa ya kikanda ambapo Serikali hii imeweza kuanza mikakati ya kuifikisha reli ya SGR nje ya mipaka ya nchi; kuendelea kuboresha kwa kasi huduma za meli, ambapo baadhi ya meli zimeanza kujengwa na kukarabatiwa; kutekeleza kwa vitendo mipango ya uboreshaji wa bandari nchini kwa Serikali ya Awamu ya Sita kuendelea kushirikisha sekta binafsi; kuanzishwa kwa Mafunzo ya urubani nchini kwa mara ya kwanza tangu kupata uhuru; na kubuni na kutekeleza mikakati iliyoondoa foleni ya Malori katika Mpaka wa Tunduma.
 
(Mafanikio yalipoatikana katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita yakiwemo ya mwaka wa fecha wa 2023/24 yameoneshwa katika Kitabu cha Hotuba yangu kuanzia uk. 132 hadi 146).

B. 3: CHANGAMOTO NA MIKAKATI YA KUZITATUA


52.    Mheshimiwa Spika, Wizara ya Uchukuzi imekabiliwa na changamoto mbalimbali katika utekelezaji wa majukumu yake. Changamoto hizo na mikakati ya kuzitatua imeoneshwa katika Kitabu cha Hotuba yangu uk. 147 hadi uk. 150).

C: MPANGO NA MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA FEDHA KWA MWAKA WA FEDHA 2024/25

53.    Mheshimiwa Spika, Makadirio ya Bajeti ya Matumizi ya Kawaida na Miradi ya Maendeleo kwa mwaka 2024/25, hususan bajeti ya miradi ya maendeleo ni kwa ajili ya kutekeleza miradi ya kimkakati inayoendelea.

54.    Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2024/25, Wizara ya Uchukuzi (Fungu 62) imetengewa jumla ya Shilingi 2,729,676,417,000 kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida na Miradi ya Maendeleo. Kati ya fedha hizo, Shilingi 114,744,476,000 ni kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida na Shilingi 2,614,931,941,000 ni kwa ajili ya Miradi ya Maendeleo. Aidha, Fedha za Matumizi ya Kawaida zilizotengwa zinajumuisha Shilingi 86,661,930,000 kwa ajili ya Mishahara ya Watumishi na Shilingi 28,082,546,000 kwa ajili ya Matumizi Mengineyo. Vilevile, Fedha za Miradi ya Maendeleo zilizotengwa zinajumuisha Shilingi 2,524,369,202,000 ni fedha za ndani na Shilingi 90,562,739,000 ni fedha za nje.
 

56.    Mheshimiwa Spika, miradi ya ukrabati na Ujenzi wa Viwanja vya ndege nchini, Mradi wa Uboreshaji wa Usalama wa Usafiri katika Ziwa Victoria; Mradi wa Uboreshaji wa Bandari ya Dar es Salaam (DMGP); Mradi wa Ujenzi wa Reli ya SGR; Mradi wa Ukarabati wa Reli ya MGR; Mradi wa Ujenzi wa Chuo cha Usafiri wa Anga; Mradi wa Ukarabati wa Reli ya TAZARA; Mradi wa Ununuzi wa vifaa na Miundombinu ya Hali ya Hewa; Mradi wa uboresheji wa Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL); Mradi wa Ujenzi na Ukarabati wa Meli katika Maziwa Makuu ikiwemo Mv Liemba na Mv Muongozo; Mradi wa Ununuzi wa Mitambo ya Mawasiliano ya Ndege (VHF Navigation Aids); Mradi wa Uboreshaji wa Miundombinu na Ununuzi wa Vifaa vya Kufundishia katika Vyuo vya DMI na NIT;

(Maelezo ya kina na kazi zitakazofanyika katika mwaka wa fedha 2024/25 kwa kila mradi wa maendeleo na fedha zilizotengwa yameainishwa katika Kitabu cha Hotuba yangu kuanzia uk.153 hadi uk. 173).

57.    Mheshimiwa Spika, kazi nyingine zitakazotekelezwa na Wizara kupitia Mapato ya Ndani ya Taasisi zilizo chini yake zimeanishwa katika Kitabu cha Hotuba yangu uk.173  hadi uk. 209.

