Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

HOTUBA YA MHESHIMIWA PROF. MAKAME MBARAWA (MB.), WAZIRI WA UCHUKUZI, KATIKA MKUTANO MKUU WA TANZANIA ONLINE DRIVERS’ ASSOCIATION (TODA) 2026
16 Sep, 2026 Pakua

 

Jumanne, tarehe 15 Septemba 2026

CPA Dkt. Habibu Suluo, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA);

Mwenyekiti wa Tanzania Online Drivers Association (TODA);

Viongozi wa Serikali na Taasisi mbalimbali;

Wawakilishi wa LATRA, NSSF na Taasisi nyingine za Serikali;

Wamiliki na Waendeshaji wa Mifumo ya Taksi Mtandao;

Madereva wa Taksi Mtandao;

Wageni Waalikwa;

Mabibi na Mabwana.

 

Awali ya yote, namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia afya njema na kutuwezesha kukutana hapa leo. Aidha, nawapongeza viongozi na wanachama wa Tanzania Online Drivers

Association (TODA), pamoja na wadau wote, kwa kuandaa Mkutano Mkuu huu unaotupatia fursa ya kujadili maendeleo, changamoto na mustakabali wa huduma za taksi mtandao nchini.

Ndugu Washiriki,

Sekta ya uchukuzi ni kichocheo muhimu cha maendeleo ya kijamii na kiuchumi. Usafiri salama, unaopatikana kwa urahisi na wenye ufanisi huwawezesha wananchi kufikia maeneo ya kazi, biashara, elimu, afya na huduma nyingine muhimu.

Katika miaka ya hivi karibuni, matumizi ya teknolojia yameleta mabadiliko makubwa katika utoaji wa huduma za usafiri. Huduma za taksi mtandao zimeongeza urahisi wa kupata usafiri na wakati huo huo zimefungua fursa za ajira, ujasiriamali na kipato, hususan kwa vijana.

Nimeelezwa kuwa hadi sasa, LATRA imetoa leseni kwa mifumo 24 ya taksi mtandao. Hii ni hatua nzuri na inaonesha ukuaji wa sekta hii. Hata hivyo, ongezeko la mifumo lazima liende sambamba na ubora wa huduma, ushindani wenye tija, usalama wa abiria na matumizi sahihi ya teknolojia.

WAJIBU WA WAMILIKI WA MIFUMO

Nitumie fursa hii kuwaasa wamiliki na waendeshaji wa mifumo ya taksi mtandao kuendelea kujenga ushindani kwa kujitangaza, kubuni huduma mpya na kuboresha ubora wa huduma zao. Tunahitaji kuona mifumo mingi zaidi ikitumika kikamilifu na kuwapa wananchi machaguo ya huduma salama na bora.

Pamoja na hilo, Serikali inataka mifumo hii iwe salama, yenye uwazi na yenye taarifa sahihi. Ni lazima kuhakikisha kuwa gari lililosajiliwa katika mfumo ndilo linalofika na kutoa huduma kwa abiria. Si salama kwa abiria kuomba gari moja kupitia mfumo, lakini gari jingine ndilo lifike kutoa huduma.

Ninawahimiza wamiliki wa mifumo kutumia teknolojia kudhibiti tatizo hili. Kwa mfano, mifumo inaweza kuweka utaratibu wa kuhakiki gari kwa kuskani namba ya usajili au picha ya gari kabla ya dereva kuanza kutoa huduma. Teknolojia tuliyonayo itumike kulinda abiria na pia kuwatambua na kuwazuia madereva wanaokiuka taratibu.

Aidha, wamiliki wa mifumo wahakikishe mifumo yao imeunganishwa ipasavyo na mifumo ya Serikali na inawasilisha taarifa kamili na sahihi kwa wakati. Serikali inahitaji takwimu sahihi ili kufanya maamuzi, kupanga sera na kusimamia sekta hii kwa ufanisi.

MAELEKEZO KWA LATRA

Ninaielekeza LATRA kuendelea kuimarisha ufuatiliaji wa huduma za taksi mtandao na kuhakikisha changamoto zinazojitokeza zinapatiwa ufumbuzi kwa wakati.

Pamoja na hilo, LATRA ifanye ukaguzi wa mifumo ya taksi mtandao ili kujiridhisha kuwa taarifa zinazowasilishwa ni sahihi na zinaakisi huduma zinazotolewa. Mfumo wa kidijitali unapopewa leseni na Serikali, lazima uwe na uwezo wa kutoa taarifa zinazohitajika kwa usahihi na kwa wakati.

Aidha, LATRA iendelee kukutana na madereva, wamiliki wa mifumo na wadau wengine ili changamoto za sekta hii zitambuliwe na kutatuliwa bila kuathiri ubunifu, uwekezaji na ubora wa huduma. Sambamba na hilo, LATRA kufanya kikao cha pamoja kitakachowahusisha TRC, TAA na TODA, kwa lengo la kujadili na kutafuta ufumbuzi wa changamoto zinazohusiana na upakiaji wa abiria katika maeneo husika, pamoja na kuweka utaratibu unaoeleweka na unaozingatia maslahi ya wadau wote.

UBORA WA MAGARI NA WELEDI WA MADEREVA

Ndugu Madereva,

Pamoja na mafanikio yaliyopatikana, nimeelezwa kuwa ipo changamoto ya uchakavu wa baadhi ya magari yanayotumika kutoa huduma za taksi mtandao. Hili linahitaji kupewa uzito kwa sababu ubora wa gari unahusiana moja kwa moja na usalama na hadhi ya huduma inayotolewa.

Nawasihi wamiliki na madereva kuhakikisha magari yao yanakuwa katika hali nzuri, safi na salama wakati wote. Gari linalotumika lazima liwe lile lililosajiliwa katika mfumo husika.

Lakini gari zuri pekee halitoshi. Ubora wa huduma unaanza na dereva. Dereva wa taksi mtandao anatakiwa kuwa mtaalamu na mwenye maadili. Anatakiwa kumheshimu abiria, kuvaa mavazi nadhifu, kutunza usafi wa gari, kuzingatia sheria za barabarani, kuendesha kwa kujihami na kuwajibika, kuwa mwaminifu na kujali usalama wa abiria na watumiaji wengine wa barabara.

Huduma nzuri kwa mteja ni sehemu ya taaluma yenu. Abiria anapoingia katika gari lako, anatarajia usalama, heshima, uaminifu na huduma bora. Weledi wa dereva mmoja unajenga taswira ya sekta nzima; vivyo hivyo, mwenendo mbaya wa dereva mmoja unaweza kupunguza imani ya wananchi katika huduma hizi.

 

MATUMIZI YA NISHATI SAFI KATIKA HUDUMA ZA TEKSI MTANDAO

Ndugu Washiriki,

Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inaweka nishati safi, nafuu na ya kuaminika kuwa miongoni mwa vichocheo muhimu vya maendeleo ya Taifa. Hivyo, ninawahimiza madereva, wamiliki wa mifumo na wawekezaji kuongeza matumizi ya magari yanayotumia umeme, gesi asilia na nishati nyingine safi katika huduma za teksi mtandao. Hatua hii itasaidia kupunguza uchafuzi wa mazingira na kulinda mazingira yetu kwa manufaa ya kizazi cha sasa na vizazi vijavyo.

Aidha, matumizi ya nishati safi yana fursa ya kupunguza gharama za uendeshaji na hivyo kuongeza tija na faida kwa madereva. Kwa kuwa utekelezaji wa Dira 2050 unatarajia sekta binafsi kuchangia asilimia 70, ninatoa wito kwa wafanyabiashara na wawekezaji kutumia fursa hii kuwekeza katika magari yanayotumia nishati safi pamoja na miundombinu inayowezesha matumizi yake. Kwa kufanya hivyo, tutakuwa tunajenga huduma za teksi mtandao zilizo za kisasa, zenye tija na rafiki kwa mazingira.

 

WAJIBU WA ABIRIA

Ndugu Washiriki,

Usalama wa taksi mtandao pia unahitaji ushirikiano wa abiria. Nawasihi wananchi kutumia huduma hizi kwa kuzingatia tahadhari za kiusalama. Kabla ya kuingia kwenye gari, abiria ahakikishe kuwa namba ya gari, aina ya gari na taarifa za dereva zinaendana na taarifa zilizooneshwa kwenye mfumo.

Pale ambapo kuna ukiukwaji, wananchi wasikae kimya. Matukio ya dereva kufuta safari bila sababu, kuomba safari ifutwe na kufanyika nje ya mfumo, kubadilisha safari kinyume na utaratibu, au kutumia gari tofauti na lililosajiliwa, yaripotiwe kupitia mfumo husika au LATRA ili hatua stahiki zichukuliwe.

Taarifa za wananchi ni sehemu muhimu ya kujenga huduma salama na yenye uwajibikaji.

 

HIFADHI YA JAMII NA USTAWI WA MADEREVA

Ndugu Washiriki,

Tunapotaka sekta hii ikue, hatuwezi kuzungumzia teknolojia, magari na mifumo pekee. Lazima pia tuzungumzie ustawi wa dereva.

Maelfu ya Watanzania wanategemea udereva wa taksi mtandao kama chanzo cha kipato. Wengi wao ni wajasiriamali wanaogharamia magari, mafuta, matengenezo na mahitaji ya familia zao.

Kwa hiyo, tunahitaji kujenga sekta ambayo siyo tu inampa dereva kipato cha leo, bali pia inamlinda kesho. Nimefurahi kuona NSSF ikishirikiana na madereva katika kuwawezesha kupata hifadhi ya jamii.

Hifadhi hii ni muhimu kwa sababu inamwezesha dereva kupata kinga ya kijamii kulingana na taratibu na mafao yanayotolewa na Mfuko.

Ninawahimiza NSSF, LATRA, TODA na wamiliki wa mifumo kuendelea kujadiliana kuhusu namna rahisi ya kutumia teknolojia kuwawezesha madereva kuchangia hifadhi ya jamii. Lengo liwe kufanya uchangiaji kuwa rahisi na unaoendana na mazingira halisi ya kazi zao.

Tunataka dereva awe na mtazamo kwamba: “Kila ninapofanya kazi na kupata kipato, ninajiandaa pia kwa maisha yangu ya baadaye.”

 

MAANDALIZI YA AFCON

Ndugu Washiriki,

Mkutano huu pia unafanyika katika kipindi muhimu tunapoendelea na maandalizi ya shughuli zinazohusiana na AFCON. Wageni wengi watakaokuja nchini watatumia huduma mbalimbali za usafiri, ikiwemo taksi mtandao.

Hii ni fursa ya kuonesha ubora wa huduma zetu na ukarimu wa Watanzania. Dereva wa taksi mtandao atakuwa miongoni mwa watu wa kwanza kukutana na baadhi ya wageni wetu. Kwa maana hiyo, dereva atakuwa pia balozi wa Tanzania.

Ninatarajia kuona magari safi na yenye hali nzuri, madereva wenye mavazi nadhifu na mawasiliano yenye staha, huduma salama na za kuaminika, pamoja na matumizi sahihi ya mifumo ya kidijitali.

Wamiliki wa mifumo nao waanze mapema kuboresha huduma zao ili kukidhi ongezeko la mahitaji na kutoa huduma inayolingana na hadhi ya mashindano hayo.

 

Ndugu Washiriki,

Serikali itaendelea kuweka mazingira yatakayowezesha ukuaji wa huduma za taksi mtandao kwa kuzingatia usalama, ubora wa huduma, ushindani, matumizi ya teknolojia, ajira na ustawi wa madereva.

Natoa wito kwa TODA kuendelea kuwa daraja kati ya madereva, Serikali na wamiliki wa mifumo. Chama hiki kitumike kuhimiza weledi, maadili, utii wa sheria na kutatua changamoto za wanachama kwa njia ya majadiliano.

Kwa wamiliki wa mifumo, endeleeni kuwekeza na kuboresha huduma zenu. Kwa madereva, zingatieni sheria, tunzeni magari yenu na mhudumie abiria kwa heshima na weledi. Kwa wananchi, tumieni mifumo iliyoidhinishwa na toeni taarifa pale mnapobaini ukiukwaji.

Na kwa LATRA, simamieni sekta hii kwa karibu, hakikisheni mifumo inawasilisha taarifa sahihi, fanyeni ukaguzi unaohitajika na mtatue changamoto za wadau kwa wakati.

Ninaamini tukifanya hivyo tutajenga sekta ya taksi mtandao ambayo ni salama, ya kisasa, yenye ushindani na inayotoa mchango mkubwa katika ajira na maendeleo ya uchumi wa Taifa.

Kwa maneno hayo, napenda kuwapongeza TODA kwa kuandaa Mkutano Mkuu huu na kuwatakia majadiliano yenye tija na mafanikio.

Ahsanteni sana kwa kunisikiliza.

Mungu ibariki TODA.

Mungu ibariki Sekta ya Uchukuzi.

Mungu ibariki Tanzania.

Prof. Makame Mnyaa Mbarawa (Mb)

Waziri wa Uchukuzi

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo

slot gacor