Awali ya yote, namshukuru Mwenyezi Mungu, Mwingi wa rehema kwa kuendelea kutupa uhai na kutuwezesha kukutana hapa leo tukiwa wazima wa afya, watulivu na salama katika Mkoa wetu wa Dar es Salaam. Nataka kuwahakikishia kwamba Mkoa wetu wa Dar es Salaam uko shwari, shughuli zote za kijamii, kibiashara na utoaji wa huduma mbalimbali zinaendelea kutolewa kwa amani na utulivu mkubwa. Karibuni sana Dar es Salaam.
Natambua kwamba Mkutano huu wa wadau, umetokana na maombi ya watoa huduma wa teksi mtandao (Bolt na Uber) ambao nimeambiwa viongozi wao wa Afrika Mashariki na Afrika kwa ujumla wanahudhuria kikao hiki. Napenda nichukue fursa hii kuwakaribisha sana wageni hao hapa Dar es Salaam na Tanzania kwa ujumla. Napenda kuwahakikishia kwamba, Serikali ya Awamu ya Sita, chini ya uongozi mahiri wa Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ni sikivu sana na ndio maana baada ya kuwasilisha maombi yao LATRA ya kutaka kusikilizwa, fursa hiyo imetolewa kwa uwazi na bila kizuizi.
Ndugu Mkurugenzi Mkuu na Wadau wote, Kwa nafasi yangu kama Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, napenda nitumie fursa hii kuipongeza sana Serikali yetu ya Awamu ya Sita kwa jitihada kubwa za kuboresha Sekta ya Uchukuzi ikiwepo miundombinu kama barabara na reli, vyombo vya usafiri 3 (meli/boti, mabasi ya masafa kwenda mikoani na nchi jirani, teksi mtandao na hata kuruhusu bodaboda kuwa usafiri wa umma). Nchi yetu ina mtandao mkubwa sana wa barabara za lami, miji imepangika vizuri na sasa kuna uwekezaji mkubwa (mega project) unaoendelea wa usafiri wa reli kupitia Shirika la Reli Tanzania (TRC). Juhudi hizi za Serikali yetu zinachochea ukuaji wa shughuli za kiuchumi na kuongeza ajira na vipato kwa wananchi.