D:   SHUKRANI


58.    Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi katika kipindi cha mwaka wa fedha 2023/24. Ufanisi huo ulipatikana kutokana na ushirikiano wa wadau mbalimbali.
 
59.    Mheshimiwa Spika, ili Wizara iendelee kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi, niwaombe Waheshimiwa Wabunge, kuishauri Serikali ipasavyo katika masuala mbalimbali hususan yanayogusa maendeleo ya wananchi moja kwa moja. Pia, niwaombe wananchi na wadau wengine kuendelea kushirikiana na Serikali katika kulinda miundombinu ya usafiri na usafirishaji ambayo Serikali imekuwa ikitumia kiasi kikubwa cha fedha kuijenga na kuikarabati.

60.    Mheshimiwa Spika, kwa dhati kabisa naomba nichukue nafasi hii kuwapongeza na kutambua mchango unaotolewa na viongozi wenzangu katika kutekeleza majukumu ya Wizara, nikianza na Naibu Waziri, Mheshimiwa David Mwakiposa Kihenzile (Mb.); Katibu Mkuu, Prof. Godius Walter Kahyarara na Naibu Katibu Mkuu Dkt. Ally Saleh Possi. Pia, kipekee napenda kuishukuru Menejimenti ya Wizara, Wakuu wa Taasisi zilizo chini ya Wizara na Watumishi wote wa Wizara na Taasisi kwa jitihada zao katika utekelezaji wa Majukumu ya Wizara.

61.    Mheshimiwa Spika, Pia, naomba kutumia fursa hii kwa niaba ya Wizara kutoa shukrani zetu za dhati na kuwatambua wadau wote wa Wizara wamechangia katika utekelezaji majukumu ya Wizara. Kwa namna ya kipekee niruhusu niwatambue wafuatao: Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Anga (ICAO); Shirika la Kimataifa la Usafiri Majini (IMO); Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO); Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB); Benki ya Dunia (WB); Japan (JICA); Korea Kusini (KOICA); Ujerumani (KfW); Foreign Commonwealth and Development Office (FCDO); Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD); Jumuiya ya Nchi za Ulaya (EU); Benki ya Uwekezaji ya Ulaya (EIB); Shirika la Maendeleo la Marekani (USAID); Trade Mark Africa; Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki – EAC; Sekretarieti ya Jumuiya ya Nchi za Kusini mwa Afrika - SADC; Nchi za Urusi; Umoja wa Falme za Kiarabu-UAE; Uingereza; Marekani; Uholanzi; Japan; India; China; Denmark;
 
Korea Kusini; Ufaransa; Ubelgiji; Ujerumani na Uturuki; Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ya NSSF na PSSSF; Taasisi za fedha za CRDB, NMB, AZANIA BANK, NBC na TCB na Asasi mbalimbali za kiraia; Sekta Binafsi pamoja na wadau wengine wengi ambao sikuwataja hapa kutokana na uwingi wao.

62.    Mheshimiwa Spika, kwa namna ya kipekee niruhusu nitoe shukrani zangu za dhati kwako wewe binafsi Mhe. Spika, Mhe. Naibu Spika na kwa Wabunge wote kwa kunisikiliza.

E: MUHTASARI WA MAOMBI YA FEDHA YA WIZARA YA UCHUKUZI KATIKA MWAKA WA FEDHA 2024/25

63.    Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2024/25, Wizara ya Uchukuzi inaomba kuidhinishiwa jumla ya Shilingi 2,729,676,417,000 kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida na Utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo. Kati ya fedha hizo, Shilingi 114,744,476,000 ni kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida na Shilingi 2,614,931,941,000 ni kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

64.    Mheshimiwa Spika, pamoja na Hotuba hii, nimeambatisha majedwali mbalimbali yenye taarifa na takwimu kwa ajili ya kutoa uelewa zaidi kwa Waheshimiwa Wabunge na Watanzania kuhusu kazi zinazotekelezwa na Wizara. Naomba viambatisho hivyo vichukuliwe kama sehemu ya hotuba hii. Hotuba hii pia inapatikana katika tovuti ya Wizara (www.uchukuzi.go.tz).


65.    Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.
 

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo